67. Utafiti juu ya Qadhwaa´ na Qadar V


Kuna masuala: Wale wanaopinga Qadhwaa´ na Qadar wahukumiwe ukafiri? Wanachuoni walipambanua suala hili na wakasema ambaye atapinga ngazi ya kwanza – ambayo ni ya elimu – na akasema kuwa Allaah hayajui mambo isipokuwa baada ya kutokea kwake kwa njia ya kwamba pale yanapotokea ndio huyajua, mtu huyu anakufuru. Kwa sababu amepinga elimu ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Lakini hata hivyo wanasema kuwa wale wenye kupinga elimu wametokomea. Hivi ndivyo alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika “al-Waasitwiyyah”[1]. Mu´tazilah waliobaki wanathibitisha elimu ya Allaah (´Azza wa Jall) ya milele. Lakini hata hivyo wanapinga Qadar. Hivyo wao ni wapotevu. Hawafikii kiwango cha ukafiri. Kwa sababu watu hawa wanathibitisha elimu ya Allaah (´Azza wa Jall) na kuandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa. Wanachopinga ni utashi na matakwa. Bi maana wamethibitisha elimu na uandishi na wakachupa mipaka katika matendo ya waja na wakasema kuwa yanatokea pasi na utashi na matakwa ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Haya bado mpaka sasa yapo na yanaendelea kwa Mu´tazilah na yale mapote mengine yaliyochukua madhehebu yao.

Huu ni ufupisho juu ya suala hili likubwa. Lakini inatosheleza kwa muislamu kuijua misingi hii na kusimama kwayo na wala asivuke mipaka katika kutafiti masuala ya Qadhwaa´ na Qadar. Asijifungulie kwenye nafsi yake mlango wa kuchukulia wepesi. Kwa kuwa hatofikia natija yoyote. Kwa kuwa Qadhwaa´ na Qadar ni siri ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa waja Wake. Huwezi kufikia natija yoyote kwa kuchukulia wepesi. Ni juu yako kutembea pamoja na dalili za Qur-aan na Sunnah na uthibitishe Qadhwaa´ na Qadar na utambue dalili zake na hukumu ya mwenye kuyapinga.

[1] Tazama “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”, uk. 164 kwa sharh ya mwandishi (Hafidhwahu Allaah)