Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.”[1]

Katika Aayah hii tukufu kuna ya kwamba kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah ni kufuru. Kufuru hii mara huwa kufuru kubwa inamtoa mtu nje ya Uislamu na mara huwa kufuru ndogo isiyomtoa mtu nje ya Uislamu. Itagemea na hali ya huyo mtawala. Akiamini kuwa kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah sio lazima, kwamba ana khiyari, akaidharau hukumu ya Allaah na akaona kuwa sheria zilizotungwa za wanadamu ndio bora kuliko au zinalingana nayo, haiendani na zama hizi, akahukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah kwa sababu ya kuwaridhisha makafiri na wanafiki, hii ni kufuru kubwa. Akiamini kuwa kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah ni lazima, akaijua hukumu hii katika hali fulani lakini hata hivyo akaiacha na huku akitambua kuwa anastahiki kuadhibiwa, basi ni mtenda dhambi. Anaitwa kafiri mwenye kufuru ndogo. Asipoijua hukumu ya Allaah ndani yake pamoja na kutumia juhudi zake na akajibidisha awezavyo katika kuitambua hukumu lakini licha ya yote hayo akakosea, huyu amekosea. Anapata ujira kwa Ijtihaad yake na kosa lake ni lenye kusamehewa. Hukumu hii inahusiana na qadhiya maalum.

Kuhusu hukumu inayohusiana na qadhiya yenye kuenea inatofautiana. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Hakimu akiwa ni mtu wa dini lakini akahukumu pasi na elimu, anakuwa ni miongoni mwa watu wa Motoni. Akiwa ni msomi lakini hata hivyo akahukumu kinyume na haki anayoijua, anakuwa ni miongoni mwa watu wa Motoni. Akihukumu bila ya uadilifu wala elimu, ana haki zaidi ya kuwa katika watu wa Motoni. Hapa ni pale atapohukumu katika qadhiya ya mtu fulani. Ama akihukumu hukumu yenye kuenea katika dini ya waislamu ambapo akaifanya haki kuwa batili na batili kuwa haki, Sunnah kuwa Bid´ah na Bid´ah kuwa Sunnah, mema yakawa maovu na maovu yakawa mema, akakataza yale aliyoamrisha Allaah na Mtume Wake na akaamrisha yale aliyokataza Allaah na Mtume Wake, hii ina rangi nyingine  ataihukumu Mola wa walimwengu. Ana wajumbe Mfalme wa siku ya malipo. Yeye ndiye anastahiki kuhimidiwa duniani na Aakhirah:

لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

“Hukumu ni Yake pekee na Kwake pekee mtarejeshwa.”[2]

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا

”Yeye ndiye aliyemtuma Mtume Wake kwa mwongozo na dini ya haki ili aishindishe juu ya dini zengine zote. Allaah anatosha kuwa ni shahidi.”[3] [4]

Vilevile amesema:

“Hapana shaka kwamba yule asiyeonelea kuwa ni lazima kwa Mitume Yake kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah ni kafiri. Mwenye kuhalalisha kuhukumu kati ya watu kwa yale anayoona yeye kuwa ndio uadilifu bila kufuata aliyoteremsha Allaah, ni kafiri. Hakuna Ummah wowote isipokuwa unaamrisha kuhukumu kwa uadilifu. Pengine uadilifu katika dini yao ni yale anayoonelea mkuu wao. Bali wengi wanaojinasibisha na Uislamu wanahukumu kwa desturi zao ambazo hazikuteremshwa na Allaah kama desturi kwa watangu wao na wakawa ni viongozi wenye kutiiwa na wakaona kuwa hayo ndio yanayopasa kuhukumiana kwayo pasi na Qur-aan na Sunnah. Hii ndio kufuru. Watu wengi wamesilimu lakini hawahukumu isipokuwa kwa desturi za kisasa zinazoamrishwa na wale wenye kutiiwa. Watu hawa wakitambua kuwa haijuzu kuhukumu isipokuwa tu kwa yale aliyoteremsha Allaah, na wasilazimiane na hilo, bali wakahalalisha kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah, basi ni makafiri.”[5]

Shaykh Muhammad bin Ibrahiym amesema:

“Ama yale yaliyosemwa kwamba ni kufuru ndogo ni pindi mtu atahukumiana kwa asiyekuwa Allaah na wakati huohuo akatambua kuwa ni mtenda dhambi na kwamba hukumu ya Allaah ndio ya haki. Isitoshe jambo hili limemtokea mara moja na mfano wake. Kuhusu ambaye amezifanya kanuni hizo ndio mpangilio na akazinyenyekea, huyo ni kafiri. Haijalishi kitu hata kama watasema kuwa wamekosea na hukumu ya Shari´ah ndio adilifu zaidi, huyu ni kafiri anayetoka nje ya Uislamu.”[6]

Ametofautisha (Rahimahu Allaah) baina ya hukumu ya sehemu ambayo haijirudirudi na baina ya hukumu yenye kuenea ambayo ndio marejeo katika hukumu zengine zote au sehemu yake kubwa. Amekariri kwamba hiyo ni kufuru yenye kumtoa mtu nje ya Uislamu kabisa. Hayo ni kwa sababu yule mwenye kuondosha Shari´ah ya Uislamu na akaziweka kanuni zilizotungwa na wanadamu badala yake ni dalili inayoonyesha kuwa anaona kuwa kanuni hizo ndio bora na zenye kusilihi zaidi kuliko Shari´ah. Hapana shaka kuwa hii ni kufuru kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu na inaivunja Tawhiyd.

[1] 05:44

[2] 28:88

[3] 48:28

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (35/388).

[5] Minhaaj-us-Sunnah an-Nabawiyyah (05/130).

[6] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/280) ya Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aalish-Shaykh.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 123-125
  • Imechapishwa: 26/03/2020