3 – Ni haramu kwa mwanamke mwenye kukaa eda ya kufiliwa mambo matano yanayoitwa ´al-Ihdaad`.

La kwanza: Manukato kwa aina zake zote. Asijitie manukato kwenye mwili wake, nguo zake na wala asitumie vitu vyenye harufu nzuri. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

“Wala asiguse manukato.”

La pili: Mapambo kwenye mwili wake. Ni haramu kwake kujipaka hina na aina zote za kujipamba kama mfano wa kupaka wanja na aina mbalimbali ya rangi zinazotiwa mwilini. Isipokuwa akilazimika kupaka wanja kwa ajili ya matibabu na si kwa ajili ya kujipamba. Katika hali hii inafaa kwake kupaka wanja usiku na akapangusa mchana. Hakuna neno pia akajitibu macho kwa kitu kingine mbali na wanja miongoni mwa vitu visivyokuwa na mapambo.

La tatu: Kujipamba kwa nguo zilizoandaliwa kwa ajili ya kujipamba katika nguo zilizotengenezwa kwa ajili ya kujipamba. Avae nguo zisizokuwa na mapambo. Hailazimu rangi maalum. Atavaa nguo vile ilivyo desturi za watu.

La nne: Kuvaa mapambo kwa aina zake zote mpaka pete.

La tano: Kulala kwenye nyumba nyingine ambayo amefariki mume wake na yeye yuko humo. Asiibadilishe isipokuwa kwa udhuru wa Kishari´ah. Asitoke kwa ajili ya kumtembelea mgonjwa, rafiki wala ndugu. Inafaa kwake kutoka mchana kwa ajili ya haja zake za kilazima. Hazuiliwi na yasiyokuwa mambo haya matano katika yale aliyohalalisha Allaah. Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Hadyi an-Nabawiy”:

“Hazuiliwi kukata kucha, kunyofoa nywele za kwapa, kunyoa nywele ambazo imependekezwa kuzinyoa, kuoga kwa mkunazi na kuchanua.”[1]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Inafaa kwake kula vile vyote alivyomhalalishia Allaah kama mfano wa matunda na nyama. Kadhalika kunywa vile alivyohalalishiwa kula.” Mpaka aliposema: “Si haramu kwake kufanya kazi miongoni mwa makazi yaliyohalalishwa kutia taraza nguo, kushona, kufuma na kazi nyenginezo wanazofanya wanawake. Inajuzu pia yale yote aliyohalalishiwa katika isiyokuwa eda kama mfano kuzungumza na wale wanaume ataohitajia kuzungumza nao midhali ni mwenye kujisitiri na kadhalika. Haya aliyotaja ndio Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliyokuwa wakifanya wake wa Maswahabah wanapofariki waume zao.”[2]

Yale yanayosemwa na wale wasiokuwa na elimu kwamba aufunike uso wake na mwezi, asipande juu ya paa la nyumba, asizungumze na wanaume na afunike uso wake mbali na Mahram zake, yote haya hayana msingi – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] (05/507).

[2] (34/27,28).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 114-116
  • Imechapishwa: 27/11/2019