68. Msingi wa tatu ni kumjua Mtume Muhammad (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa tatu – ni kumjua Mtume wenu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)

Alikuwa ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim. Haashim alikuwa anatokamana na [kabila la] Quraysh, Quraysh ni kutokamana na waarabu na waarabu ni kutokamana na kizazi cha Ismaa´iyl, mtoto wa Ibraahiym al-Khaliyl – swalah na salamu bora kabisa ziwe juu yake na juu ya Mtume wetu. Aliishi kwa umri wa miaka sitini na tatu, arubaini kabla ya utume na ishirini na tatu kama Nabii na Mtume. Alipewa unabii kwa [kupewa Suurah] “Iqra´” na akapewa utume kwa “al-Muddaththir”. Mji wake ni Makkah.

MAELEZO

Msingi wa tatu – Bi maana katika misingi mitatu ambayo ni wajibu kwa muislamu kuijua. Misingi hii ni mtu kumjua Mola Wake, dini yake na Mtume wake. Kumeshatangulia maneno juu ya mja kumjua Mola Wake na dini yake. Ama kuhusu kumjua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumekusanya mambo matano:

1- Kumjua kikoo. Ni katika watu wenye ukoo bora zaidi. Alikuwa ni katika ukoo wa Haashim, kabila la Quraysh na kutoka katika waarabu. Anaitwa Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim.

2- Kujua umri wake, mahali alipozaliwa na nchi aliyohamia. Haya yamebainishwa na Shaykh pale aliposema:

“Aliishi kwa umri wa miaka sitini na tatu, arubaini kabla ya utume na ishirini na tatu kama Nabii na Mtume. Alipewa unabii kwa [kupewa Suurah] “Iqra´” na akapewa utume kwa “al-Muddaththir”. Mji wake ni Makkah.”

Alizaliwa Makkah na akabaki huko kwa muda wa miaka khamsini na tatu. Halafu akahamia al-Madiynah ambapo aliishi miaka kumi. Akaaga dunia Rabiy´ al-Awwal miaka kumi na moja baada ya kuhama.

3- Kujua maisha yake ya kiutume ambapo ilikuwa kwa miaka ishirini na tatu. Alianza kuteremshiwa Wahy pindi alipokuwa na miaka arobaini. Mmoja katika washairi amesema:

Alifikisha miaka arobaini na hapo ndipo

Likaangaza kutoka kwake jua la kinabii katika Ramadhaan

4- Ni kwa kitu gani alikuwa Nabii na Mtume? Alikuwa Nabii wakati alipoteremshiwa maneno Yake (Ta´ala):

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ

“Soma! Kwa jina la Mola wako aliyeumba – amemuumba mtu kutokana na pande la damu linaloning’inia! Soma! Na Mola wako ni Mkarimu kabisa, ambaye aliyefunza kwa kalamu, amemfunza mtu yale asiyoyajua!” (al-´Alaq 96 : 01-05)

Kisha akawa Mtume pindi alipoteremshiwa maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye! Na Mola wako mtukuze! Na nguo zako zitwaharishe! Na masanamu epukana nayo! Na wala usifanye wema kwa ajili ya kutaraji kukithirishiwa! Na kwa ajili ya Mola wako subiri!” (al-Muddaththir 74 : 01-07)

Ndipo akasimama (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka nje, akaonya na akasimama kwa amri ya Allaah (´Azza wa Jall).

Tofauti kati ya Mtume na Nabii, kama wanavyosema baadhi ya wanachuoni, ni kwamba Nabii ni yule mtu ambaye ameteremshiwa Wahy kwa Shari´ah, pasi na kuamrishwa kuifikisha. Ama Mtume ni yule ambaye ameteremshiwa Wahy kwa Shari´ah na akaamrishwa kuifikisha na kuitendea kazi. Hivyo basi, kila Mtume ni Nabii na si kila Nabii ni Mtume.

5- Ametumwa kwa kitu gani na kwa nini? Ametumwa kwa kumpwekesha Allaah (Ta´ala) na Shari´ah Yake ilio na kufanya yale yaliyoamrishwa na kuacha yaliyokatazwa. Ametumwa kama rehema kwa walimwengu. Ametumwa ili awaondoe watu kutoka katika giza la shirki, kufuru na ujinga na kuwapeleka katika nuru ya elimu, imani na upwekeshaji. Yote haya ili waweze kupata msamaha na radhi za Allaah na kuokoka na adhabu na hasira Zake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 122-123
  • Imechapishwa: 03/06/2020