69. Tashahhud ya kwanza na vikao vyake

Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumaliza Rak´ah ya pili alikuwa akikaa katika Tashahhud. Swalah ikiwa ya Rak´ah mbili, kama vile Fajr, basi hukaa kama vile anavyokaa kati ya Sujuud mbili[1]. Hivyo ndivyo alivyokuwa akikaa kwenye Tashahhud ya kwanza katika zile swalah zilizo na Rak´ah tatu na Rak´ah nne[2].

Vivyo hivyo alimuamrisha yule mtu aliyeswali kimakosa na kumwambia:

“Unapokaa katikati ya swalah basi tulizana, tandaza paja lako la kushoto kisha usome Tashahhud.”[3]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kipenzi changu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinikataza kuchutama kama achutamavyo mbwa.”[4]

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akikataza kizingiti cha shaytwaan.”[5]

Alipokuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akikaa katika Tashahhud alikuwa akiweka kitanga chake cha mkono wa kulia juu ya paja lake la kulia[6] na kitanga cha mkono wake wa kushoto[7] juu ya paja lake la kushoto[8].

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiweka kisugudi chake cha mkono wa kulia[9] juu ya paji lake la kulia[10].

Alimkataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwanaume mmoja ambaye alikuwa ameketi katika swalah hali ya kuegemea mkono wake wa kushoto na akamwambia:

“Hiyo ni swalah ya mayahudi.”[11]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Usiketi namna hiyo. Hivyo huketi wale wanaoadhibiwa.”[12]

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Hivyo ndivyo huketi wale walioghadhibikiwa.”[13]

[1] an-Nasaa’iy (1/173) kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[2] al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[3] Abu Daawuud na al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.

[4] at-Twayaalisiy, Ahmad na Ibn Abiy Shaybah. Abu ´Ubaydah na wengineo wamesema kuhusu kuhusu al-Iq´aa´:

“Ni pale mtu anapogandamiza kikalio chake kwenye ardhi, anaweka muundi wake wima na mikono mbele yake kama afanyavyo mbwa.”

Hii sio ile al-Iq´aa´ inayokubalika katika Shari´ah baina ya Sujuud mbili, kama ilivyotangulia.

[5] Muslim, Abu ´Awaanah na wengineo. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (316).

[6] Katika upokezi mwingine imekuja “kwenye goti lake la kulia”.

[7] Katika upokezi mwingine imekuja “kwenye goti lake la kushoto”.

[8] Muslim na Abu ´Awaanah.

[9] Inavyoonekana ni kwamba hakutenganisha viwiko vyake na mbavu zake, kama alivyoweka wazi hilo Ibn-ul-Qayyim katika “Zaad-ul-Ma´aad”.

[10] Abu Daawuud na an-Nasaa’iy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[11] al-Bayhaqiy na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Hiyo na Hadiyth ya kufuata zimetajwa katika “al-Irwaa´” (380).

[12] Ahmad na Abu Daawuud kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.

[13] ´Abdur-Razzaaq. Swahiyh kwa mujibu wa ´Abdul-Haqq katika ”al-Ahkaam” (1284 kwa uhakiki wangu).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 136-137
  • Imechapishwa: 20/08/2017