Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Akamfanya yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume wa mwisho hali ya kuwa ni mwenye kutoa bishara njema na mwenye kuonya, na mlinganiaji kwa Allaah kwa idhini Yake na talaa lenye kuangaza. Akamteremshia Kitabu Chake cha hekima. Kwacho akaifafanua dini Yake ilionyooka na kwacho akaongoa katika njia ilionyooka.

MAELEZO

Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni nwenye kutoa bishara njema kwa wema na kuwaonya waovu. Alikuwa ni mwenye kulingania kwa Allaah kwa yale Aliyomuwekea katika Shari´ah, dini na kuabudiwa Kwake Yeye pekee. Alikuwa ni taa lenye kuwaangazia watu ambapo Allaah anamtoa yule amtakaye kutoka gizani na kumwingiza ndani ya nuru. Taa hili linawaangazia viumbe kwa nuru ya imani, uongofu na Wahy.

Allaah amemteremshia Qur-aan. Qur-aan ambayo ndio Kitabu kitukufu zaidi na chenye kuvidhibiti Vitabu vyengine vyote. Hakuna batili inayokiingilia kwa mbele na kwa nyuma, ni uteremsho kutoka kwa Yule ambaye ni Mwingi wa hekima, anayestahiki kuhimidiwa kwa kila kitu. Qur-aan ndio itakayoendelea kubaki mpaka pale itaponyanyuliwa katika zama za mwisho. Allaah ameifafanua dini Yake kupitia Kitabu cha hekima. Qur-aan ndio ambayo imeifafanua dini. Amesema (Ta´ala):

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ

“Tumekuteremshia Kitabu hali ya kuwa ni chenye kubainisha kila kitu na ni mwongozo na rehema na bishara kwa waislamu.”[1]

Kitabu ni chenye kubainisha kila kitu ambacho kinahitajiwa na watu mpaka kisimame Qiyaamah. Hakuna tukio linalotokea isipokuwa ndani ya Qur-aan kumebainshwa hukumu yake kwa yule ambaye anayo elimu na uoni wa mbali. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

“Wala hawakujii kwa mfano wowote isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri nzuri kabisa.”[2]

Isitoshe Sunnah ni yenye kuibainisha na kuifasiri Qur-aan. Amesema (Ta´ala):

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yale yaliyoteremshwa kwao.”[3]

[1] 16:89

[2] 25:33

[3] 16:44

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 52
  • Imechapishwa: 10/08/2021