Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Kisha akaumalizia ujumbe Wake na unabii kwa Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Mtume wa kwanza ni Nuuh (´alayhis-Salaam). Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama tulivyomfunulia Wahy Nuuh na Manabii baada yake.”[1]

Hata hivyo walikuweko Manabii Aadam na Idriys walioishi kabla ya Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Mtume wa kwanza anayetambulika ni Nuuh na wa mwisho wao ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Allaah daima ni mjuzi wa kila jambo.”[2]

Hakuna Nabii mwingine atakayejitokeza baada yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watajitokeza katika Ummah wangu waongo thelathini na kila mmoja atadai kuwa yeye ni Nabii. Hata hivyo mimi ndiye Nabii wa mwisho. Hakuna Nabii mwingine baada yangu.”[3]

Nabii atabaki ni yeye mpaka pale kitaposimama Qiyaamah. Baada ya kutumilizwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna haja ya kutumiliza Mitume wengine, kwa sababu ujumbe wake ni wenye kutosheleza mpaka pale kitaposimama Qiyaamah. Qur-aan ni yenye kusilihi katika kila zama na pahali. Vivyo hivyo Shari´ah ya Kiislamu. Yule mwenye kumwamini Mtume mwingine baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kafiri na yule mwenye kuwasadikisha Mitume waongo ni kafiri pia. Kwa ajili hiyo wakati Ahmad al-Qaadiyaaniy alipojidai utume waislamu kwa kukubaliana wote walimuhukumu kwamba ni kafiri yeye na wafuasi wake, kwa sababu Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Allaah daima ni mjuzi wa kila jambo.”

Vilevile maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watajitokeza katika Ummah wangu waongo thelathini na kila mmoja atadai kuwa yeye ni Nabii. Hata hivyo mimi ndiye Nabii wa mwisho. Hakuna Nabii mwingine baada yangu.”

Viumbe hawahitajii Mtume mwingine baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wala hakuna Kitabu kingine baada ya Qur-aan. Ni katika misingi ya ´Aqiydah kuamini kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Nabii wa mwisho na kwamba yule ambaye atajidai kuwa ni Nabii baada yake ni kafiri mwongo.

[1] 4:163

[2] 33:40

[3] Ahmad (22395), Abu Daawuud (4252), at-Tirmidhiy (2219), Ibn Hibbaan (7238) na Abu Nu´aym (2/289). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaat” (5406).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 10/08/2021