71. al-Qummiy upotoshaji wake wa nane wa Aal ´Imraan

al-Qummiy amesema pindi alipokuwa akifasiri Aayah:

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ وَأَمَّا الَّذِينَ ابْيَضَّتْ وُجُوهُهُمْ فَفِي رَحْمَةِ اللَّـهِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Siku ambayo [kuna] nyuso zitakuwa nyeupe na [nyingine] zitakuwa nyeusi. Basi wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi [wataambiwa]: “Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Hivyo onjeni adhabu kwa yale mliyokuwa mkikufuru!” Na wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe [watakuwa] katika Rahmah ya Allaah na wao humo watadumu.”[1]

“´Aliy bin Ibraahiym amesema: Baba yangu amenieleza, kutoka kwa Swafwaan bin Yahyaa, kutoka kwa Abul-Jaaruud, kutoka kwa ´Imraan bin Haytham, kutoka kwa Maalik bin Dhamrah, kutoka kwa Abu Dharr aliyesema: “Pindi Aayah:

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ

“Siku ambayo [kuna] nyuso zitakuwa nyeupe na [nyingine] zitakuwa nyeusi.”

ilipoteremshwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema: “Ummah wangu siku ya Qiyaamah utanijia na bendera tano.

Bendera moja itakuja na ndama wa Ummah huu. Nitawauliza: “Mlifanya nini na vile vizito viwili baada yangu?” Watasema: “Kuhusiana na kile kikubwa, tulikipotosha na tukakitupa nyuma ya migongo yetu. Kuhusiana na kile kidogo, tulikuwa ni maadui wake, tukamchukia na tukamdhulumu.” Kisha nitasema: “Tokomeeni Motoni, hali ya kuwa ni wenye kiu na nyuso nyeusi.”

Kisha bendera nyingine ije na Fir´awn wa Ummah huu. Nitawauliza: “Mlifanya nini na vile vizito viwili baada yangu?” Watasema: “Kuhusiana na kile kikubwa, tulikipotosha, tukakivunja na tukaenda kinyume nacho. Kuhusu kile kidogo, tulikuwa ni maadui wake na tukampiga vita.” Kisha nitasema: “Tokomeeni Motoni, hali ya kuwa ni wenye kiu na nyuso nyeusi.”

Halafu bendera nyingine ije na Saamiriy wa Ummah huu. Nitawauliza: “Mlifanya nini na vile vizito viwili baada yangu?” Watasema: “Kuhusiana na kile kikubwa, tulikiasi na kukitupilia mbali. Kuhusiana na kile kidogo, tulimkosesha nusura, tukampoteza na tukafanya nae mabaya.” Kisha nitasema: “Tokomeeni Motoni, hali ya kuwa ni wenye kiu na nyuso nyeusi.”

Halafu bendera nyingine ije na mtu aliye na kifua na mkono vya kufanana pamoja na Khawaarij wa kwanza. Nitawauliza: “Mlifanya nini na vile vizito viwili baada yangu?” Watasema: “Kuhusiana na kile kikubwa tulifarikiana nacho, tukakivunja na kujiweka nacho mbali. Kuhusu kile kidogo, tulikipiga vita na kukiua.” Kisha nitasema: “Tokomeeni Motoni, hali ya kuwa ni wenye kiu na nyuso nyeusi.”

Halafu bendera nyingine itakuja na kiongozi wa wachaji Allaah, bwana wa waliopewa wasia na kiongozi wa mwanga na wasii wa Mtume wa Allaah wa Mola wa walimwengu. Nitawauliza: “Mlifanya nini na vile vizito viwili baada yangu?” Watasema: “Kuhusiana na kile kikubwa tulikifuata na kukitii. Kuhusu kile kidogo, tulimpenda, tukasimama upande wake, tukamtukuza na tukamnusuru mpaka damu yetu ikamwagwa kwa ajili yake.” Kisha nitasema: “Nendeni Peponi, mkiwa hamna kiu na mkiwa na nyuso nyeupe. Halafu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasoma:

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ وَأَمَّا الَّذِينَ ابْيَضَّتْ وُجُوهُهُمْ فَفِي رَحْمَةِ اللَّـهِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Siku ambayo [kuna] nyuso zitakuwa nyeupe na [nyingine] zitakuwa nyeusi. Basi wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi [wataambiwa]: “Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Hivyo onjeni adhabu kwa yale mliyokuwa mkikufuru!” Na wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe [watakuwa] katika Rahmah ya Allaah na wao humo watadumu.”[2]

Tazama namna ambavyo Baatwiniy huyu anavyowakufurisha Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuwatuhumu ukafiri, khiyana na upotoshaji na kuwahukumu kuingia Motoni milele.

Bendera ya kwanza, ambayo ni ya ndama, analengwa Abu Bakr na Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliowatokomeza wenye kuritadi.

Bendera ya pili, ambayo ni ya Fir´awn, analengwa ´Umar bin al-Khattwaab ambaye aliwatokomeza waabudu moto na akaujaza ulimwengu uadilifu.

Bendera ya tatu, ambayo ni ya Saamiriy, analengwa ´Uthmaan ambaye aliwatokomeza waabudu moto, ambaye wanamuonea haya Malaika wa rahmah na ambaye alifanyiwa uasi na Ibn Sabaa´ na wafuasi wake ambao ndio waasisi wa Raafidhwah.

Bendera ya nne, ambayo ni ya kiongozi wa wachaji Allaah, bwana wa waliopewa usia na kiongozi wa mwanga, analengwa ´Aliy bin Abiy Twaalib ambaye Allaah amemtakasa kutokamana na wao na ambaye aliwaua wa kale wao.

Tazama namna Raafidhwah wanavyodai kuwa wao ndio wanaishi kwa mujibu wa Qur-aan na kwamba wao ndio wanahakikisha haki za familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na kwamba wao ndio ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe na ndio wataoingia Peponi. Wanadai kwamba Aayah hii inawahusu wao tu. Sambamba na hilo Maswahabah wa Muhamamd (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wafuasi wao ndio ambao watakuwa na nyuso nyeusi; ambao wamepambana kwa Qur-aan na kuifungua miji mikubwa ya Kiislamu. Raafidhwah Baatwiniyyah hawa ndio warithi wa mayahudi pale wanaposema kuwa wao ndio wana na wapenzi wa Allaah:

وَقَالُوا لَن يَدْخُلَ الْجَنَّةَ إِلَّا مَن كَانَ هُودًا أَوْ نَصَارَىٰ

“Na walisema: “Hatoingia Peponi isipokuwa aliyekuwa myahudi” – au “mnaswara”.”[3]

Allaah (Ta´ala) akawakadhibisha kwa kuwaambia:

تِلْكَ أَمَانِيُّهُمْ ۗقُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Hivyo ndivyo wanavyotamani. Sema: “Leteni ushahidi wenu, mkiwa ni wasema kweli.”

[1] 03:106-107

[2] 03:106-107 Tafsiyr al-Qummiy (1/109-110).

[3] 02:111

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 107-108
  • Imechapishwa: 13/04/2017