69. Sura ya tisa: Mtazamo wa kilimwengu na uharibifu unaopatikana ndani yake

Kuna mitazamo miwili ya maisha:

1- Mtazamo wa kilimwengu.

2- Mtazamo ambao ni sahihi.

Mitazamo yote miwili ina athari zake. Mtazamo wa kilimwengu:

Maana yake ni kwamba fikira za mwanadamu ziwe zimefupika katika kupata starehe za harakaharaka za hapa duniani na matendo yake yote zimefungana na mipaka hiyo na fikira yake haivuki yaliyo nyuma ya hayo katika mambo kutazama mwisho wa mambo yatavyoishia, haitendei kazi, hatilii umuhimu jambo lake na wala hatambui kuwa Allaah ameifanya dunia hii kuwa ni shamba kwa ajili ya Aakhirah ambapo akaifanya dunia hii kuwa ni nyumba ya kutenda na akaifanya Aakhirah ni nyumba ya malipo. Yule mwenye kuitumia dunia yake kwa matendo mema basi atafuzu duniani na Aakhirah. Mwenye kuipoteza dunia yake basi Aakhirah yake pia itapotea:

الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ

“Hiyo ndiyo khasara ya wazi.”[1]

Allaah hakuiumba dunia hii kwa ajili ya mchezo. Bali ameiumba kwa sababu ya hekima kubwa. Amesema (Ta´ala):

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Ambaye ameumba kifo na uhai ili akujaribuni ni nani kati yenu mwenye matendo mazuri zaidi.”[2]

إِنَّا جَعَلْنَا مَا عَلَى الْأَرْضِ زِينَةً لَّهَا لِنَبْلُوَهُمْ أَيُّهُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Hakika Sisi tumefanya vilivyoko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwajaribu nani kati yenu mwenye matendo mazuri zaidi..”[3]

Amefanya (Subhaanah) katika dunia hii kuwepo kwa starehe za harakaharaka na mapambo ya waziwazi katika mali, watoto, vyeo, ufalme na ladha mbalimbali zisizojua yeyote isipokuwa Allaah.

Miongoni mwa watu – na ndio wengi – wako ambao wamelifupiza jicho lao katika yale mambo yake ya waziwazi, fitina zake na wakazistarehesha nafsi zao kwayo na wala hawakuzingatia siri yake. Matokeo yake wakashughulishwa na kuitafuta, kuikusanya na kustarehe nayo kuliko kufanyia kazi yaliyo baada yake. Bali huenda hata wakapinga kuwepo kwa maisha mbali na haya. Amesema (Ta´ala):

وَقَالُوا إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ

“Walisema: “Haya si chochote isipokuwa ni uhai wetu wa dunia tu na wala sisi hatutofufuliwa.”[4]

Allaah amewatishia wale wenye mtazamo huu katika maisha yao. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا وَرَضُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاطْمَأَنُّوا بِهَا وَالَّذِينَ هُمْ عَنْ آيَاتِنَا غَافِلُونَ أولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمُ النَّارُ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ

“Hakika wale wasiotaraji kukutana Nasi na wakaridhika na uhai wa dunia na wakakinaika nayo na wale ambao wanaghafilika na Aayah Zetu – hao makazi yao ni Moto kwa waliyokuwa wakiyachuma.”[5]

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لاَ يُبْخَسُونَ أُوْلَئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الآخِرَةِ إِلاَّ النَّارُ وَحَبِطَ مَا صَنَعُواْ فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

”Anayetaka maisha ya dunia na mapambo yake, basi Tutawalipa kikamilifu matendo yao humo nao hawatopunjwa humo – [lakini] hao ndio wale ambao hawatokuwa na chochote katika Aakhirah isipokuwa Moto, yataharibika yale yote waliyoyafanya ndani yake [hapa duniani] na yatabatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.”[6]

Matishio haya yanawagusa watu wenye mitazamo hii. Ni mamoja wanaofanya hivo ni miongoni mwa wale wanaofanya matendo ya Aakhirah na huku wanakusudia maisha ya dunia, kama wanavofanya wanafiki au wale wenye kujionyesha kwa matendo yao, au ni miongoni mwa makafiri ambao hawaamini kufufuliwa na hesabu, kama ilivo hali ya watu wa kipindi cha kikafiri, madhehebu angamivu katika wabepari, wakomunisti, wanasekula wakanamungu ambao hawakujua nafasi ya maisha. Jicho lao kuitazama halivuki jicho la mnyama, bali wao wamepotea zaidi. Kwa sababu wao zimefunikwa akili zao, bidii zao zimekhasirika na wamepoteza wakati wao katika jambo ambalo halitodumu kwao, wao hawatobaki kwa ajili yake na wala hawakufanyia kazi mwisho wao unaowasubiri na hawana njia yoyote ile ya kuukwepa. Mnyama hauna mwisho unaomsubiri na wala hauna akili za kulifikiria jambo hilo tofauti na watu hao. Ndio maana amesema (Ta´ala) juu yake:

أَمْ تَحْسَبُ أَنَّ أَكْثَرَهُمْ يَسْمَعُونَ أَوْ يَعْقِلُونَ ۚ إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ ۖ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا

“Je, unadhania kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Wao si chochote isipokuwa kama wanyama, bali wao wamepotea zaidi njia.”[7]

Allaah amewasifu watu wa mitazamo hii kutokuwa na elimu. Amesema (Ta´ala):

وَعْدَ اللَّـهِ ۖ لَا يُخْلِفُ اللَّـهُ وَعْدَهُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ يَعْلَمُونَ ظَاهِرًا مِّنَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ عَنِ الْآخِرَةِ هُمْ غَافِلُونَ

“Ahadi ya Allaah [na] Allaah hakhalifu ahadi Yake, lakini watu wengi hawajui. Wanajua yaliyo dhahiri ya uhai wa dunia, lakini wao wameghafilika kutokamana na Aakhirah.”[8]

Wao, ijapokuwa ni watu wenye uzowefu katika mambo ya kuvumbua na kuunda, ni wajinga wasiostahiki kusifiwa elimu. Kwani elimu zao hazikuwavukisha mambo ya waziwazi ya maisha ya duniani. Isitoshe elimu hii ni pungufu ambayo wenye nayo hawastahiki kupewa sifa hii tukufu. Wenye kuitwa “wanachuoni” ni wale wenye kumtambua na kumcha Allaah. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

“Hakika wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni wanazuoni.”[9][10]

[1] 22:11

[2] 67:02

[3] 18:07

[4] 06:29

[5] 10:07-08

[6] 11:15-16

[7] 25:44

[8] 30:06-07

[9] 35:28

[10] Nzuri kupitia zengine.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 133-135
  • Imechapishwa: 06/04/2020