Zakaah ni moja katika faradhi za Uislamu na nguzo ya Kiislamu muhimu baada ya Shahaadah na swalah. Uwajibu wake umetolewa dalili na Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu. Yule mwenye kupinga uwajibu wake ni kafiri aliyeritadi anayetakiwa kuambiwa atubie. Ima atubie au auawe. Asiyetoa kwa sababu ya ubakhili au kutolipa thamani yake kamilifu ni dhalimu na anastahiki adhabu ya Allaah (Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖبَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

“Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni kheri kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. Na ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi.  Na Allaah kwa myatendayo ni Mjuzi.” (03:180)

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye Allaah atampa mali na asiitolei zakaah, basi mali hiyo siku ya Qiyaamah itageuzwa kuwa joka dume lenye upara, mwenye madoa mawili machoni, atajizungusha katika mwili wa mtu huyo halafu atamkaba shingoni huku akimwambia: “Mimi ndio mali yako, mimi ndio hazina yako.”[1]

Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

“Enyi mlioamini! Hakika wengi katika marabi na watawa wanakula mali za watu kwa batili na wanazuilia [watu] njia ya Allaah. Na wale wanaorundika [hazina za] dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo. Siku [mali zao] zitakapopashwa katika Moto wa Jahannam, kisha kwa hayo vikachomwa Moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao [huku wakiambiwa]: “Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika.” (09:34-35)

Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mtu aliye na dhahabu au fedha na asiitolei zakaah isipokuwa siku ya Qiyaamah atapewa sahani za Moto zilizochochewa kwenye Moto wa Jahannam kisha apigwe nazo kwenye mbavu zake, paji lake la uso na kwenye mgongo wake. Kila zinapopoa zinatiwa moto tena kwa siku moja ambayo ni sawa na miaka 50.000 mpaka pale waja watakapohukumiwa.”[2]

Zakaah ina faida za kidini, kitabia na za kijamii ikiwa ni pamoja na:

1- Ni kutekeleza nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu ambayo juu yake kunapatikana furaha ya mja duniani na Aakhirah.

2- Inachangia kwa kumkurubisha mja kwa Mola Wake na kufanya imani yake ikazidi. Ni kama ´ibaadah nyenginezo.

3- Mtu anapata ujira mkubwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَمْحَقُ اللَّـهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ

“Allaah Huifuta  [baraka mali ya] ribaa na Huzibariki swadaqah.” (02:276)

وَمَا آتَيْتُم مِّن رِّبًا لِّيَرْبُوَ فِي أَمْوَالِ النَّاسِ فَلَا يَرْبُو عِندَ اللَّـهِ ۖ وَمَا آتَيْتُم مِّن زَكَاةٍ تُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّـهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُضْعِفُونَ

“Na mlichotoa katika [pesa za kuwakopesha watu mpate] ribaa ili kizidi katika mali za watu, basi [hicho] hakizidi kwa Allaah. Na mlichotoa katika Zakaah mnataka Uso wa Allaah, basi hao [wafanyao hivyo] ndio wenye kuzidishiwa.” (30:39)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mwenye kutoa tende moja kutoka kwenye pato la halali isipokuwa Allaah anaichukua kwenye Mkono Wake wa kulia ambapo inakua kwenye Kitanga cha Mwingi wa rehema mpaka inakuwa kubwa mfano wa jibali.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

4- Allaah anafuta madhambi kwa zakaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swadaqah inafuta madhambi kama jinsi maji yanavyozima moto.”[4]

Makusudio ya swadaqah hapa ni zakaah na ile ya kujitolea.

Baadhi ya faida za kitabia ni zifuatazo:

1- Mtoa zakaah anakuwa ni mmoja katika watoaji na wakarimu.

2- Zakaah inamfanya yule mtoaji kusifika kuwa na huruma na upole kwa ndugu zake mafukara – Mwingi wa huruma huwarehemu wale wenye kurehemu.

3- Jinsi atakavyozidi kuwasaidia waislamu kimali na kimwili ndivyo jinsi atavyozidi kupendwa na kutukuzwa na ndugu zake waislamu.

4- Zakaah inamtwaharisha yule mtoaji na ubakhili na uchoyo. Allaah (Ta´ala) amesema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

“Chukua katika mali zao Swadaqah, uwatwaharishe na uwatakase kwazo.”  (09:103)

Baadhi ya faida za kijamii ni zifuatazo:

1- Zakaah inatatua haja za mafukara. Mafukara ndio wengi katika jamii.

2- Zakaah inafanya waislamu kuwa na nguvu na inawanyanyua. Ndio maana Jihaad katika njia ya Allaah ni moja katika wale wenye kustahiki kupewa zakaah.

3- Zakaah inaondosha chuki na vifundo vinavyokuwa kwenye vifua vya mafukara na masikini. Mafukara wakiona jinsi wale matajiri wanavyoburudika pasina kunufaika na kitu katika vile walivyo navyo huenda wakaanza kuwa na uadui na chuki dhidi ya wale matajiri kwa vile hawajali haki zao na wanapuuzia haja zao. Hisia hii huisha na nafasi yake kunaingia mapenzi na mahaba pale ambapo matajiri wanawapa kitu katika mali zao mara moja kwa mwaka.

4- Zakaah inafanya baraka ya mali kuzidi kuongezeka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swadaqah haifanyi mali ikapungua.”[5]

Bi maana ikiwa swadaqah inafanya mali kupungua kiidadi, basi baraka yake haipungui na kuongezeka huko mbeleni. Uhakika wa mambo ni kwamba Allaah huweka badala yake nyingine na kumbarikia mali yake.

5- Sura ya mali inazidi kupanuka. Pindi mali inapotolewa sura zake zinazidi kupanuka na watu wengi wananufaika nayo. Kinyume na pale ambapo inakuwa ni yenye kuzunguka kati ya matajiri.

Faida zote hizi ni zenye kuonesha kuwa zakaah ni kitu cha kidharurah kutokana na maslahi kwa mtu mwenyewe na kwa jamii. Kutakasika kwa mapungufu ni Kwako Allaah, Mjuzi wa yote, Mwingi wa hekima.

Zakaah ni wajibu kwa mali maalum ikiwa ni pamoja vilevile na dhahabu na fedha zinapofikisha kile kiwango cha wajibu [niswaab]. Kiwango cha wajibu cha dhahabu ni gramu 85 au pesa ilio sawa na thamani hiyo. Kiwango cha wajibu cha fedha ni gramu 595 au pesa ilio sawa na thamani hiyo. Zakaah ilio ya wajibu katika dhahabu na fedha ni 2.5%. Haijalishi kitu sawa dhahabu au fedha ikiwa ni pesa, vipande vipande au [dhahabu za] kujipamba. Kutokana na hilo ni wajibu kwa mwanamke kutolea zakaah vipodozi vyake vya dhahabu na fedha vikifikisha kiwango cha wajibu, sawa ikiwa anavivaa au ameviazima. Ushahidi wa hilo ni zile dalili za jumla zinazowajibisha zakaah katika dhahabu. Dalili hazijafafanuliwa. Vilevile kuna dalili maalum zenye kuonesha kuwa ni wajibu vipodozi kuvitolea zakaah  hata kama vinatumiwa kwa kuvaliwa. Kwa mfano ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa kuna mwanamke alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwenye mkono wa msichana wake kulikuwa na cheni mbili kubwa. Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Unaitolea zakaah?” Akasema: “Hapana.” Akasema: “Utafurahia Allaah akikupa cheni mbili za Moto kwazo?” Akazitupa na kusema: “Nimezitoa kwa ajili ya Allaah na Mtume Wake.”[6]

Ibn Hajar amesema katika “Buluugh-ul-Maraam” kuwa imepokelewa na watatu na kwamba mlolongo wa wapokezi wake una nguvu. Kile kilicho na usalama ndio bora zaidi.

Zakaah ni wajibu vilevile katika bidhaa za biashara ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya biashara kama majengo, magari, mifugo, vitambaa na vinginevyo. Ni wajibu kuvitolea 2.5%. Baada ya mwaka mmoja bidhaa hizi zitapigiwa hesabu na kutolewe thamani sawa na 2.5%. Haijalishi kitu sawa ikiwa itakuwa ni chini, zaidi au sawa sawa na ile bei aliyonunua. Hata hivyo sio wajibu kutolea zakaah vile vitu anavyotumia mwenyewe au anavyokodisha katika majengo, magari, vifaa na vinginevyo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Sio wajibu kwa muislamu kumtolea zakaah mtumwa na farasi wake.”[7]

Pamoja na hivyo ni wajibu kutolea zakaah kodi na vipodozi vya dhadhabu na fedha baada ya kueneza mwaka.

[1] al-Bukhaariy (8403).

[2] Muslim (987).

[3] al-Bukhaariy (1410) na Muslim (1014).

[4] at-Tirmidhiy (2616) ambaye ameisahihisha, Ibn Maajah (9373) na Ahmad

[5] Muslim (2588), at-Tirmidhiy (2029) na Ahmad (2/235).

[6] Abu Daawuud (1563), at-Tirmidhiy (638) na an-Nasaa’iy (2479).

[7] al-Bukhaariy (1464).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 15-18
  • Imechapishwa: 05/06/2017