66. Baadhi ya mambo yanayofaa kati ya waislamu na makafiri

Kilichobaki kwetu sisi kujua; ni mambo yepi ambayo inafaa kwetu kutaamiliana nao. Yako mambo ambayo inafaa kutangamana pamoja na makafiri. Kwa sababu hayaingii katika kuwafanya marafiki wala katika kuwapenda. Isipokuwa ni katika mambo yaliyoruhusiwa na ni katika manufaa ya kushirikiana. Inafaa kwetu:

La kwanza: Kutangamana na makafiri kwa kufanya biashara kwa njia ya kwamba sisi tukawauzia na tukanunua kutoka kwao.

La pili: Tukafaidika kutoka katika mambo ya uzoefu wao na kuwaajiri ili wafanye kazi ambazo haziwezi kufanywa na waislamu. Haifai kuwaajiri na kuwafichulia mambo yetu maalum kama kwa mfano kuwafanya wakawa mawaziri au washauri. Isipokuwa tunawaajiri kufanya kazi ambazo wanaweza kuzifanya na wakati huohuo wakawa mbali na siri za waislamu. Mfano wa kazi hizo ni za ujenzi na za mashirika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuajiri na kumpa kazi kafiri ili amuelekeze njia katika safari ya kuhajiri. Alimpa kazi ´Abdullaah bin Urayqitw ili amuelekeze njia kwa sababu alikuwa ni na ujuzi wa kuelekeza njia[1]. Hivyo akafaidika na uzoefu wake. Hili kwa sharti tusiwafichulie siri zetu na wandani wa mambo yetu.

La tatu: Inajuzu kuandikiana mikataba na makafiri ikiwa katika kufanya hivyo kuna manufaa kwa waislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia mikataba ya amani na mayahudi wa al-Madiynah washirikina huko Hudaybiyah[2]. Ikiwa kuna manufaa kwa waislamu au waislamu hawawezi kupigana na makafiri, basi itafaa kuandikiana mikataba na kupatana nao kutomana na yale manufaa yanayopatikana kwa kufanya hivo kwa waislamu.

La nne: Inajuzu kuwalipa wema wakapotufanyia wema. Amesema (Ta´ala):

لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

”Allaah hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale wasiokupigeni vita katika dini na wala hawakukutoeni kutoka majumbani mwenu. Hakika Allaah anawapenda wafanyao uadilifu.” (al-Mumtahinah 60:08)

Wakiwafanyia mazuri waislamu, basi waislamu nao watawalipa mazuri na kuwatendea wema. Hawafanyi hivi kwa sababu ya kuwapenda. Bali wanafanya hivi kwa sababu ya kulipiza wema. Ni wajibu kwa mtoto kumtendea wema mzazi wake ambaye ni kafiri pasi na kumpenda. Amesema (Ta´ala):

َوَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ إِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ

”Tumemuusia mwanadamu [kuwafanyia wema] wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake akimzidishia udhaifu juu ya udhaifu na [kumnyonyesha na] kuacha kwake ziwa katika miaka mwili ya kwamba: Unishukuru Mimi na wazazi wako – kwani Kwangu ndio marejeo ya mwisho. Lakini wakikufanyia juhudi kwamba unishirikishe na yale usiyokuwa na elimu nayo, basi usiwatii. Suhubiana nao kwa wema duniani na fuata njia ya anayerudi Kwangu.” (Luqmaan 31:14-15)

Ni wajibu kwa mtoto kumfanyia wema mzazi wake japokuwa ni kafiri. Lakini asiwapende moyoni. Lakini hata hivyo asimpende moyoni mwake:

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَه

”Hutowapata watu wanaomuamini Allaah na siku ya Mwisho kwamba wanawapenda wale wanaopingana na Allaah na Mtume Wake.” (al-Mujaadilah 58:22)

Kuwapenda ni kitu kimoja na kutangamana nao kwa uzuri ni kitu kingine.

Alikuja mama yake na Asmaa´ bint Abi Bakr na alikuwa bado ni mshirikina. Alikuja akimuomba mali kiasi fulani. Asmaa´ akaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumwambia:

“Mama yangu amenijia na anataka mawasiliano. Je, nimuunge?” Akasema: “Ndio, ungana na mama yako.”[3]

[1] Zaad-ul-Ma´aad (03/126).

[2] al-Bukhaariy (2731) na (2732) na Muslim (1785) na (1783).

[3] al-Bukhaariy (5979) na Muslim (1003) kupitia kwa Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhaa).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 92-95