64. Mwisho wa “Sharh Usuwl-is-Sunnah”

Tumemaliza kwa upitiaji huu wa haraka haraka na himdi zote zinamstahikia Allaah. Natarajia tumefaidika. Naiusia nafsi yangu na yenu juu ya kumcha Allaah, kumtakasia Yeye nia, kuwa na bidii katika kujifunza elimu na kushikamana barabara na Kitabu cha Allaah, Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mfumo wa Salaf.

Mimi nakushaurini kukihifadhi kitabu hiki kikubwa ambacho ni kidogo kwa kiwango lakini kikubwa kihadhi. Nakunasihini kukihifadhi na kukielewa. Kutokea kwenye hicho ndio mtaviendea vitabu vya ´Aqiydah vilivyoingia kwa undani zaidi vilivyoandikwa na wahenga wetu (Rahimahumu Allaah). Walitambua ni umuhimu gani wa ´Aqiydah na misingi hii mikubwa. Ametangulia kusema Ahmad ya kwamba yule mwenye kufanya kasoro katika msingi wowote miongoni mwa misingi hii basi anatoka katika Ahl-us-Sunnah. Misingi hii inapambanua na kuwatenganisha Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na wengineo. Mnatambua kuwa moja katika misingi hii ni kupenda na kuchukia kwa ajili ya Allaah, kuwachukia Ahl-ul-Bid´ah na kutahadharisha nao. Kuna idadi kubwa ya maimamu ambao wamenakili na kuuthibitisha msingi huu.

Ninamuomba Allaah atuthibitishe sisi na nyinyi katika dini na njia Yake na njia ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na atufanye kushikamana na misingi hii iliyoandikwa na imamu huyu katika kijitabu hiki kilicho kidogo kwa kiwango lakini kikubwa kihadhi.

Allaah atuwafikishe sote katika yale Anayoyapenda na kuyaridhia na atuthibitishe katika Sunnah na uongofu. Hakika Mola wetu ni Mwenye kuyasikia maombi yetu. Namwachia Allaah dini na amana yenu katika ulinzi Wake.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 445
  • Imechapishwa: 08/01/2018