65. Adhkaar kati ya Sujuud mbili


Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema baina ya Sujuud mbili:

1-

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لي وارْحَمْني وَاهدِني وَاجْبرْني وَعَافِنِي وَارْزُقْني

“Ee Allaah! Nisamehe, nihurumie, niongoze, niunge, niafu na uniruzuku.”[1]

Katika matamshi mengine imekuja:

رَبِّ اغْفِرْ لِي وارْحَمْني وَاهدِني وَاجْبرْني وَعَافِنِي وَارْزُقْني

“Ee Mola! Nisamehe, nihurumie, niongoze, niunge, niafu na uniruzuku.”

Mara nyingine akisema:

رَبِّ اغْفِرْ لِي ربِّ اغْفِرْ لي

“Ee Mola! Nisamehe! Ee Mola! Nisamehe!”[2]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akizisoma katika swalah ya usiku[3].

Halafu analeta Takbiyr na anasujudu Sujuud ya pili[4]. Alimwamrisha kufanya hivo yule mtu aliyeswali kimakosa na kumwambia baada ya kumwamrisha kutulia baina ya Sujuud mbili:

“Kisha useme:

الله اكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Kisha sujudu mpaka kila mfupa utulie mahala pake. [Halafu ufanye hivo katika swalah yako yote iliyobaki.]”[5]

Wakati mwingine (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akinyanyua mikono sambamba na Takbiyr hii[6].

Akifanya katika Sujuud hii kama alivyofanya katika ile Sujuud ya kwanza. Halafu akinyanyua kichwa chake na kusema:

الله اكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Alimwamrisha kufanya hivo yule mtu aliyeswali kimakosa[7] na kumwambia:

“Halafu ufanye hivo katika kila Rak´ah na kila Sajdah. Iwapo utafanya hivo, basi swalah yako imetimia, na ukipunguza kitu kwayo, kumepungua kutoka katika swalah yako.”[8]

Wakati mwingine alikuwa anaweza kunyanyua mikono yake[9].

[1] Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[2] Ibn Maajah kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Imaam Ahmad amechagua du´aa hii. Ishaaq bin Raahuuyah amesema:

“Ima aisome mara tatu au asome:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لي وارْحَمْني وَاهدِني وَاجْبرْني وَعَافِنِي وَارْزُقْني

“Ee Allaah! Nisamehe, nihurumie, niongoze, niunge, niafu na uniruzuku.”

Kwa sababu zote mbili zimepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baina ya Sujuud mbili.” (Masaa-il-ul-Imaam Ahmad wa Ishaaq bin Raahuuyah, uk. 19, ya Ishaaq al-Marwaziy)

[3] Haina maana kwamba haikuwekwa katika Shari´ah kusoma hivo katika swalah za faradhi kwa sababu hakuna tofauti kati ya swalah ya faradhi na ya Sunnah, kama alivyosema ash-Shaafi´iy, Ahmad na Ishaaq. Wanaonelea kuwa kitendo hicho kinafaa katika swalah ya faradhi na ya sunnah, kama alivyotaja at-Tirmidhiy. Hata at-Twahaawiy anaonelea kuwa kitendo hicho kimewekwa katika Shari´ah, kama ilivyotajwa katika kitabu “Mushkil-ul-Aathaar”. Kipimo sahihi kinatilia nguvu hili. Kwa sababu hakuna sehemu yoyote katika swalah ambayo haikuwekwa katika Shari´ah kusoma kitu. Kwa hivyo ni lazima hali iwe hivo sehemu hii. Ni jambo liko wazi.

[4] al-Bukhaariy na Muslim.

[5] Abu Daawuud na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Nyongeza imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim.

[6] Abu ´Awaanah na Abu Daawuud kwa isnadi mbili Swahiyh. Kunyanyua mikono huku ni maoni ya Ahmad na pia maoni ya Maalik na ash-Shaafi´iy.

[7] Abu Daawuud na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[8] Ahmad na at-Tirmidhiy aliyeisahihisha.

[9] Abu ´Awaanah na Abu Daawuud kwa isnadi mbili Swahiyh. Kunyanyua mikono huku ni maoni ya Ahmad na pia maoni ya Maalik na ash-Shaafi´iy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 133-134
  • Imechapishwa: 07/08/2017