1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila mmoja ni mchungi na kila mmoja ataulizwa juu ya kile alichokichunga. Kiongozi ni mchungi juu ya wananchi wake na ataulizwa juu yao. Mwanamme ni mchungi juu ya watu wa nyumbani kwake na ataulizwa juu yao. Mwanamke ni mchungi juu ya nyumba ya mume wake na ataulizwa juu yake.”

2 – Sunnah, kupitia kwa mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), imesema wazi kwamba kila mchungi ataulizwa juu ya kile alichokichunga. Kwa ajili hiyo ni lazima kwa kila yule ambaye ni mchungi alazimiane na kile anachokichunga. Wachungi wa watu ni wanazuoni. Wachungi wa wafalme ni akili. Wachungi wa waja wema ni kule kumcha kwao Allaah. Mchungi wa mwanafunzi ni mwalimu. Mchungi wa mwana ni baba yake. Mlinzi wa mwanamke ni mume wake. Mlinzi wa mtumwa ni bwana wake. Kila mchungi wa watu ataulizwa juu ya kile alichokichunga.

3 – Wafalme wanalo jukumu kubwa juu ya kile wanachokichunga. Wao ndio wenye kuwachunga. Wao ndio wachungi wakubwa kutokana na kwamba mara nyingi yanafanyiwa kazi maamrisho yao. Wasipozingatia nyakati zao na wakawapuuza wananchi wao basi wao wanaangamia na kuwafanya wengine pia wakaangamia. Pengine ulimwengu mzima ukaangamia kwa sababu ya kuharibika mfalme mmoja. Nguvu za mfalme ni zenye kuendelea muda wa kuwa yuko na wasaidizi wanaomtii. Wasaidizi hawatomtii pasi na waziri. Hayo hayatopatikana mpaka waziri awe mwenye mapenzi na mwenye kuwatakia watu mema. Hayo hayatopatikana kwa waziri mpaka awe mwenye kujichunga na machafu na mwenye maono. Watu hawa hawawezi kuongozwa pasi na pesa. Pesa haiwezi kupatikana isipokuwa mpaka wananchi watengemae. Wananchi hawatengemai mpaka waongozwe kwa uadilifu. Kwa njia moja ni kama vile utawala hauwepo isipokuwa kwa kulazimiana na uadilifu. Kwa njia nyingine ni kwamba unaondoka kukiwepo dhuluma.

4 – Ni wajibu kwa mfalme kuwaangalia wafanyikazi wake ili awe akitambua wema wa anayefanya wema na uovu wa anayefanya maovu.  Wakati mfalme hajui yale yanayofanywa na wafanyikazi wake basi hawezi kutekeleza uadilifu.

5 – Haitakiwi kwa mtawala kuwa mwenye furaha sana kwa wananchi wake wala kuyafanya kidogo. Kufanya kwa wingi jambo hilo kutampelekea katika upumbavu. Kufanya kwa uchache jambo hilo kutampelekea katika kujikweza na kiburi. Haitakiwi kwa mfalme kukasirika, kwa sababu nguvu zake zimetandaa juu ya haja yake. Haitakiwi kwa mfalme kusema uwongo, kwa sababu hakuna yeyote awezaye kumtenza nguvu kitu. Haitakiwi kwa mfalme kuwa bakhili, kwa sababu hana udhuru wowote kamaa yuko na mali na nafasi. Haitakiwi kwa mfalme kuwa mwenye chuki, kwa sababu anatakiwa kuwa mtukufu zaidi kutokamana na kuadhibu. Mtawala bora ni yule asiyekuwa na kiburi.

6 – Mtawala ni kama moto. Akiwa mdogo, hakuna faida yake. Akiwa mkubwa, madhara yake yanakuwa makubwa zaidi. Mtawala bora ni yule ambaye ni kama mvua inayonufaisha mazingira yake na si kama moto ambao unachoma mazingira yake.

7 – Mtawala mwadilifu ni bora kuliko mvua kubwa. Mtawala dhalimu ni bora kuliko fitina itakayodumu. Watu wanahitaji zaidi mtawala mwadilifu kuliko wakati wenye rutuba.

8 – al-Ahnaaf bin Qays amesema:

“Uhusiano wa mtawala kwa wananchi ni kama uhusiano wa roho kwa mwili ambao hauwezi kuishi isipokuwa kwayo na uhusiano wa kichwa kwa viungo vya mwili ambavyo hawezi kubaki pasi nacho.”

9 – Ni lazima kwa mtawala kabla ya kila kitu aanze kumcha Allaah na atengeneze hali zake za kisiri kati yake na Muumba Wake. Kisha afikirie lile jukumu ambalo Allaah amempa juu ya ndugu zake ambalo Amemnyanyua yeye juu yao. Anapaswa kutambua kuwa ataulizwa juu ya mambo yao yote makubwa na madogo. Anapaswa kutambua kwamba atafanyiwa hesabu juu ya mambo yao yote makubwa na madogo. Halafu ateue waziri mwema, mwenye busara, mwenye kujichunga na machafu na mwenye kuwatakia watu mema. Anatakiwa kuwa na wafanyikazi wema na waliopevuka. Anapaswa kuwa na wasaidizi waliojificha na watumishi wanaojulikana.

10 –  Mtawala anatakiwa kuwashurutishiwa wafanyikazi wake kumcha Allaah na kumtii. Pesa ichukuliwe kutoka katika vyanzo halali pekee na baadaye igawanywe kwa wale wanaoistahiki. Mtawala anatakiwa kuhakikisha hazina ya mali hakuingizwi ndani yake hata nafaka moja ya haramu kwa njia ya uonevu, dhuluma, ujambazi, uporaji, wizi au hongo. Mtawala ndiye atakayeulizwa kwa kila kidogo kinachoingizwa ndani yake. Atafanyiwa hesabu kwa kila nafaka iliyo ndani yake. Kisha asitumie mali hiyo kwa jambo jengine isipokuwa yale ambayo Allaah ameyaamrisha katika Suurah “al-Anfaal[1].

[1] Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا غَنِمْتُم مِّن شَيْءٍ فَأَنَّ لِلَّـهِ خُمُسَهُ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا يَوْمَ الْفُرْقَانِ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ ۗ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

”Tambueni kwamba ghanima yoyote mnayoipata, basi humusi yake ni ya Allaah na Mtume na jamaa wa karibu na mayatima na masikini na wasafiri ikiwa nyinyi kweli mumemuamini Allaah na yale tuliyoyateremsha kwa mja Wetu siku ya upambanuzi; siku yaliyokutana makundi mawili [katika vita vya Badr]. Na Allaah juu ya kila jambo ni Muweza.” (08:41)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 268-271
  • Imechapishwa: 08/09/2021