69. Mwenye kuamini kuwepo kwa hukumu bora kuliko ya Mtume


2- Suala la pili: Mwenye kuitakidi ya kwamba hukumu isiyokuwa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  ni bora kuliko hukumu yake,  amekufuru. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwenye kufikisha kutoka kwa Allaah. Hukumu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni hukumu iliotoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِتَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ بِمَا أَرَاكَ اللَّـهُ

”Hakika Sisi tumekuteremshia Wewe Kitabu kwa haki ili uhukumu baina ya watu kwa aliyokuonyesha Allaah.” (an-Nisaa´ 04: 105)

وَأَنِ احْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ

”Wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Allaah.” (al-Maaidah 05:49)

Mtume (´alayhis-Salaam) anahukumu kwa hukumu ya Allaah na kwa anayomuonyesha Allaah. Allaah hakumwambia ahukumu kwa yale anayoona yeye. Bali amemwambia ahukumu kwa yale aliyomuonyesha Allaah. Kwa hivyo ni wajibu kuikubali hukumu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kujisalimisha na kunyenyekea kwayo. Amesema (Ta´ala):

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

”Basi Naapa kwa Mola wako kwamba hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana baina yao, kisha kusipatikane katika nyoyo zao uzito wowote katika uliyohukumu na wajisalimishe hali ya kujisalimisha kikweli” (an-Nisaa´ 04:65)

Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anahukumu kwa hukumu ya Allaah (´Azza wa Jall), ijapokuwa anaweza kukosea katika baadhi ya Ijtihaad, basi inapokuwa hivo Allaah hanmkubalii kosa. Bali anambainishia usawa. Haijuzu kupingana na hukumu yake. Amesema (Ta´ala):

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

”Haimstahikii muumini mwanamme na wala muumini mwanamke pindi Allaah na Mtume Wake wanapohukumu amri yoyote wakawa na khiyari katika amri yao.  Yule anayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika amepotea upotofu wa wazi.” (al-Ahzaab 33:36)

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni. Mcheni Allaah! Hakika Allaah ni mkali wa kuadhibu.” (al-Hashr 59:07)

Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Wahy kutoka kwa Allaah. Sunnah inaifasiri Qur-aan na ndio Wahy wa pili baada ya Qur-aan na ndio chanzo cha pili baada ya Qur-aan. Kwa hiyo ni wajibu kuzikubali kama inavyokubalika Qur-aan. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Enyi mlioamini! Msitangulize mbele ya Allaah na Mtume Wake. Mcheni Allaah! Hakika Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote).”(al-Hujuraat 49:01)

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.” (an-Najm 53:03-04)

Kwa hiyo ni wajibu kwa muislamu kuzipokea hukumu kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hatakiwi kuhukumu kitu kwa mtazamo wake tu usiokuwa na dalili au kwa kile anachokiona yeye ni kizuri. Bali apokee kutoka katika Kitabu cha Allaah  na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Haijuzu vilevile kwake kutanguliza kauli ya fulani juu ya kauli ya Allaah na kauli yake Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika mwenye kufanya hivyo, basi atakuwa ametangulia mbele ya Allaah na Mtume Wake.

Vilevile haijuzu kuzitumia akili na fikira zake au akakubali maoni ya mwengine kwa yale yanayoenda kinyume na Qur-aan na Sunnah.

Ni wajibu kuamini ya kwamba hukumu ya Allaah na Mtume Wake ndio haki na ya sawa na kwamba zinazokwenda kinyume nazo ni batili. Hii ni ´Aqiydah ambayo muislamu anatakiwa kuamini.

Mwenye kuitakidi kwamba hukumu za viumbe ni bora kuliko hukumu ya Allaah (´Azza wa Jall) au hukumu isiyokuwa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni bora kuliko hukumu yake, basi atakuwa amekufuru. Hili ni miongoni mwa mambo yanayotengua Uislamu wa mtu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 99-100
  • Imechapishwa: 12/11/2018