7. Uwajibu wa kuingia katika Uislamu kikamilifu na kuacha mengine yote

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ

“Enyi mlioamini! Jisalimisheni kikamilifu na wala msifuate hatua za Shaytwaan – hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.” (02:208)

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُواْ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُواْ إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُواْ أَن يَكْفُرُواْ بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلاَلاً بَعِيدًا

”Je, huoni wale ambao wanadai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako na yale yaliyoteremshwa kabla yako, wanataka wahukumiane kwa Twaaghuut na hali wameamrishwa wakanushe hiyo, na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali kabisa.” (04:60)

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

“Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi huna lolote kuhusiana na wao. Hakika amri yao iko kwa Allaah, kisha atawajulisha kwa yale waliyokuwa wakifanya.” (06:159)

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ

“Siku [baadhi ya] nyuso zitang´ara na [nyingine] zitafifia. Basi wale ambao nyuso zao zitafifia [wataambiwa:] “Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa yale mliyokuwa mkikufuru.” (03:106)

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Wale walioshikamana na Sunnah na kuungana ndio nyuso zao zitang´ara na wale walioshikamana na Bid´ah na tofauti ndio nyuso zao zitafifia.”[1]

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ummah wangu utafikwa na yale yaliyowafika wana wa israaiyl kiasi cha kwamba, ikiwa kuna katika wao aliyemwingilia mama yake hadharani basi kutapatikana katika Ummah wangu ambaye atafanya vivyo hivyo. Hakika wana wa israaiyl walifarikiana katika makundi sabini na mbili na Ummah wangu utafarikiana katika makundi sabini na tatu; yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni lipi hilo?” Akasema: “Ni lile linalofuata yale mimi na Maswahabah zangu tunayofuata.”[2]

Muumini ambaye anataraji kukutana na Allaah azingatie maneno ya mkweli na msadikishwaji na khaswa pale aliposema:

“Ni lile linalofuata yale mimi na Maswahabah zangu tunayofuata.”

Ni mawaidha yaliyoje lau yatazifikia nyoyo zilizo hai!”

Ameipokea at-Tirmidhiy.

at-Tirmidhiy ameipokea tena kupitia kwa Abu Hurayrah na akaisahihisha. Lakini hata hivyo ndani yake hakukutajwa Moto, kama ilivyo katika Hadiyth ya Mu´aawiyah inayopatikana kwa Ahmad na Abu Daawuud. Humo mna:

“Katika Ummah wangu watajitokeza watu wanaopatwa na matamanio kama ambavo maradhi ya kichaa yanavompata mwenye nayo; hayatoacha mshila wala kiungo chochote isipokuwa utaingia ndani yake.”[3]

Tafsiri ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “mwenye kutaka katika Uislamu mwenendo  wa kipindi cha kikafiri” imekwishatangulia.

[1] Ibn Abiy Haatim (3/729), al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika ”Taariykh Baghdaad” (7/379) na al-Laalakaa’iy katika ”Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jama´ah” (1/72).

[2] at-Tirmidhiy (2641).

[3] Ahmad (4/102), Abu Daawuud (4597), al-Haakim (1/218) na at-Twabaraaniy (19/376). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (2).

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-ul-Islaam, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 23/10/2016