Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Daraja ya tatu ni Ihsaan. Ina nguzo moja, nayo ni “kumwabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona”. Dalili ya ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ

“Hakika Allaah yu pamoja na wenye kumcha na wale watendao wema.” (an-Nahl 16 : 128)

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

“Tegemea kwa Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mwenye kurehemu. Aambaye anakuona wakati unaposimama na mageuko yako katika wenye kusujudu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.” (ash-Shu´araa´ 26 : 217-220)

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ

“Hushughuliki jambo lolote na wala husomi humo katika Qur-aan na wala hamtendi matendo yoyote isipokuwa Tunakuwa mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo.” (Yuunus 10 : 61)

MAELEZO

Ihsaan ni kinyume cha kufanya kitu kiovu na maana yake ni kule kujitahidi kufanya mema na kujizuia na maovu. Kwa njia hiyo ina maana ya kujitahidi kuwafanyia wema waja wa Allaah kwa mali yake, nafasi yake, elimu yake na mwili wake.

Ama mali, inahusiana na kujitolea, kutoa swadaqah na kutoa zakaah. Zakaah ndio aina bora ya Ihsaan kwa sababu ni moja katika nguzo za Uislamu na misingi yake mikubwa. Uislamu wa mtu haukamiliki isipokuwa kwayo. Ni bora ya vinavyotolewa vinavyopendwa zaidi na Allaah (´Azza wa Jall). Inafuatiwa na yale yanayomuwajibikia mume kumhudumia mke wake, wazazi wake, watoto wake, ndugu zake, watoto wa nduguye, dada zke, ami zake, wajomba zake, shangazi zake na wengineo. Halafu inafuatiwa na swadaqah kuwapa masikini na wengineo wenye kustahiki kupewa swadaqah kama kwa mfano wanafunzi.

Ama nafasi, pengine mtu akawa na nafasi fulani kwa mtu ambaye yuko na utawala. Katika hali hii mtu anatakiwa kutumia nafasi yake. Kwa mfano akaja mtu kwake na kumuomba amuombee kwa mtawala. Inaweza kuhusiana na kumkinga na madhara au kumletea kheri.

Ama elimu, anatumia elimu yake kwa kuwafundisha waja wa Allaah katika vikao vya watu wote na watu binafsi na katika duara za kielimu. Hili linahusu hata kama mtu atakuwa katika kikao cha kahawa. Ni katika kheri na wema kuwafundisha watu. Hata hivyo unatakiwa kutumia hekima katika mlango huu. Usiwatie uzito watu kwa njia ya kwamba kila unapokaa nao, basi unawawaidhi na kuzungumza nao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa watu mawaidha pasi na kukithirisha hilo. Kwa sababu watu huchoka. Pindi wanapochoshwa, huchoka na kudhoofika. Inaweza kufikia kiasi cha kwamba wakaanza kuchukia kheri kwa kukithiri kwa maneno marefu na ya watu wengi.

Ama mwili, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni katika swadaqah kumsaidia mtu na kipando cake kwa kumbeba juu yake au kumpandishia mzigo wake.”[1]

Hapa kuna mtu ambaye unamsaidia kumbebea mzigo wake, kumwelekeza njia au mfano wa hayo. Yote haya ni katika Ihsaan. Haya yanahusiana na kuwafanyia Ihsaan waja wa Allaah.

Kuhusinaa na Ihsaan katika ´ibaada ya Allaah, ni kule kumwabudu Allaah kama vile unamuona. Hili limesemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Ibaadah ya kumwabudu Allaah kama vile unamuona, ni ´ibaadah iliombatana na bidii na shauku. Wakati ´ibaadah inapokuwa na bidii na shauku, basi mtu anakuwa na moyo kwayo, kwa sababu anajitahidi kwa kitu ambacho anakipenda. Hivyo anamwabudu Allaah kama vile anamuona. Anamkusudia Yeye, anarejea Kwake na kujikurubisha Kwake (Subhanaahu wa Ta´ala).

Sentesi “ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona” ndani yake mna ´ibaadah ya kukimbia na kukhofu. Kwa ajili hii ndio maana ikawa daraja ya pili ya Ihsaan. Ikiwa humwabudu Allaah (´Azza wa Jall) kama vile unamuona, kumtafuta na kuihimiza nafsi yako kumfikia, basi mwabudu Allaah kama vile Yeye ndiye anakuona. Katika hali hii unamwabudu kwa ´ibaadah ya khofu kama vile kukimbia adhabu Yake. Ngazi hii kwa waja wema wenye kuabudu iko chini kuliko ile ngazi ya kwanza.

´Ibaadah anayofanyiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni kama alivyosema Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah):

´Ibaadah anayofanyiwa Mwingi wa rehema ni kwamba

Mja wake ana mapenzi na kujidhalilisha Kwake kwa hali ya juu

Hizi ndio nguzo mbili

´Ibaadah imejengeka juu ya mambo haya mawili; mapenzi ya hali ya juu na kujidhalilisha kwa hali ya juu. Katika mapenzi kuna kufanya jitihada na katika kujidhalilisha kuna kufanya khofu na kukimbia. Hii ndio Ihsaan katika ´ibaadah anayofanyiwa Allaah (´Azza wa Jall). Ikiwa mtu anamwabudu Allaah kwa njia hii, atamwabudu (´Azza wa Jall) kwa Ikhlaasw.  Kwa ´ibaadah yake kama hii hakusudii kujionyesha, kutaka kusikika wala sifa kutoka kwa watu. Hajali sawa ikiwa watu watamuona au hawamuoni. Haoni tofauti yoyote katika hali zote hizo mbili. Kwa hali yoyote ile, yeye anaifanya ´ibaadah yake kwa hali nzuri. Bali ni katika Ikhlaasw iliotimia mtu akafanya kila aliwezalo watu wasimuone na akamwabudu Mola Wake kwa siri. Isipokuwa tu ikiwa katika kufanya hilo hadharani kuna manufaa kwa waislamu au juu ya Uislamu. Mfano wa hilo ni mtu akawa mwenye kufuatwa ambaye anachukuliwa kama kiigizo na akataka kuwabainishia watu ni vipi anavofanya ´ibaadah ili waweze kumuigiliza katika kitendo hicho. Mfano mwingine ni yeye kufanya ´ibaadah hadharani ili marafiki na wenzake waweze kumuigiliza. Ni kitendo cha kheri. Manufaa ya kufanya kitendo hichi hadharani yanaweza kuwa ni bora kuliko manufaa ya kuficha. Kwa ajili hii Allaah (´Azza wa Jall) anawasifu wale wenye kuzitoa mali zao kwa siri na kwa dhahiri. Endapo ni vyema, manufaa, uchaji Allaah na kurejea kwa mioyo zaidi kufanya hilo kwa siri, basi mtu afanye hilo kwa siri. Na endapo kuna manufaa zaidi juu ya Uislamu, kudhihirika nembo zake, na ikawa waislamu wataigiliza jambo hili, basi itafanywa hadharani.

Muumini siku zote huangalia lile lililo na manufaa zaidi. Kila ambavo ´ibaadah itakuwa na manufaa zaidi, ndivyo jinsi itavyokuwa kamilifu na bora zaidi.

[1] al-Bukhaariy (2891) na Muslim (1009).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 118-120
  • Imechapishwa: 03/06/2020