Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba kuridhia misiba ni jambo gumu zaidi kuliko subira. Imeshatangulia ya kwamba subira ni jambo gumu kabisa juu ya nafsi. at-Tirmidhiy amepokea ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ujira mkubwa unatokamana na majaribio makubwa. Allaah akiwapenda watu basi huwapa mtihani. Anayeridhia, hupata radhi Zake, na anayekasirika, hupata hasira zake.”

Wanachuoni kutoka katika madhehebu ya Imaam Ahmad na wengineo wametofutiana kama ni wajibu au imependekezwa kuridhia misiba. Mja anaweza kuwa na subira juu ya msiba lakini asiuridhie. Kuridhia ni ngazi iliyo juu kuliko kuvumilia. Lakini wamekubaliana juu ya uwajibu wa kuwa na subira na wakatofautiana juu ya uwajibu wa kuridhia. Kushukuru ni ngazi iliyo juu zaidi kuliko kuridhia. Mwenye kushukuru anauona ule msiba kama neema na hivyo anaushukuru.

ash-Shaafi´iy amepokea kutoka kwa ´Abdul-Waahid bin Zayd aliyesema:

“Kuridhia ndio mlango mkubwa wa Allaah, Pepo ya dunia na mataa ya wenye kuabudu.”

Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ

“Hausibu msiba wowote [unaokusibuni] isipokuwa kwa ni idhini ya Allaah. Na yeyote anayemuamini Allaah, huuongoza moyo wake.” 64:11

´Alqamah bin Abiy Waqqaas amesema:

“Inahusiana na msiba unaomfika mtu akajua kuwa unatoka kwa Allaah na hivyo akaridhia na kujisalimisha nao.”

´Umar bin Dharr amesimulia kuwa Umm-ud-Dardaa´ alikuwa akisema:

“Wanaoridhia mipango ya Allaah ni wale wenye kuridhia yale yote Allaah aliyowapangia. Siku ya Qiyaamah watakuwa na ngazi Peponi ambazo hata mashahidi watazitamani.”

Sulaymaan bin al-Mughiyrah amesema:

“Allaah (Ta´ala) alimteremshia Daawuud (´alayhis-Salaam): “Hutokutana na Mimi ukiwa na kitendo ambacho kitanifanya Mimi kuwa radhi sana na wewe na kukufutia dhambi zako kama kuridhia mipango Yangu. Na wala hutokutana na Mimi na kitendo ambacho ni dhambi kubwa na kitachonifanya kukukasirikia sana kama kiburi. Ee Daawuud! Nakutahadharisha na kiburi!”

Abu Sulaymaan ad-Daaraaniy amesema:

“Nataraji kuwa nimepewa kuridhia. Nikiingizwa Motoni kwa hilo nitakuwa mwenye kuridhia.”

Ibn Abiy Dunyaa amepokea kupitia kwa Ibn Zayd aliyesema:

“´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) alimwangalia ´Adiyy bin Haatim na akamuona kuwa ni mwenye huzuni. Akamwambia: “Ee ´Adiyy! Ni kwa nini uko na huzuni?” Akasema: “Vipi nisiwe na huzuni ilihali watoto wangu wameuawa na jicho langu limetobolewa?” ´Aliy akamwambia: “Ee ´Adiyy! Yule mwenye kuridhia mipango ya Allaah analipwa thawabu. Asiyeridhia mipango ya Allaah Allaah anayabatilisha matendo yake.”

Abu ´Abdillaah al-Baraa-iy amesema:

“Mwenye kutunukiwa kuridhia basi amefikia daraja iliyo juu kabisa.”

Mtu akiuliza ni vipi mtu ataridhia misiba, jibu ni kuwa hakuna mgongano kati ya yale maumbile yanayofanya mtu kuikimbia misiba na moyo unaoridhia makadirio. Tunaridhia mipango ya Allaah, lakini pengine tusipende kile kilichopangwa. Kulisemwa kuambiwa mtu mmoja mwema kwamba mtoto wake ameuawa katika njia ya Allaah. Akaanza kulia. Akaulizwa ni vipi anaweza kulia ilihali mtoto wake amekufa akiwa shahidi, akasema:

“Kinachoniliza najiuliza ni vipi alikuwa radhi na Allaah (´Azza wa Jall) pindi upanga ulipomchukua.”

Ibn-ul-Jawziy amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wake kupitia kwa ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Ee Allaah! Lau ningejua kuwa Utaniridhia nikikonga moto mkubwa na kujitupa ndani yake basi ningefanya hivo. Lau ningejua kuwa Utaniridhia nikijitupa ndani ya maji nikazama ningefanya hivo.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 152-154
  • Imechapishwa: 06/11/2016