71. Kuhukumu kinyume na aliyoteremsha Allaah II

Kadhalika inahusiana na yule mwenye kusema ya kwamba ni mwenye khiyari kati ya kuhukumu kwa Shari´ah na kuhukumu kwa kanuni zilizotungwa na watu. Mtu akitaka anaweza kuhukumu kwa Shari´ah na akitaka anaweza kuhukumu kwa kanuni walizotunga watu. Huyu pia ni mwenye kuritadi kutoka katika dini ya Uislamu. Kwa sababu hakuna khiyari kuhusu kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah kwa njia ya kwamba mwenye kupenda atafanya hivo na asiyependa anaweza kuacha kufanya hivo. Bali kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah ni jambo la lazima. Amesema (Ta´ala):

وَأَنِ احْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ

“Wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Allaah na wala usifuate matamanio yao.” (al-Maaidah 05:49)

Hukumu ya Allaah ni lazima. Watu hawawezi kutengemaa isipokuwa kwa hukumu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Jambo halihusiani na kutaka au kutokutaka:

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

”Haiwi kwa muumini mwanamme na wala kwa muumini mwanamke Allaah anapohukumu na Mtume Wake amri yoyote iwe wana khiyari katika jambo lao. Anayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi kwa hakika amepotea upotofu wa wazi.” (al-Ahzaab 33:36)

Kuhukumu kwa aliyoteremsha Allaah ni aina ya ´ibaadah. Kwa hivyo ni wajibu kwa waja wote wajisalimishe juu ya hukumu ya Allaah (´Azza wa Jall) na waitakidi kwamba hakuna kitu kilicho sawa au kilicho bora kuliko hukumu Yake. Ama kuhusu yule mwenye kudhani kwamba mambo yanahusiana na khiyari na anaona kuwa watu wako huru; uhuru wa maoni, uhuru wa kufikiria na mfano wa hayo ambayo yanalinganiwa na baadhi ya mazanadiki, wanafiki, wanasekula na wengineo ambao wanasema maneno kama haya. Watu hawa wamekufuru. Kwa sababu hawatekelezi hukumu ya Allaah na wanafanya kiburi juu ya hukumu ya Allaah (´Azza wa Jall).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 101
  • Imechapishwa: 12/11/2018