68. Faida zinazopatikana katika kisa cha Banuu Israa´iyl na baadhi ya Maswahabah

Lakini kisa hiki kinafidisha ya kwamba Muislamu wa kawaida, bali hata mwanachuoni, anaweza kutumbukia katika aina ya shirki bila ya kujua. Kinafidisha kujifunza na kuwa makini na kujua ya kwamba maneno ya mjinga “Tunajua Tawhiyd” ni katika ujinga mkubwa na hila za shaytwaan. Kinafidisha pia ya kwamba Muislamu mwenye kufanya Ijtihaad endapo atatamka neno la kufuru pasi na kujua. Akizinduliwa juu ya hilo na akutubia papo hapo, hakufuru, kama walivyofanya Banuu Israaiyl na wale waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na kinafidisha pia ya kwamba hata kama hakukufuru, anatakiwa kukemewa kwa makemeo makali kabisa, kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Katika kisa hiki kuna faida zifuatazo:

Faida ya kwanza: Kutahadhari na shirki na kwamba inaweza kujipenyeza kati ya waislamu kwa njia ya kufuata kichwa mchunga na kujifananisha na makafiri:

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi mungu kama walivokuwa hawa wana mungu!” (07:138)

“Tufanyie Dhaat Anwaatw kama wao walivyo na Dhaat Anwaatw.”

Katika hayo kuna matahadharisho kutokamana na kuwapaka mafuta makafiri na kutahadhari na ile fitina inayoweza kutokamana na hilo. Katika hayo ni kuabudu makaburi ambayo wameyazua na wakapewa mtihani nayo na wakawa ni wenye kuwalingania watu kwayo. Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyeyavunja masanamu kwa mkono wake, akaudhiwa na akafikia mpaka kutupwa ndani ya moto kwa sababu ya kukemea shirki anasema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ

“Uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu. Mola wangu! Hakika hao wamepoteza wengi sana katika watu.” (14:35)

Wapo wengine wanaokosoa muqararati za Tawhiyd katika masomo, mashule na vyuo vikuu na kusema kwamba hakuna haja ya misongamano hii ya muqararati ya Tawhiyd na kwamba watu ni waislamu na kwamba watoto wamezaliwa katika maumbile na kwamba wanafunzi wanaweza kujifunza Tawhiyd katika mazingira ya kijamii na maneno yao mengine ya kipuuzi. Ukiwauliza wanaosema hivo jambo moja lepesi kuhusu Tawhiyd hawatokujibu jibu la sawa.Alichelea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtihani juu ya nafsi yake na akachelea mtihani juu ya kizazi chake. Vipi mjinga anaweza kuthubutu kusema kuwa yeye anaweza kujifunza Tawhiyd mnamo dakika tano? Yeye anaonelea muhimu ni kutafiti mambo ya siasa, kuwatukana watawala na kujua mambo ya kisasa (Fiqh-ul-Waaqi´) kama wanavyosema. Maana yake ni kwamba watu wafuatilie matukio ya kimataifa, mambo waliyohalalisha na wajishughulishe nayo badala ya kujifunza dini.

Faida ya pili: Hii ni kanuni kubwa, nayo ni kwamba mwenye kutamka neno la kufuru ilihali ni mjinga hajui kisha akazinduliwa na akawa ametubia papo hapo hakufuru. Dalili ya hilo ni kisa cha Banuu Israa´iyl pamoja na Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baadhi ya Maswahabah pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao hawakukufuru. Lakini hata hivyo ni lazima kutimie sharti hizi mbili:

1- Awe amesema maneno haya kwa ujinga na hakuyakusudia.

2- Atubie papo hapo na aachane na jambo hili ikimbainikia kuwa ni kufuru. Maneno aliyoyasema hayatomdhuru.

Haya ndio majibu ya shubuha zao zilizotangulia ambapo wanasema kuwa Banuu Israa´iyl hawakukufuru na kwamba Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakukufuru kwa maneno haya. Tunawajibu kwa kuwaambia ya kwamba hawakukufuru kwa kuwa waliyasema kwa ujinga na walipozinduliwa wakayaacha na kutubu kwa Allaah (´Azza wa Jall) tofauti na nyinyi mnazinduliwa usiku na mchana lakini bado mnaendelea kuyaabudu makaburi, watu wema na wala hamtaki kusikia yale mnayoambiwa kutokana na kiburi na ukaidi.

Faida ya tatu: Kisa hiki kinafidisha kuwa asiyekufuru kwa neno la kufuru pindi atapolisema kwa ujinga asichukuliwe wepesi. Kinyume chake inatakiwa kumkemea kwa ukali kama ambavyo Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyowakemea watu wake na kama ambavyo vilevile Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakemea Maswahabah wake waliosema maneno hayo. Mtu afanye hivo kwa lengo la kukemea na kutahadharisha ili watu wajiepushe na kutahadhari nayo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 105-106
  • Imechapishwa: 16/02/2017