66. Mtume (صلى الله عليه وسلم) kuihami Tawhiyd na kuziba njia zote za shirki


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- ´Abdullaah bin ash-Shukhayr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilifuatana na mjumbe wa Banuu ´Aamir kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tukasema: “Wewe ndiye bwana wetu.” Akasema: “Bwana ni Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).” Tukasema: “Wewe ni mbora wetu kwa ubora na ni mkubwa wetu kwa ukarimu.” Akasema: “Semeni msemayo, au baadhi yake tu, na wala asikupotezeni shaytwaan.”[1]

Ameipokea Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi nzuri.

2- Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba kuna watu walisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Ee mbora wetu na mtoto wa mbora wetu! Bwana wetu na mtoto wa bwana wetu.” Ndipo akasema: “Enyi watu! Semeni msemayo, au baadhi yake tu, na wala asikupotezeni shaytwaan. Mimi ni Muhammad, ni mja wa Allaah na Mtume Wake. Sipendi mnipandishe zaidi ya cheo changu alichonipa Allaah (´Azza wa Jalla).”[2]

Ameipokea an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi nzuri.

MAELEZO

Hapa mwandishi anazungumzia kuihami Tawhiyd kwa njia ya maneno. Tayari kuihami Tawhiyd kwa njia ya matendo kumeshatangulia. Mlango huu unazungumzia kuihami mipaka ya Tawhiyd. Mipaka sio dhati yenyewe ya kitu. Kwa hiyo kichwa cha khabari ni chenye nguvu zaidi juu ya yale yaliyofungamana na Tawhiyd na maneno.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameihami Tawhiyd na akaihami mipaka ya Tawhiyd dhidi ya maneno na vitendo ili watu wasije kuisogelea Tawhiyd na kutumbukia ndani yake. Alitahadharisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile juu ya njia zote zinazopelekea katika shirki, jambo ambalo ni miongoni mwa ukamilifu wa ujumbe.

1- ´Abdullaah bin ash-Shukhayr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilifuatana na mjumbe wa Banuu ´Aamir kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tukasema: “Wewe ndiye bwana wetu.” Akasema: “Bwana ni Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).” Tukasema: “Wewe ni mbora wetu kwa ubora na ni mkubwa wetu kwa ukarimu.” Akasema: “Semeni msemayo, au baadhi yake tu, na wala asikupotezeni shaytwaan.”

Ameipokea Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi nzuri.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Bwana ni Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hivo kwa sababu ya unyenyekevu na kuchelea wasije kutumbukia katika upetukaji. Vinginevyo yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye bwana wa wanaadamu. Lakini alisema hivo kwa sababu ya unyenyekevu na kwa kukhofia wasije kutumbukia katika kuchupa mipaka. Ni dalili inayoonyesha kuwa mtu akiambiwa na mwengine kwamba yeye ni bwana wao basi anatakiwa kusema:

“Bwana ni Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

Anasema hivi ili asije kuingiwa na majivuno.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… na wala asikupotezeni shaytwaan.”

Bi maana shaytwaan asije kuwavuta katika mambo yasiyotakikana. Msimwache akakuingizeni katika shirki na kuvuka mipaka. Tumieni maneno yaliyozoeleka kama vile Abul-Qaasim, Mtume wa Allaah na Nabii wa Allaah. Msitumie maneno ambayo yanaweza kukuingizeni katika kuchupa mipaka. Allaah (Ta´ala) amesema:

 أَيُّهَا الرَّسُولُ

“Ee Mtume!” (al-Maaidah 05:67)

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ

”Ee Nabii!” (al-Mumtahinah 60:12)

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا م

”Utakasifu ni wa ambaye Alimsafirisha usiku mja Wake… ” (al-Israa´ 17:01)

حَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَنزَلَ عَلَىٰ عَبْدِهِ الْكِتَابَ وَلَمْ يَجْعَل لَّهُ عِوَجًا

“Himdi zote anastahiki Allaah ambaye amemteremshia mja Wake Kitabu na wala hakukifanya kikawa na ukombo.” (al-Kahf 18:01)

Makusudio ya haya yote ni kufunga njia zote ziwezazo kuwapelekea watu kuchukulia wepesi shirki. Wakitumia maneno kama “bwana” na mfano wake katika upetukaji ambayo yanatumiwa na watu hii leo matokeo yake yanaweza kuwafanya wakaanza kumwabudu badala ya Allaah, wakamuomba, wakamtaka msaada, kudai kwamba anajua mambo yaliyofichikana na mfano wake. Kama alivosema mwandishi wa “al-Burdah” wakati aliposema:

Ee kiumbe mbora! Sina mwengine zaidi yako wa kumkimbilia wakati wa majanga

Usiponitukuza siku ya Qiyaamah na ukanishika mkono, nimeangamia.

Katika ukarimu wako ni pamoja na dunia hii na mali zake

na miongoni mwa elimu zako ni pamoja na elimu ya Ubao na Kalamu.

Kuvuka mipaka kulimpelekea akasema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye ambaye atamwokoa siku ya Qiyaamah na kwamba yule ambaye hatookolewa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ameangamia. Huu ni upetukaji mkubwa. Amesema vilevile kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anayajua yaliyomo katika Ubao na katika Kalamu na kwamba yeye anakijua kila kitu.

Ni wajibu kwa muislamu kuuchunga ulimi wake na awe mkati na kati anapoongea sawa akiwa anamzungumzia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au mwengine. Ni lazima kwake kujipamba na adabu za Kishari´ah inapokuja kwa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam), waja wema na wanachuoni ili asije kutumbukia katika upetukaji waliyotumbukia ndani yake mayahudi na manaswara. Hatimaye wakaanza kuwaabudu Mitume wao, waja wao wema na wanachuoni na wakawaomba msaada. Wakatumbukia katika shirki kubwa ambayo ndio dhambi isiyosamehewa.

[1] Abu Daawuud (4806) na al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad” (211). Cheni ya wapoezi wake ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (4900).

[2] Ahmad (13553) na an-Nasaa’iy (10078). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Iswlaah-ul-Masaajid” (1/126).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 181-182
  • Imechapishwa: 15/11/2018