68. Kitenguzi cha nne: Mwenye kuamini kwamba kuna uongofu bora kuliko wa Mtume

Shaykh na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La nne

Mwenye kuitakidi ya kwamba uongofu usiyokuwa wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni bora kuliko uongofu wake au ya kwamba hukumu ya asiyekuwa yake ni bora kuliko hukumu yake; kwa mfano kama wale wanaofadhilisha hukumu ya Twawaaghiytjuu ya hukumu yake, huyo ni kafiri.

MAELEZO

Amesema (Rahimahu Allaah):

“Kichenguzi cha nne miongoni mwa vitenguzi vya Uislamu, mwenye kuitakidi ya kwamba uongofu usiyokuwa wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni bora kuliko uongofu wake au ya kwamba hukumu ya asiyekuwa yake ni bora kuliko hukumu yake; kwa mfano kama wale wanaofadhilisha hukumu ya Twawaaghiyt juu ya hukumu yake, huyo ni kafiri.” Hapa kuna mambo mawili:

1- Suala la kwanza: Mwenye kuitakidi ya kwamba kuna uongofu kinyume na uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ni bora kuliko uongofu wake. Uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ile dini na njia aliyopita juu yake wakati wa kulingania kwake kwa Allaah, kufunza kwake na tabia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mtu mwenye uongofu bora kabisa. Kama alivyosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika maneno bora kabisa ni ya Kitabu cha Allaah na uongofu bora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[1]

Yeye ndiye mwenye uongofu bora kabisa inapokuja katika kutangamana kwake na watu wengine na wale anaowalingania. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitangamana nao kwa matangano yaliyo bora kabisa. Amesema (Ta´ala):

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ

”Hakika wewe bila shaka una tabia nzuri mno.” (al-Qalam 68:04)

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ

”Basi ni kwa rehema kutoka kwa Allaah umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelikukimbia. Hivyo basi wasamehe na waombee msamaha na washauri katika mambo.”(Aal ´Imraan 03:159)

Hii ndio ilikuwa tabia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa akiwafunza watu kwa njia bora kabisa. Hakuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitumia ususuwavu au ghadhabu wakati wa kufundisha. Kama ilivyo katika kisa cha yule mtu aliyeingia na akakojoa msikitini ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha wamwache mpaka amalize kukojoa kisha akaamrisha pamwagiwe juu yake maji, kisha baa ya hapo ndipo akamwita na kumwambia:

“Misikiti haikujengwa kwa lengo hilo. Hakika si vyengine isipokuwa imejengwa kwa ajili ya kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall).”[2]

Kuna matukio mengine vilevile ambayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakutana nayo katika kutangamana na watu katika kuwafunza akitumia njia ilokuwa bora kabisa na uongofu uliokuwa mkamilifu zaidi.

Miongoni mwa hayo ni alikuwa ni mwenye ustahamilivu juu ya maudhi ya watu na wala hakasiriki pindi anapokosewa katika haki yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa akimfanyia upole yule mwenye kukosea. Lakini inapokiukwa mipaka ya Allaah, hapo ndipo alikuwa anaghadhibika kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall). Hakuwa ni mwenye kughadhibika kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, isipokuwa alikuwa anaghadhibika kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall). Hili ni jambo limethibiti katika Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[3].

Hali kadhalika alipomjia mtu anayemdai deni lake ambapo akamkasirikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno makali. Maswahabah wakataka kumshambulia ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia:

“Mwacheni! Hakika mwenye haki yake ana lakusema.”

Halafu akaamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) apewe bora kuliko kile alichokuwa anamdai Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akampa zaidi. Kisha akasema:

“Mbora wenu ni yule ambaye katika nyinyi analipa kwa ubora zaidi.”[4]

Vivyo hivyo uongofu wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kuntangamana kwake na watu wa nyumbani kwake. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitangamana na watu wa nyumbani kwake kwa njia iliokuwa bora kabisa. Amesema:

“Mbora wenu ni yule mbora kwa familia yake na mimi ni mbora wenu kwa familia yangu.”[5]

Hili ni jambo linalotambulika katika maisha yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuna yeyote awezaye kuwa sawa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika uongofu wake. Vipi basi atakuwa ni mbora kuliko yeye? Ambaye atadai kwamba kuna yeyote ambaye ni mbora kuliko Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu basi amekufuru kufuru kubwa inayomtoa katika Uislamu.

[1] Ameipokea Muslim (867).

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (219) na Muslim (285) na (284).

[3] Ameipokea al-Bukhaariy (6126) na Muslim (2327).

[4] Ameipokea al-Bukhaariy (2306) na (Muslim (1601).

[5]  Ameipokea Ahmad (74029) na at-Tirmidhiy (3895).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 97-99
  • Imechapishwa: 12/11/2018