70. Radd kwa njia sita juu ya shubuha iliyotangulia kutomuua mtu anayetamka Shahaadah

Shaykh (Rahimahu Allaah) amejibu utata huu kwa majibu sita ya kijumla:

Jibu la kwanza: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita watu wenye kutamka shahaadah. Aliwapiga vita mayahudi ilihali wanasema ´hapana mungu isipokuwa Allaah`. Vilevile Maswahabah waliwapiga vita watu wanaotamka shahaadah pindi kulipodhihiri kutoka kwao mambo yanayopingana na neno hili. Neno hili halikuwafaa kitu na wala haikuwa ni kizuizi cha kuwaua.

Jibu la pili: Linabainisha kujigonga kwa watu hawa pale ambapo wanasema yule mwenye kupinga swalah, zakaah, hajj na kufufuliwa wanaonelea kuwa anakufuru tofauti na yule anayepinga Tawhiyd ambapo wanaonelea kuwa hakufuru.

Jibu la tatu: Maana ya Hadiyth ya Usamaah bin Zayd sio kama walivyoelewa kwamba mwenye kutamka shahaadah anakuwa muislamu kwa hali yoyote ingawa atafanya shirki na kufuru. Maana yake ni kuwa mwenye kutamka shahaadah ni wajibu kumsalimisha mpaka kudhihiri kutoka kwake yenye kwenda kinyume na neno hili katika kufuru au shirki.

Jibu la nne: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Anapokujieni fasiki kwa khabari yoyote ile, basi hakikisheni.” (al-Hujuraat 49 : 06)

Akaamrisha (Subhaanah) kuhakikisha ikiwa na maana kuthibitisha kwa yule mwenye kutamka shahaadah. Iko wapi faida ya kuthibitisha ikiwa hauawi kabisa yule mwenye kuitamka?

Jibu la tano: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuwaua Khawaarij ilihali ni miongoni mwa watu walio na ´ibaadah nyingi, kumwogopa na kumcha Allaah. Bali walisoma kwa Maswahabah pamoja na hivyo aliamrisha wapigwe vita pindi walipofanya mambo yanayopingana na Uislamu ilihali wanatamka shahaadah, ni watu wanafanya ´ibaadah kwa wingi kukiwemo kuswali na kusoma Qur-aan.

Jibu la sita: Kisa cha Baniy al-Mustwalaq ambalo ni kabila lililoingia katika Uislamu ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), msadikishwaji, akawatumia mjumbe kuhusu uwajibu wa kutoa zakaah. Lakini hata hivyo hakuwaendea. Bali akarudi na kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa wamekataa kutoa zakaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatamani kuwapiga vita. Ndipo Allaah akateremsha:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ

“Enyi mlioamini! Anapokujieni fasiki kwa habari yoyote ile, basi hakikisheni msije mkawasibu [madhara] watu kwa ujinga mkawa juu ya mliyoyafanya ni wenye kujuta.” (49:06)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitamani kupambana nao na kuwapiga vita pamoja na kuwa wanatamka shahaadah. Kwa nini? Pindi ilipomfikia khabari ya kwamba wanakataa kutoa zakaah. Kukataa kutoa zakaah kunapingana na shahaadah. Huu ndio mukhtaswari wa majibu ya Shaykh (Rahimahu Allaah) juu ya utata huu wa khatari.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 109-111
  • Imechapishwa: 10/03/2017