1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye anamwamini Allaah na siku ya Mwisho basi amkirimu mgeni wake. Yule anamwamini Allaah na siku ya Mwisho basi asimuudhi jirani yake.”

2 – Napendekeza kwa mwenye busara kuwa na mazowea ya kuwalisha watu chakula na kudhibiti jambo la kumkirimu mgeni. Kulisha chakula ni moja katika sifa tukufu, kubwa na nzuri zaidi. Anayetambulika kwa kuwalisha watu chakula huzingatiwa ni mtukufu mbele ya kila mtu. Kumkirimu mgeni kunamnyanyua mtu katika ngazi za juu hata akiwa anatokana na ukoo wa chini.

3 – Sa´iyd bin al-Musayyab amesema:

“Ibraahiym (´alayhis-Salaam) ndiye alikuwa wa kwanza kumkirimu mgeni.”

4 – Kila ambaye alikuwa bwana katika kipindi cha kikafiri na katika Uislamu alikuwa hivo kwa kuwalisha watu chakula na kuwakirimu wageni.

5 – Waarabu walikuwa hawaoni ukarimu kuwa chochote isipokuwa kwa kuwakirimu wageni na kulisha chakula. Walikuwa hawaonelei mtu kwamba ni mkarimu isipokuwa kwa kuwa na sifa hizo. Baadhi walikuwa wanaweza kutembea kilomita nyingi ili tu waweze kumpata mgeni.

6 – al-Hasan bin ´Iysaa bin Maasarjas amesema:

“Nilisafiri na Ibn-ul-Mubaarak kutoka Khuraasaan mpaka Baghdaad na sikuwahi kumuona siku hata moja akila peke yake.”

7 – Kitu kinachozingatiwa katika kumkirimu mgeni ni kutokidharau kile kidogo. Mtu amwalike mgeni kwa kile alichomwandalia. Yule anayedharau kitu basi hakitoi.

8 – ´Uqbah bin ´Alqamah na Mubashshir bin Ismaa´iyl walimuuliza al-Awzaa´iy nini maana ya kumkirimu mgeni. Akasema:

“Uso wenye bashasha na maneno mazuri.”

9 – Mtu bakhili kabisa ni yule mwenye kufanya ubakhili katika kulisha chakula na mtu mkarimu zaidi ni yule mwenye kufanya ukarimu katika kulisha chakula.

10 – Miongoni mwa kumkirimu mgeni ni maneno mazuri, uso wenye bashasha na mwenyeji binafsi amuhudumie mgeni. Yule anayewahudumia wageni wake hawi mdhalilifu na yule anayewatumikisha au akawaomba malipo hatukuki.

11 – Sa´iyd bin al-Musayyab amesema:

“Napendezwa zaidi kulisha tumbo kuliko kufanya hajj  baada ya hajj.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 258-263
  • Imechapishwa: 06/09/2021