7. Tofauti ya mwanaume mtu mzima na kijana

2- Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَن يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ ۖ وَأَن يَسْتَعْفِفْنَ خَيْرٌ لَّهُنَّ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Na wanawake, ambao hawapati tena hedhi na ambao hawataraji kuolewa, basi hakuna lawama yoyote kwao wakikhafifisha kitu katika baadhi ya nguo zao, bila ya kuibusha mapambo ya kike. Na kama wakijisitiri [kwa kujifunika vyema] ni bora kwao. Na Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.”[1]

Kusudio katika Aayah hii ni kwamba Allaah anasema kuwa wanawake watu wazima, ambao hawataraji kuolewa kwa sababu wanaume hawavutiki nao kutokana na ukubwa wa umri wao, hawapati dhambi lau watakhafifisha mavazi midhali hawakusudii kujishaua kwa kuonyesha mapambo yao. Bila ya shaka Aayah haikusudii wavue mavazi kiasi cha kwamba wabaki hali ya kuwa uchi. Aayah inakusudia vazi linalowekwa juu ya kanzu na mfano wake ambalo asli linaonyesha tu uso na vitanga vya mikono. Mavazi wanayofaa kuvua ni yale yenye kuufunika mwili mzima. Kwa vile Aayah inawahusu wanawake watu wazima tu, hiyo ina maana ya kwamba wanawake vijana ambao bado wanataraji kuolewa hawana hukumu moja. Lau hukumu ingelikuwa inawagusa wote, basi kungelikuwa hakuna faida yoyote ya kuwalenga wanawake watu wazima. Vilevile isitoshe Allaah (Ta´ala) anasema:

غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ

“… bila ya kuibusha mapambo ya kike.”

Ni dalili nyingine yenye kuonesha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kijana ambaye anataraji kuolewa kujisitiri. Mwanamke anapoonyesha uso wake mara nyingi hutaka kuonesha mapambo na uzuri wake ili wanaume waweze kumsifu na mfano wa hayo. Wanawake wasiofikiria hivo ni nadra na nadra haina hukumu.

[1] 24:60

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 26/03/2017