1 – Hana eda yule mwenye kuachwa kabla ya kuingiliwa. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا

“Enyi walioamini! Mnapofunga ndoa na waumini wa kike kisha mkawataliki kabla ya kuwajamii, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu.”[1]

Ibn Kathiyr amesema katika “Tafsiyr” yake:

“Hili ni jambo ambalo wanachuoni wameafikiana kwalo kwamba mwanamke akitalikiwa kabla ya kuingiliwa basi hana eda. Papo hapo anaweza kwenda zake na kuolewa na anayemtaka.”[2]

2 – Mwenye kuachwa kabla ya kuingiliwa na ameshatajiwa mahari basi anapata nusu yake. Na yule ambaye hajatajiwa mahari basi apewa Mut´ah kwa kile kitachowepesika katika mavazi na mfano wake. Na yule mwenye kuachwa baada ya kuingiliwa atapata mahari. Amesema (Ta´ala):

لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً ۚ وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ

“Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa [kuwajamii] au kuwabainishia kwao mahari; wapeni kiliwazo kwa mwenye wasaa kiasi cha uwezo wake na mwenye dhiki kiasi cha uwezo wake.”

Mpaka aliposema:

وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ

“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa [kuwajamii] na mkawa mmeshawabainishia kwao mahari, basi [wapeni] nusu ya hayo mliyobainisha.”[3]

Maana yake ni kwamba, enyi waume, hakuna ubaya juu yenu kuwataliki wanawake kabla ya kuwajamii na kuwapa mahari yao. Ingawa katika hilo kuna kumvunja moyo mwanamke huyo lakini hata hivyo kunaungwa na hiyo Mut´ah. Mut´ah inategemea kila mume na hali yake, nzito na ngumu, kwa mujibu wa ilivyo desturi za watu. Kisha (Subhaanah) akamtaja yule ambaye tayari ameshakadiriwa mahari na akaamrisha apewe nusu yake. Ibn Kathiyr amesema katika “Tafsiyr” yake:

“Ile kumgawanyia mahari nusu katika hali hii ni jambo ambalo wanachuoni wameafikiana na hakuna tofauti kati yao.”[4]

[1] 33:49

[2] (05/479).

[3] 02:236-237

[4] (01/512).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 113-114
  • Imechapishwa: 27/11/2019