71. Radd juu ya utata wa kumi na mbili: kujuzu kuwaomba maiti kwa kuwa watu siku ya Qiyaamah watawaomba Mitume

Washirikina wana shubuha nyingine. Nayo ni yale aliyoyasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba watu siku ya Qiyaamah watamuomba msaada Aadam, kisha Nuuh, kisha Ibraahiym, kisha Muusa kisha ´Iysa. Wote watatoa udhuru mpaka watapoishia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanasema: “Hii ni dalili ya kwamba kumuomba msaada mwengine asiyekuwa Allaah sio shirki”. Tunajibu kwa kusema: “Ametakasika yule ambaye Amezipiga muhuri nyoyo za maadui wake. Kwa hakika kuwaomba msaada viumbe kwa yale mambo wayawezayo, hatulipingi. Kama alivyosema (Ta´ala) katika kisa cha Muusa:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

”Akamsaidia yule ambaye ni katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake.” (al-Qaswasw 28 : 15)

Kama jinsi mtu anaweza kumuomba msaada mwenziwe katika vita au mfano wa hilo kwa kitu ambacho anakiweza kiumbe. Na sisi tunachopinga, ni kule kuomba msaada wa ki-´Ibaadah kama wanavyofanya katika makaburi ya mawalii au katika kutokuwepo kwao katika mambo ambayo hawayawezi yeyote isipokuwa Allaah pekee. Likithibiti hilo, kuwaomba kwao msaada Mitume siku ya Qiyaamah, wanataka kutoka kwao wamuombe Allaah awafanyie hesabu watu, ili watu wa Peponi watolewe katika kisimamo cha hali nzito.” Na hili ni jambo linajuzu duniani na Aakhirah. Ni mfano wa kumuendea mtu mwema aliye hai na aliyekaa na wewe na anayasikia maneno yako. Halafu ukamwambia: “Niombee kwa Allaah, kama jinsi Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walivyokuwa wakimuomba hilo katika uhai wake.” Ama baada ya kufa kwake, hawakumuomba kamwe kwenye kaburi lake, bali as-Salaf as-Swaalih wamekataza kwa mwenye kukusudia kumuomba Allaah kwenye kaburi lake. Vipi iweje kumuomba yeye mwenyewe?

MAELEZO

Huu ni utata miongoni mwa shubuha zao. Nao ni kwamba imethibiti katika Hadiyth Swahiyh kuhusu uombezi mkubwa – inakuja huko mbele. Watu siku ya Qiyaamah kutaporefuka kusimama kwao kwa miguu kwa miaka elfu khamsini na jua limesogezwa karibu nao na viumbe wote wamekusanywa sehemu moja kuanzia wa mwanzo mpaka wa mwisho wao katika msongamano mkubwa na jua kama tulivyosema limewekwa karibu na vichwa vyao, watapokuwa katika hali hii nzito watakumbuka uombezi wa Allaah (´Azza wa Jall) na wataona kuwa Mitume ndio wa kwanza watakaoomba mbele ya Allaah. Watamwendea Aadam kumuomba awaombee kwa Allaah ili awastareheshe kutokamana na kisimamo hichi ambapo (´alayhis-Swalaatu wa-Salaam) ataomba udhuru kutokana na kosa lililompitikia kwake pamoja na kwamba alitubia kwalo na Allaah akamsamehe. Atastahi kwa Allaah. Halafu watamwendea Nuuh, ambaye ndiye Mtume wa kwanza, naye ataomba udhuru. Kisha watamwendea Muusa na kumuomba ambapo na yeye ataomba udhuru. Halafu watamwendea ´Iysaa (´alayhis-Swalaatu wa-Salaam), ambaye ndiye Nabii wa mwisho wa Banuu Israa´iyl, naye ataomba udhuru kwa kuwa nafasi hii ni kubwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hatimaye watamwendea Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo ataenda na kusujudu mbele ya Mola wake na kumhimidi na kumsifu mpaka pale Atapoambiwa:

“Ee Muhammad, inua kichwa chako, omba utapewa na ombea utasikizwa!”[1]

Kwa kuwa hapana yeyote atakayeombea mbele Yake isipokuwa kwa idhini Yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakurupuka na kwenda moja kwa moja kuomba mbele ya Allaah. Bali ataanza kumuomba idhini Mola wake na kusujudu mbele Yake mpaka aidhinishwe. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake?” (02:255)

Atamuomba Allaah awahukumu waja Wake na awastareheshe kwa kuwaondoa katika kisimamo ambapo Allaah ataitikia uombezi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huu ndio unaitwa ´uombezi mkubwa` na ´cheo chenye kusifiwa`. Amesema (Ta´ala):

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا

“Katika usiku amka ufanye ´ibaadah – ni ziada ya Sunnah kwako wewe. Huenda Mola wako akakuinua cheo kinachosifika.” (17:79)

Bi maana atasifiwa na wa mwanzo na wa mwisho.

Waabudu makaburi wanasema kuwa hapa kuna dalili ya kujuzu kuwataka uokozi Mitume, mawalii na waja wema ilihali nyinyi mnapinga kuomba uokozi kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Vilevile wamesema kuwa haya yanathibitisha kwamba kuomba uokozi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – sawa awe hai au ameshakufa – na wengine inajuzu. Majibu juu ya haya ni kama alivyosema Shaykh. Hali hii ni kama mfano wa kumuomba mtu aliye hai na mwenye uwezo kukuombea na kuidhinisha uombezi. Kumuomba mtu katika hali ya uhai wake na kwa anachokiweza sio jambo lililokatazwa. Dalili ya hilo ni kisa cha Muusa:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

”Akamsaidia yule ambaye ni katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake.” (28:15)

Ni kama jinsi mtu anavyoweza kumuomba uokozi mwenzie vitani na kwenginepo. Hapa kuna dalili ya kwamba kumuomba uokozi aliye hai katika mambo anayoyaweza ni jambo linalojuzu. Kitachopitika kwa watu siku ya Qiyaamah ni kuomba msaada kwa waliohai na kuomba wawaombee. Inajuzu kwenda kwa mtu aliye hai na muweza anayeyasikia maneno yako na kumwambia akuombee kitu fulani. Maswahabah walikuwa wakiyafanya haya kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa uhai wake. Kitendo hichi sio shirki. Kitendo ambacho ni shirki na tunachokikaripia ni kuwaomba uokozi maiti. Haya hayana mafungamano yoyote na Hadiyth ya uombezi kwa kuwa nyinyi mnawaomba uokozi maiti na pia mnaomba uombezi kutoka kwao. Maiti hawawezi kitu. Kwa hivyo haijuzu kwa mtu kwenda kwenye kaburi na kuwaita, kuwaomba wakuombee na mengineyo. Kuna tofauti kati ya matendo ya washirikina hawa na yaliyoko katika Hadiyth Swahiyh na katika kisa cha Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa upambanuzi huu utata huu utakuwa umeondoka na himdi zote anastahiki Allaah.

[1] al-Bukhaariy (7072), Muslim (193), Ibn Maajah (4312), Ahmad (03/116) na ad-Daarimiy (52).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 112-114
  • Imechapishwa: 15/03/2017