65. Utafiti juu ya Qadhwaa´ na Qadar IV


Tano: Kuhusu mambo yanayopelekea madhehebu ya Jabriyyah na Qadariyyah. Yanapelekea katika mambo ya khatari yafuatayo:

La kwanza: Madhehebu ya Qadariyyah yanapelekea katika kuthibitisha waungu wengi pamoja na Allaah. Hii ni shirki katika uola. Kwa ajili hii ndio maana wameitwa kuwa ni waabudu moto wa Ummah huu.

La pili: Madhehebu ya Jabriyyah yanapelekea kumsifu Allaah kwa dhuluma na kwamba anawaadhibu waja kwa kitu ambacho hawakufanya wao bali kimefanya Allaah. Allaah anawaadhibu kwa kitu ambacho wao hawakufanya. Wao wanaendeshwa tu pasi na khiyari wala kutaka kwao. Huku ni kumsifu Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa dhuluma ya kwamba anawaadhibu waja kwa kitu ambacho hawakufanya wao bali kimefanya Yeye Mwenyewe. Uharibifu wa madhehebu haya batili haufichikani. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Na wala hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.” (36:54)

Amefungamanisha adhabu kwa kufuru, maasi na madhambi kama ambavyo vilevile amefungamanisha utiifu kwa mambo ya utiifu na ya kheri. Allaah hamdhulumu yeyote.

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا

“Hakika Allaah hadhulumu [kiumbe yeyote] uzito wa atomu na ikiwa ni [‘amali] njema huizidisha.” (04:40)

Huu ndio uadilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Miongoni mwa uadilifu Wake ni kuwa hayaongezi madhambi. Analipa kwa mfano wake. Katika fadhila Zake ni kuwa analiongeza jema moja kwa kupenda Kwake Mwenyewe (Subhaanahu wa Ta´ala).

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا

“Hakika Allaah hadhulumu [kiumbe yeyote] uzito wa atomu na ikiwa ni [‘amali] njema huizidisha.”

Huku kuongezewa ni fadhila kutoka kwa Allaah mpaka kufikia kumi mfano wake mpaka kufikia mia saba na zaidi ya hivyo. Kuhusu maovu Allaah analipa mfano wake na hazidishi juu yake. Haya ni kutokana na uadilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini Jabriyyah wanamsifu Allaah kwa dhuluma ya kwamba anawaadhibu waja kwa matendo Aliyofanya Mwenyewe. Wanasema kuwa wao hawakufanya kitu wanapelekwa kama chombo na kama upepo hewani. Haya ni madhehebu batili.

La tatu: Madhehebu yao yanapelekea kuacha kufanya sababu na mtu akasema kuwa midhali Ameshakadiria na kupanga basi mimi nakaa na nilichokadiriwa kitanijia.

La nne: Madhehebu ya Mu´tazilah, kama tulivyotangulia kusema, yanapelekea katika kushirikisha katika uola.

La tano: Madhehebu yao yanapelekea katika madhara makubwa ambayo ni kumfanya Allaah (´Azza wa Jall) kutoweza na kwamba kunapitika katika ufalme Wake kile asichokitaka na kukipenda. Huku ni kumsifu Allaah (´Azza wa Jall) kutokuwa na uwezo. Hii ni khatari kubwa.

Madhehebu yote mawili ni batilifu na yanapelekea katika madhara makubwa. Kuhusu madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah yako kati kwa kati na adilifu katika mambo yote.