7. Mateso Makkah na uhamiaji wa Abyssinia

Maudhi ya washirikina yalipozidi na kuwapa mitihani waumini zaidi na zaidi. Walikuwa wanaweza kuwafunga kamba, kuwaweka kwenye jua kali na kuweka jiwe kubwa juu ya vifua vyao wakati wa jua kali. Wanapoacha hawawezi hata kukaa kutokana na ukali wa maumivu. Walikuwa wanaweza kuwalazimisha wasema al-Laat ni mungu wao badala ya Allaah ambapo wanaitikia kwa kutenzwa nguvu. Wanapopita kwa al-Ju´l wanasema kuwa ni mungu wao badala ya Allaah ambapo wanaitikia kwa kutenzwa nguvu.

Adui khabithi wa Allaah Abu Jahl ´Amr bin Hishaam alipita wakati mama yake na ´Ammaar Sumayyah, mume wake na mvulana wake wanaadhibiwa. Akachukua mkuki na kumdunga nao kwenye tupu yake akafa. Allaah amuwie radhi yeye, mvulana wake na mume wake!

Wakati Abu Bakr as-Swiyddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) alipokuwa anapita karibu na mtumwa anayeadhibiwa anamnunua kutoka kwa mmiliki wake na kumwacha huru. Baadhi ya watu hao ni Bilaal, mama yake Hammaamah, ´Aamir bin Fuhayrah, Umm ´Abs, Zinniyrah, an-Nahdiyyah, msichana wake na wajakazi wa Banuu ´Adiyy ambao ´Umar alikuwa akiwaadhibu kabla ya kuingia katika Uislamu. Baba yake Abu Quhaafah alifikia kumwambia: “Ee mwanangu! Ninaona jinsi unavyowaacha huru watumwa. Ni kwa nini usiwaache huru watumwa wenye nguvu ambao watakulinda?” Abu Bakr akasema: “Nataka ninalolitaka.” Imesemekana kuwa Aayah hizi zimeteremka kwa mnasaba wake:

وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ مَا لِأَحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَىٰ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ

“Na ataepushwa nao [Moto huu] mwenye taqwa – ambaye anatoa mali yake kujitakasa, na hali hakuna mmoja yeyote yule aliyemfanyia fadhila yoyote hata amlipe, isipokuwa kwa kutaka Uso wa Mola wake Aliyetukuka. Na bila shaka atakuja kuridhika.” (92:17-21)

Wakati mitihani ilipozidi ndipo Allaah akawapa idhini wahamie Abyssinia iliokuwa magharibi mwa Makkah. Kati ya nchi hizo mbili kulikuwa sahara ya Sudan na bahari nyekundu. Mtu wa kwanza kuhama kwa ajili ya dini yake ilikuwa ni ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh). Alikuwa pamoja na mke wake Ruqayyah, msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Watu wengine wakamfuata. Maoni mengine yanasema kuwa mtu wa kwanza kuhama ilikuwa ni Abu Haatib bin ´Amr bin ´Abdi Shams bin ´Abdi Wadd bin Naswr bin Maalik. Kisha baada ya hapo akatoka Ja´far bin Abiy Twaalib na wengine (Radhiya Allaahu ´anhum). Walikuwa karibu wanaume 80.

Miongoni mwa watu waliohama ambao Muhammad bin Ishaaq ametaja ilikuwa ni Abu Muusa ´Abdullaah bin Qays al-Ash´ariy. Sijui ni kipi kilichomfanya kufanya hivo. Jambo hili liko wazi kabisa kwa wale ambao sio wajuzi zaidi kama yeye. Kwa ajili hiyo al-Waaqiydiy na wasomi wengine wa wasifu wamekataa hilo na kusema kuwa Abu Muusa alihama kutoka Yemen kwenda Abyssinia na akajiunga na Ja´far. Ni kitu kimetajwa kwa uwazi kabisa katika al-Bukhaariy na Muslim kupitia upokezi wake (Radhiya Allaahu ´anh).

Wakati wahamaji walipofika Ashamah katika ufalme wa an-Najaashiy akawatunza na kuwakirimu. Kwake walikuwa na usalama. Baada ya muda Quraysh walipofikiwa na khabari wakamwagiza ´Abdullaah bin Abiy Rabiy´ah na ´Amr bin al-´Aasw. Walikuwa na mazawadi kutoka katika mji wao kumpelekea an-Najaashiy ili awarudishe kwao. an-Najaashiy akawakatalia hilo. Hivyo wakawageukia majenerali wake kwa kutarajia kwamba watawafanyia uombezi. Mwishoni wakasema kumwambia: “Watu hawa wanamtukana ´Iysaa vibaya sana na wanasema kuwa ni mja!” Waislamu wakapelekwa katika kikao chake wakiongozwa na Ja´far bin Abiy Twaalib (Radhiyha Allaahu ´anh). Akasema: “Mnasemaje juu ya haya yanayosemwa na watu hawa kuhusu ´Iysaa?” Ndipo Ja´far akaanza kusoma Suurat Maryam. Alipomaliza an-Najaashiy akachukua kijiti kwenye ardhi kisha akasema: “Hakusema zaidi ya yaliyomo katika Tawrat wala kijiti hiki.” Halafu akasema: “Nendeni. Mko na usalama katika nchi yangu. Anayewatukaneni itamgharimu.” Akamwambia ´Amr na ´Abdullaah: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba lau mgenipa mlima wa dhahabu nisingeliwasalimisha kwenu!” Baada ya hapo akaamrisha wachukue mazawadi yao. Wakarudi na mkia ulio kati ya miguu.

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 18/03/2017