71. Maana ya kuamini siku ya Mwisho

Imani ya kuamini siku ya Mwisho ina maana ya kuamini yale yote yatayokuwa baada ya kufa. Kuanzia maswali watayohoji Malaika wawili, adhabu au starehe za ndani ya kaburi, kufufuliwa kutoka ndani ya makaburi, kusimama kwenye kiwanja cha kukusanyika na yatayopitika baada ya hapo. Kumethibiti dalili nyingi kuhusu hayo kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Hivyo ni wajibu kuyaamini.

Kuamini siku ya Mwisho kunaingia katika kuamini mambo yaliyofichikana. Kuamini mambo yaliyofichikana ni moja katika nguzo za imani. Bali ndio imani yenyewe. Inahusiana na kumuamini Allaah kwa majina na sifa Zake. Haya ni kuamini mambo yaliyofichikana. Kwa sababu sisi hatujamuona Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kuwaamini Malaika ni katika kuamini mambo yaliyofichikana. Kuamini majini na mashaytwaan ni katika kuamini mambo yaliyofichikana. Kuamini mambo aliyoelezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo yatayopitika katika zama za mwisho ni katika kuamini mambo yaliyofichikana. Kuamini mambo yaliyowapitikia watu waliokuwa hapo kabla – japo hatukuyaona – lakini hata hivyo ni katika kuamini mambo yaliyofichikana. Mambo yaliyofichikana yanahusiana ima na mambo yaliyopita au yaliyoko huko mbele. Ni wajibu kuyaamini. Kwa ajili hii amesema (Subhaanahu wa Ta´ala) mwanzoni mwa Suurah “al-Baqarah”:

الم ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“Alif Laam Miym. Hiki ni Kitabu kisicho na shaka ndani yake ni mwongozo kwa wenye kumcha Allaah [ambao] huamini ghaibu na husimamisha swalah na hutoa sehemu katika vile Tulivyowaruzuku.” (02:01-03)

Ameanza kwa kuamini mambo yaliyofichikana.

Kwa hivyo kitendo cha kukanusha kufufuliwa kinapelekea kukanusha kumuamini Allaah (Jalla wa ´Alaa), Malaika na yale yote yasiyoonekana hapa ulimwenguni. Haya ndio maoni ya watu wa mazingira, wakanamungu na washirikina ambao wanakanusha mambo yenye kufichikana.

Kwa hivyo imani ya kumuamini Allaah kunaingia ndani yake yale yote yatayopitika baada ya kufa. Mosi katika hayo ni kuwa pale ambapo maiti atawekwa ndani ya kaburi na kufukiwa udongo na watu wakamuacha, husikia mlio wa viatu vyao. Hujiwa na Malaika wawili ambao wanamrudishia roho yake ndani ya kiwiliwili chake. Wanamkaza na kumuuliza: “Ni nani Mola Wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume Wako?”[1]

Ni maswali matatu. Akijibu majibu sahihi huokoka, kufuzu na kufaulu, na asipoweza kujibu amekula khasara na amepoteza nguvu zake bure.

[1] al-Bukhaariy (1338) na (1374) na Muslim (70) na (287)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 159-161
  • Imechapishwa: 12/01/2024