69. Mtume kabla ya Qiyaamah


Amesema (Ta´ala):

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً ۖ فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا ۚ فَأَنَّىٰ لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ

“Je, basi wanangojea nini isipokuwa Saa iwafikie ghafla? Na kwa hakika zimekwishakuja alama zake. Basi kutoka wapi kutawafaa kukumbuka kwao itakapowajia?”[1]

Bi maana alama zake. Saa imegawanyika alama aina tatu: ndogondogo, za kati na kati na kubwakubwa. Baadhi ya alama zimekwishatokea. Ikiwa ni pamoja na kutumilizwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika yeye ni Nabii wa Saa na amesema:

“Mimi na Saa tumetumilizwa kama viwili hivi” na akaashiria kidole kirefu na kidole cha shahada[2].

Baadhi ya alama za kati na kati zimekwishatokea. Zingine ziko njiani. Zilizobaki ni zile alama kubwakubwa. Itakapoanza moja basi zingine zitafuatana. Miongoni mwa alama hizi kubwakubwa ni kuchomoza jua upande wa magharibi na kuchomoza kwa mnyama ambao utaweka alama kwenye mapaji ya nyuso za watu wote ili kila mmoja aweze kujua dini ya mwenzake.

Alama nyingine ni kuchomoza kwa Ya´juuj na Ma´juuj. Ni watu ambao wanakaribia kutofahamu kitu na ambao wataeneza ufisadi ardhini. Hapo kabla watu walimuomba Dhul-Qarnayn awatenganishe na ulimwengu. Kutokana na ule uwezo na nguvu aliyompa akafanikiwa kuwajengea ukuta wasiyoweza kuubomoa unaowatenganisha na watu wote. Ukuta huu utaendelea kuweko kwa kipindi fulani mpaka pale ambapo Ya´juuj na Ma´juuj watafanikiwa kuubomoa:

فَمَا اسْطَاعُوا أَن يَظْهَرُوهُ وَمَا اسْتَطَاعُوا لَهُ نَقْبًا قَالَ هَـٰذَا رَحْمَةٌ مِّن رَّبِّي ۖ فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ رَبِّي جَعَلَهُ دَكَّاءَ ۖ وَكَانَ وَعْدُ رَبِّي حَقًّا وَتَرَكْنَا بَعْضَهُمْ يَوْمَئِذٍ يَمُوجُ فِي بَعْضٍ ۖ وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَجَمَعْنَاهُمْ جَمْعًا

“Basi hawakuweza kuukwea, na wala hawakuweza kuutoboa. [Dhul-Qarnayn] akasema: “Hii ni rehema kutoka kwa Mola wangu. Basi itakapokuja ahadi ya Mola wangu ataufanya upasukepasuke na ahadi ya Mola wangu daima ni ya kweli na siku hiyo tutawaacha wasongamane wao kwa wao na litapulizwa baragumu tutawakusanya wote katika mkusanyo mmoja.”[3]

Hatimaye Allaah atawatokomeza na kuwasalimisha waislamu kutokamana na wao, kama ilivyotajwa katika Hadiyth.

[1] 47:18

[2] al-Bukhaariy (4936).

[3] 18:97-99

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 53-54
  • Imechapishwa: 11/08/2021