67. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) “Hawakumkadiria Allaah inavyostahiki kukadiriwa!”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

”Hawakumkadiria Allaah inavyostahiki kukadiriwa! Ardhi yote itawekwa mkononi Mwake siku ya Qiyaamah na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume.” (az-Zumar 39:67)

2- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna mwanachuoni mmoja wa kiyahudi alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamwambia: “Ee Muhammad! Sisi tunakuta kuwa Allaah ataziweka mbingu saba juu ya kidole, ardhi saba juu ya kidole, miti juu ya kidole, maji na vumbi juu ya kidole na viumbe vyengine vilivyobaki juu ya kidole. Halafu atasema: “Mimi ndiye Mfalme.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka magego yake yakaonekana kwa kusadikisha maneno ya mwanachuoni huyu. Kisha akasoma:

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

”Hawakumkadiria Allaah inavyostahiki kukadiriwa! Ardhi yote itawekwa mkononi Mwake siku ya Qiyaamah na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume.”aa

3- Katika upokezi mwingine wa Muslim imekuja:

“… milima na miti juu ya kidole. Kisha atavitikisa na atasema: “Mimi ndiye Mfalme, Mimi ndiye Allaah.”

Katika upokezi mwingine wa al-Bukhaariy imekuja:

“Allaah ataziweka mbingu juu ya kidole, maji na mchanga juu ya kidole na viumbe vyengine vilivyobaki juu ya Kidole.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim[1].

Muslim amepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah atazikunja mbingu siku ya Qiyaamah, kisha atazishika kwa mkono Wake wa kulia. Halafu atasema: “Mimi ndiye Mfalme! Wako wapi wenye jeuri? Wako wapi wenye kiburi?” Kisha atazikunja ardhi saba, kisha atazishika kwa mkono Wake wa kushoto kisha atasema: “Mimi ndiye Mfalme! Wako wapi wenye jeuri? Wako wapi wenye kiburi?”[2]

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba amesema:

“Hazikuwa mbingu saba wala ardhi saba katika kiganja cha Mwingi wa rehema isipokuwa ni kama chembe ya hardali katika kiganja cha mmoja wenu.”

Ibn Jariyr kasema: “Yuunus amenihadithia: Ibn Wahb ametukhabarisha: Ibn Zayd amesema: Baba yangu amenihadithia: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mbingu sana ukizilinganisha na Kursiy ni kama mfano wa vipande saba vya fedha vilivyotupwa katika ngao.”

Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kursiy ukiilinganisha na ´Arshi si kitu isipokuwa ni kama mfano wa kijipete cha chuma kilichotupwa katika uwanja mkubwa.”[3]

4- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Masafa ya baina ya mbingu ya dunia na inayofuatia ni miaka 500. Baina ya kila mbingu mpaka nyingine ni miaka 500. Baina ya mbingu ya saba na Kursiy ni miaka 500. Baina ya Kursiy na maji ni miaka 500. ´Arshi iko juu ya maji na Allaah Yuko juu ya ´Arshi na hakuna kinachofichikana Kwake katika matendo yenu.

Ameipokea Ibn Mahdiy kutoka kwa Hammaad bin Salamah, kutoka kwa ´Aaswim, kutoka kwa Zirr, kutoka kwa ´Abdullaah. al-Mas´uudiy amepokea mfano wahiyo, kutoka kwa ´Aaswim, kutoka kwa Abu Waa-iyl, kutoka kwa ´Abdullaah. Haafidhw adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Imepokelewa kwa njia nyingi.”

5- al-´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hivi mnajua ni masafa ngapi baina ya mbingu na ardhi?” Tukajibu: “Allaah na Mtume Wake ndio wajuzi zaidi.” Akasema: “Baina yake kuna masafa ya miaka 500. Kutoka katika mbingu moja hadi nyingine ni mwendo wa miaka 500. Unene wa kila mbingu ni mwendo wa miaka 500. Baina ya mbingu ya saba na ´Arshi kuna bahari. Kutoka chini yake mpaka juu yake ni kama umbali wa baina mbingu na ardhi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Yuko juu ya hivyo na hakuna kinachojificha katika matendo ya wanaadamu.”[4]

Ameipokea Abu Daawuud na wengineo.

MAELEZO

Mlango huu wa mwisho umekusanya sampuli zote tatu za Tawhiyd:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

”Hawakumkadiria Allaah inavyostahiki kukadiriwa! Ardhi yote itawekwa mkononi Mwake siku ya Qiyaamah na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume.”

Aayah hii inathibitisha ukubwa wa utukufu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba atazikunja mbingu na ardhi. Aliye na sifa kama hii ana kila haki ya kuabudiwa na kutiiwa. Yeye ndiye Mwenye ukamilifu katika majina, sifa na matendo Yake. Yeye hana anayefanana Naye, hana mshirika na wala halinganishwi na viumbe Wake. Yeye ni muweza wa kila jambo.

2- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna mwanachuoni mmoja wa kiyahudi alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamwambia: “Ee Muhammad! Sisi tunakuta kuwa Allaah ataziweka mbingu saba juu ya kidole, ardhi saba juu ya kidole, miti juu ya kidole, maji na vumbi juu ya kidole na viumbe vyengine vilivyobaki juu ya kidole. Halafu atasema: “Mimi ndiye Mfalme.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka magego yake yakaonekana kwa kusadikisha maneno ya mwanachuoni huyu. Kisha akasoma:

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

”Hawakumkadiria Allaah inavyostahiki kukadiriwa! Ardhi yote itakamatwa mkononi Mwake wa kuume siku ya Qiyaamah.”

Hadiyth inathibitisha kwamba Allaah ana sifa na kwamba Yeye (Subhaanah) ana mkono wa kuume na wa kushoto na kwamba yote miwili ni ya kuume, kama ilivyokuja katika Hadiyth nyingine. Mmoja unaitwa mkono wa kuume na mwingine unaitwa mkono wa kushoto, lakini inapokuja kimaana na utukufu mikono yake yote miwili ni ya kuume na haina aina yoyote ile ya mapungufu. Vivyo hivyo Hadiyth hii inathibitisha kiganja cha Allaah:

“Hazikuwa mbingu saba wala ardhi saba katika kiganja cha Mwingi wa rehema isipokuwa ni kama chembe ya hardali katika kiganja cha mmoja wenu.”

5- al-´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hivi mnajua ni masafa ngapi baina ya mbingu na ardhi?” Tukajibu: “Allaah na Mtume Wake ndio wajuzi zaidi.” Akasema: “Baina yake kuna masafa ya miaka 500. Kutoka katika mbingu moja hadi nyingine ni mwendo wa miaka 500. Unene wa kila mbingu ni mwendo wa miaka 500. Baina ya mbingu ya saba na ´Arshi kuna bahari. Kutoka chini yake mpaka juu yake ni kama umbali wa baina mbingu na ardhi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Yuko juu ya hivyo na hakuna kinachojificha katika matendo ya wanaadamu.”

Hadiyth hizi zinathibitisha sifa za Allaah na Allaah kuwa juu. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameafikiana juu ya kwamba Allaah yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe Wote na kwamba ujuzi Wake umeenea kila mahali. Dalili juu ya hili hazidhibitiwi.

Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ni Swahiyh na nzuri. Vivyo hivyo Hadiyth ya al-´Abbaas, hata kama cheni ya wapokezi imekatika, inatiwa nguvu na zengine. Kuna mapokezi mengine yanayosema kwamba masafa ni 71, 72 na 73. Wanachuoni wameyaoanisha baina yake kwamba tofauti hizo zinatokamana na kasi ya ule mwendo. Kwa njia hiyo mwendo wa miaka 500 ni ngamia aliyebeba mizigo, mtu anayetembea kwa miguu na mwendo wa kawaida ilihali miaka 73 ni mwendo khafifu na wenye nguvu kiasi ambao kasi yake ni mara sita ukilinganisha na ule mwendo mzito. Kwa hali yoyote ile zinafahamisha juu ya utukufu na ujuu wa Allaah na kwamba hakuna matendo ya wanaadamu wowote yanayofichikana Kwake.

Hadiyth zinafahamisha vilevile ujuu wa viumbe vilivyotajwa na namna masafa marefu yaliyo baina yake. Hata hivyo Mola wako na Muumbaji Wako (Jalla wa ´Alaa) ambaye kaviumba ni mtukufu na mkubwa zaidi.

Himdi zote zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] al-Bukhaariy (4811) na Muslim (2786).

[2] Muslim (2788).

[3] Jaami´-ul-Bayaan (5/399) na Abuush-Shaykh katika ”al-´Adhwamah” (2/587).

[4] Ahmad (1770), Abu Daawuud (4723), at-Tirmidhiy (3320), Ibn Maajah (193) na al-Haakim (3137). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaami´” (6093).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 183-186
  • Imechapishwa: 15/11/2018