71. Si muhimu kujua ni lini kitatokea Qiyaamah

Leo wako watu ambao wanajaribu kuhesabu ni lini kitatokea Qiyaamah. Ni waongo na mdajali, kwa sababu hakuna mwingine anayejua ni lini Qiyaamah kitatokea isipokuwa Allaah pekee. Malaika hawajui, Mitume hawajui. Ni vipi watu hawa watajua? Ni waongo tu na madajali.

Jengine ni kwamba sio muhimu ni lini Qiyaamah kitatokea. Kilicho muhimu ni mtu kukifanyia kazi. Wakati bwana mmoja alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni lini Qiyaamah kitatokea akamjibu:

“Umekiandalia nini?”[1]

Kinachozingatiwa ni matendo, na si lini kitatokea. Hakuna manufaa yoyote kwako kujua ni lini, vinginevyo Allaah angelitubainishia. Kwa ajili hiyo washirikina, kutokana na ukubwa wao wa kumpa changamoto na kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), walimuuliza ni lini Qiyaamah kitatokea, Allaah akawajibu:

قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ

“Hakika si vyenginenyo ujuzi wake uko kwa Mola wangu.”[2]

Si kazi ya Mtume kuwafunza ni lini Qiyaamah kitatokea, kazi yake ni kuwafunza Tawhiyd, ´ibaadah na matendo mema na kuwakataza shirki, ukafiri na madhambi – hii ndio kazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ ۚ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا

“Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: “Ujuzi wake uko kwa Allaah. Na kipi kitakujulisha huenda Saa itakuwa karibu.””[3]

[1] al-Bukhaariy (2688).

[2] 7:187

[3] 33:63

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 55
  • Imechapishwa: 11/08/2021