07. Tafsiri ya maneno ya ´Umar neema ya Bid´ah iliyoje hii

Nahisi kana kwamba mnauliza vipi ninafasiri maneno ya ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) pindi alipomwamrisha Ubayy bin Ka´b na Tamiym ad-Daariy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kuwaongoza watu kwenye swalah katika Ramadhaan na kusema:

“Ni neema ya Bid´ah iliyoje hii!”[1]

Hili linaweza kufasiri kwa njia mbili:

1 – Haijuzu kwa yeyote kupingana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno ya Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy wala maneno ya mwengine yeyote. Amesema (Ta´ala):

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitina au ikawasibu adhabu iumizayo.”[2]

Imaam Ahmad amesema:

“Je, unajua fitina ni nini? Shirki. Huenda ataporudisha kitu katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingiwa  ndani ya moyo wake na kitu katika upindaji na hivyo matokeo yake akaangamia.”

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mawe yanakaribia kuwaangukia kutoka mbinguni; ninakwambieni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema na nyinyi mnasema Abu Bakr na ´Umar wamesema.”

2 – Tunajua kwa yakini kabisa ya kwamba kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa ni miongoni mwa watu wenye kuadhimisha kwa hali ya juu kabisa maneno ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa anajulikana kukomeka katika mipaka ya Allaah (Ta´ala) mpaka alikuwa ni mwenye kusifiwa kusimama kwenye maneno ya Allaah (Ta´ala). Kisa cha mwanamke aliyepingana naye wakati alipoweka kikomo cha mahari ni chenye kujulikana kwa watu wengi. Alipingana naye kwa maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا

“… na mmempa mmoja wao mirundi ya mali.”[3]

Hivyo ´Umar akawa ameacha kuweka kikomo cha mahari. Lakini hata hivyo kisa hiki usahihi wake unahitajia kuangaliwa vyema. Lakini tunachotaka kusema ni kwamba ´Umar alikuwa ni mtu mwenye kusimama katika mipaka ya Allaah (Ta´ala) na haivuki. Haimstahikii kabisa ´Umar akapingana na maneno ya kiongozi wa watu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasifu Bid´ah ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Ninakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

Kwa msemo mwingine ni kwamba Bid´ah ambayo ´Umar alikuwa akiizungumzia haiingii kwenye Bid´ah ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anamaanisha pindi aliposema:

“Ninakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alichokuwa anamaanisha ni waswaliji kukusanyika nyuma ya imamu mmoja baada ya kuwa walikuwa ni wenye kufarikiana. Kitendo chenyewe tayari kilikuwa kimeshafanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha watu nyusiku tatu za mwanzo. Usiku wa nne hakutoka kwenda msikitini. Asubuhi yake akasema:

“Nimekuoneni nini mlichofanya usiku wa jana. Kilichonizuia kuwajia ni kwamba nilichelea swalah hii isije kufaradhishwa kwenu ikawashinda.”[4]

Kusimama usiku katika Ramadhaan ni katika Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Umar aliita kitendo hichi “Bid´ah” kwa kuzingatia ya kwamba watu walikuwa ni wenye kutofautiana katika makundi mbalimbali baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuiacha. Ndipo kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) akaonelea kuwakusanya watu wote waswali nyuma ya imamu mmoja. Basi kitendo chake hichi ikawa ni Bid´ah kwa kuzingatia kule kufarikiana kwa watu hapo kabla na sio Bid´ah moja kwa moja iliyozushwa na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). Kwa sababu Sunnah hii ilikuwepo tangu zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo kitendo hichi ni Sunnah ambayo watu waliiacha tangu wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuanzia wakati wa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ndipo ikawa imerudi. Kwa ajili hiyo Ahl-ul-Bid´ah hawawezi kutumia maneno ya ´Umar ili kuzichukulia Bid´ah zao kuwa nzuri.

[1] al-Bukhaariy (2010).

[2] 24:63

[3] 04:20

[4] al-Bukhaariy (2012) na Muslim (761).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ibdaa´ fiy Kamaal-ish-Shar´ wa Khatwar-il-Ibtidaa´, uk. 9-11
  • Imechapishwa: 23/10/2016