67. Radd juu ya utata wa kumi: Banuu Israa´iyl na Maswahabah hawakukufuru

Washirikina wana shubuha nyingine ambayo wanajaribu kuijadili kwa kisa hiki. Wanasema: “Kwa hakika Banuu Israaiyl hawakukufuru kwa hilo na hali hadhalika wale waliosema “Tufanyie Dhaat Anwaatw”, hawakukufuru”. Tunawajibu kwa kusema: “Banuu Israaiyl hawakufanya hilo, na hali kadhalika waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakufanya hilo. Na wala hakuna tofauti ya kwamba Banuu lau wangelifanya hilo wangelikufuru na wala hakuna tofauti ya kwamba wale aliowakataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lau wasingelimtii na wakachukua Dhaat Anwaatw baada ya makatazo, wangelikufuru. Na hili ndilo linalotakikana.

MAELEZO

Miongoni mwa dalili za kwamba ambaye anafanya moja katika vitenguzi vya Uislamu anakufuru hata kama anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, anaswali, anafunga na matendo mengine ni yale Allaah aliyosimulia kuhusu Banuu Israa´iyl pindi walipomuomba Allaah awafanyie mungu kama mungu wa washirikina na kisa cha wale walimuomba Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awafanyie Dhaat Anwatw na kwamba Mitume wakarimu waliwakemea hayo na wakayazingatia kuwa ni shirki inayomtoa mtu katika Uislamu endapo wangeliyafanya pamoja na kuwa wanawaamini Mitume hao wakarimu na walipigana Jihaad bega kwa bega pamoja nao. Halafu Shaykh akataja kipingamizi cha dalili hizi. Nacho ni kwamba Banuu Israa´iyl waliomuomba Muusa awafanyie mungu hawawakufuru. Vivyo hivyo wale waliomuomba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awafanyie Dhaat Anwaatw hawakukufuru. Amejibu vipingamizi hivi ya kwamba makundi yote mawili hayakutekeleza waliyoyasema. Wangeliyafanya wangekufuru. Lakini pindi walipowazindua juu ya hayo na wakawabainishia kuwa ni kufuru wakajiepusha na wakakomeka. Kinacholengwa katika visa vyote viwili ni kwamba yule mwenye kufanya shirki anakufuru hata kama anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, anawaamini Mitume na anafanya matendo mema.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 104
  • Imechapishwa: 14/02/2017