70. Radd kwa makafiri wenye kupinga kufufuliwa


Kuamini siku ya Mwisho ni nguzo moja wapo ya imani. Ambaye ataikanusha amekufuru. Mwenye kusema kuwa hakuna kufufuliwa na kwamba kuna maisha ya dunia peke yake, huyu ni kafiri kwa kuwa amemkadhibisha Allaah, Mtume Wake, maafikiano ya waislamu na jambo ambalo linajulikana katika Uislamu fika. Hakuna shaka juu ya ukafiri wa anayepinga kufufuliwa. Amesema (Ta´ala):

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu, bila shaka mtafufuliwa kisha mtajulishwa kwa yale mliyoyatenda – na hayo kwa Allaah ni mepesi.”” (64:07)

Allaah alimuamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aape kwa Mola Wake ya kwamba atawafufua. Maneno Yake:

Madai maana yake ni uongo. Bi maana wamesema uongo katika maneno yao haya. Amesema (Ta´ala):

وَقَالُوا إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ

“Walisema: “Haya si chochote isipokuwa ni uhai wetu wa dunia tu na wala sisi hatutofufuliwa.”” (06:29)

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ

“Wakasema: “Huu si chochote isipokuwa ni uhai wetu wa dunia, tunakufa na tunahuika, na hakuna cha kutuangamiza isipokuwa dahari.”” (45:24)

أَيَعِدُكُمْ أَنَّكُمْ إِذَا مِتُّمْ وَكُنتُمْ تُرَابًا وَعِظَامًا أَنَّكُم مُّخْرَجُونَ هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ لِمَا تُوعَدُونَ إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ

“Je, anakuahidini kwamba nyinyi mtakapokufa mkawa mchanga na mifupa kuwa hakika mtatolewa? Mbali kabisa, mbali kabisa! Hayo mnayoahidiwa. Hakuna lolote isipokuwa tu uhai wetu wa hapa duniani tunakufa na tunahuika na wala sisi hatutofufuliwa.” (23:35-37)

Hivi ndivyo walivyokuwa wakisema makafiri tangu hapo mwanzo hadi sasa ambapo wanapinga kufufuliwa. Hawana hoja yoyote. Kinachowashangaza ni vipi watu watakufa wawe udongo halafu wafufuliwe. Wanasema kuwa ni kitu kisichowezekana kabisa:

قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ

“Akasema: “Ni nani atakayehuisha mifupa hii na hali imeshasagika na kuwa kama vumbi.”” (36:78)

Ametakasika Allaah. Hapo kabla asli ni kwamba hawakuwepo na baada ya hapo ndipo Allaah (Jalla wa ´Alaa) akawaumba. Ambaye aliwaumba mara ya kwanza ana haki zaidi ya kuwarudisha:

وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ ۖ قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ

“Akatupigia mfano akasahau kuumbwa kwake; akasema: “Ni nani atakayehuisha mifupa hii na hali imeshasagika na kuwa kama vumbi.” Sema: “Ataihuisha Yule aliyeianzisha mara ya kwanza Naye ni mjuzi wa kila [namna ya] kuumba.”” (36:78-79)

Ndani ya Qur-aan kumejaa Radd juu ya ambaye anapinga kufufuliwa.

Jengine ni kuwa lau kusingekuwa kufufuliwa na kulipwa juu ya matendo, kuumbwa kwa viumbe ingelikuwa ni mchezo. Vipi atawaumba na wafanye ima matendo mema au matendo ya kikafiri kisha wafariki na kuachwa hivi hivi? Hili halistahiki juu ya uadilifu wa Allaah (Jalla wa ´Alaa):

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ

“Je, mlidhania kwamba Sisi tulikuumbeni bila kusudio na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?” Ametukuka Allaah mfalme wa haki [ambaye] hapana mungu wa haki ila Yeye. Mola wa ‘Arshi tukufu.”” (23:115-116)

Allaah ametakasika kutokamana na hili. Ni lazima kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) awafufue watu na awapambanue waumini kutokamana na makafiri na amlipe muumini kwa imani yake na kafiri kwa ukafiri wake:

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Je, Tuwafanye wale walioamini na wakatenda mema kuwa sawa kama wenye kueneza ufisadi katika ardhi au Tuwafanye wachaji Allaah sawa na waovu?” (38:28)

Hivi kweli wote wafe na wasifufuliwe na wala wasilipwe juu ya matendo yao? Haiwezekani kabisa.

Isitoshe Allaah amewatisha makafiri, washirikina na watenda maovu ya kwamba [ipo siku] watarejea kwa Mola Wao ili awafanyie hesabu na kuwalipa. Ni jambo linalofahamisha kuwa kufufuliwa ni jambo lazima litokee na hakuna njia ya kulikwepa. Dunia ni pahali pa kufanya matendo na Aakhirah ni pahali pa malipo. Hii ni hekima ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).