69. Radd juu ya utata wa kumi na moja: Mtume (صَلَّى اللّٰهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) alimkemea Usaamah kwa kumuua mtu aliyetamka Shahaadah

Washirikina wana shubuha nyingine. Wanasema: “Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkemea Usaamah pindi alipomuua mtu aliyesema: “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Na akamwambia:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hapana mungu isipokuwa Allaah?”[1]

Amesema vilevile:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”.”[2]

Na kuna Hadiyth zingine zinazozungumzia kumsalimisha yule mwenye kuitamka. Makusudio ya hawa wajinga ni kwamba mwenye kuitamka hawezi kukufuru wala hauawi, walau atafanya yakufanya.

Ndio maana inatakiwa kusemwa kuambiwa washirkina hawa wajinga: “Ni jambo linalojulikana ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita mayahudi na akawafunga ilihali na wao wanasema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”. Na Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliwapiga vita Baniy Haniyfah nao wanashuhudia “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah”, wanaswali na kudai Uislamu. Hali kadhalika wale aliowaunguza ´Aliy bin Abiy Twaalib kwa moto. Na wajinga hawa wanakubali kuwa yule mwenye kupinga kufufuliwa anakufuru na kuuawa, hata kama atasema “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, na kwamba yule mwenye kupinga chochote katika nguzo za Uislamu amekufuru na kuuawa, hata ikiwa ataitamka [Shahaadah]. Vipi basi isimfai ikiwa kapinga kitu katika mambo ya matawi, lakini imfae akipinga Tawhiyd ambayo ni msingi na asli ya dini ya Mitume? Lakini maadui wa Allaah hawakufahamu maana ya Hadiyth.

Ama Hadiyth kuhusu Usaamah, alimuua mtu ambaye alidai Uislamu kwa sababu alidhani ya kwamba anadai Uislamu kwa khofu tu ya kuuliwa na mali yake. Na mtu akidhihirisha Uislamu, basi ni wajibu kumwacha mpaka kubainike yanayokhalifu hilo. Allaah ameteremsha juu ya hilo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Mnapotoka katika njia ya Allaah hakikisheni.” (an-Nisaa´ 04 : 94)

Yaani “thibitisheni”. Aayah inatoa dalili ya kwamba ni wajibu kumsalimisha mpaka mtu athibitishe. Baada ya muda kukibainika kutoka kwake yanayokhalifu Uislamu, anauawa, kwa Kauli Yake (Ta´ala) “hakikisheni”. Na lau ingelikuwa hauawi kabisa akiitamka, basi kuhakikisha kungekuwa hakuna maana yoyote. Hali kadhalika Hadiyth nyingine na mfano wake. Maana yake ni haya tuliyoyataja; ya kwamba mwenye kudhihirisha Tawhiyd na Uislamu basi ni wajibu kumsalimisha isipokuwa ikibainika kutoka kwake yanayotengua hilo. Dalili ya hili ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hapana mungu isipokuwa Allaah?””[3]

Amesema vilevile:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”.”[4]

ndiye huyo huyo aliyesema kuhusu Khawaarij:

“Popote mtapokutana nao waueni. Lau nitakutana nao, nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad”[5],

pamoja na kuwa ni katika watu wenye kufanya ´Ibaadah sana, Tahliyl[6] na Tasbiyh[7]. Mpaka hata Maswahabah walikuwa wakizidharau swalah zao wakilinganisha na zao. Pia wamejifunza elimu kutoka kwa Maswahabah, hata hivyo haikuwafaa kitu “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, wala wingi wa ´Ibaadah wala kudai kwao Uislamu pindi ilipodhihiri kwao kukhalifu kwao Shari´ah. Hali kadhalika kuhusu tuliyoyataja kupigwa vita mayahudi na Maswahabah kuwapiga vita Baniy Haniyfah. Hali kadhalika alitaka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwavamia Baniy al-Mustwalaq baada ya kuambiwa na mtu kutoka katika wao ya kwamba wamekataa kutoa zakaah, mpaka Allaah akawa ameteremsha:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Anapokujieni fasiki kwa khabari yoyote ile, basi hakikisheni.” (al-Hujuraat 49 : 06)

Hata hivyo ikaonekana ya kwamba mtu huyo amewasemea uongo[8]. Yote haya yanaonesha dalili ya kwamba makusudio ya Mtume (Swalla Allaah ´alayhi wa sallam) kwa Hadiyth ambazo wanatumia kama hoja ni haya tuliyoyataja.

MAELEZO

Huu ni utata wa washirikina wenye kuyaabudu makaburi wanaodai Uislamu na wanadai kuwa kuabudu makaburi, kuwataka uokozi maiti, kuwaomba walioko mbali na kuwaomba watatue matatizo ya kwamba mambo haya hayadhuru na wala hayamtoi mtu katika Uislamu maadamu mwenye kufanya hayo anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Wanatumia dalili kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkemea Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ´anhumaa) pindi alipomuua mshirikina mmoja aliyedhihirisha Uislamu na kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`. Pamoja na hivyo Usaamah akamuua baada ya hapo alipodhani kuwa amesema hivo kwa ajili tu ya kujisalimisha na kuuawa. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amemkemea. Wametumia dalili kisa hiki ya kwamba yule mwenye kutamka shahaadah ni muislamu pasi na kujali zile aina mbalimbali za shirki kubwa atazofanya zinazoitengua. Vilevile wametumia dalili kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”.”[9]

Wamesema kuwa hii ni dalili ya kwamba yule mwenye kutamka maneno haya hauawi hata kama atafanya atayoyafanya katika aina mbalimbali za shirki katika ´ibaadah kwa maiti, makaburi na akawatekelezea ´ibaadah wasiokuwa Allaah midhali anasema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`.

Kwa kifupi huu ndio utata wao. Ni utata wa khatari ambao ukisikiwa na mjinga pengine ukamuathiri na khaswa ukizingatia kuwa wanautumia kwa njia danganyifu ambapo wanataja Hadiyth Swahiyh lakini hata hivyo wanazitumia mahali kusipokuwa pake.

[1] al-Bukhaariy (6478), Muslim (96), Abu Daawuud (2643) na Ahmad (05/200).

[2] al-Bukhaariy (385), at-Tirmidhiy (2608), an-Nasaa´iy (3967), Abu Daawuud (2641) na Ahmad (03/225).

[3] al-Bukhaariy (6478), Muslim (96), Abu Daawuud (2643) na Ahmad (05/200).

[4] al-Bukhaariy (385), at-Tirmidhiy (2608), an-Nasaa´iy (3967), Abu Daawuud (2641) na Ahmad (03/225).

[5] al-Bukhaariy (6995), Muslim (1064), an-Nasaa´iy (2578), Abu Daawuud (4764), Ibn Maajah (169) na Ahmad (03/68).

[6] Kusema ”Laa ilahaa illa Allaah”.

[7] Kusema: ”Subhaan Allaah”.

[8] Tazama Tafsiyr ya Ibn Kathiyr (04/210-211).

[9] al-Bukhaariy (2786), Muslim (21), at-Tirmidhiy (2606), an-Nasaa´iy (3971), Abu Daawuud (2640), Ibn Maajah (3928) na Ahmad (01/11).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 107-109
  • Imechapishwa: 09/03/2017