64. Mlango kuhusu kumuapia Allaah


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Jundub bin ´Abdillaah (Rahiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna mtu alisema: “Naapa kwa Allaah kwamba Allaah hatomsamehe fulani.” Allaah (´Azza wa Jall) akasema: “Ni nani huyo anayeniapia Mimi ya kwamba sintomsamehe fulani? Mimi nimemsamehe mtu huyo na nimeyaporomosha matendo yako.”[1]

Ameipokea Muslim.

2- Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Rahiya Allaahu ´anhu) imekuja ya kwamba mtu aliyesema hivi alikuwa ni mtu mwenye kufanya ´ibaadah. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kaongea maneno ambayo yameiharibu dunia yake na Aakhirah yake.”

MAELEZO

Mlango huu ndani yake kuna matishio. Kumuapia Allaah ni kuthubutu kwa Allaah, kunaipunguza Tawhiyd na kuidhoofisha imani.

1- Jundub bin ´Abdillaah (Rahiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna mtu alisema: “Naapa kwa Allaah kwamba Allaah hatomsamehe fulani.” Allaah (´Azza wa Jall) akasema: “Ni nani huyo anayeniapia Mimi ya kwamba sintomsamehe fulani? Mimi nimemsamehe mtu huyo na nimeyaporomosha matendo yako.”

Jundub pia inaweza kusemwa Jundab.

Hadiyth hii ndani yake kuna matahadharisho ya kumuapia Allaah kwamba hatofanya kitu kadhaa kama vile kumsamehe fulani na mfano wake. Yote hii ni dhuluma na kuthubutu. Ni jambo lisilojuzu kwa sababu mtu hajui Allaah atachofanya na hana haki yoyote ya mtu huyo hata kama mtu huyu ni mtenda dhambi mkubwa. Wajibu wako ni kumuombea uongofu. Allaah anaweza kumsamehe pasi na wewe kujua. Haya yanaonyesha ukhatari wa ulimi. Ni wajibu kuuchunga ulimi wako na kutoongea namna hii kwa sababu ni jambo linaipunguza Tawhiyd na imani.

2- Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Rahiya Allaahu ´anhu) imekuja ya kwamba mtu aliyesema hivi alikuwa ni mtu mwenye kufanya ´ibaadah. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kaongea maneno ambayo yameiharibu dunia yake na Aakhirah yake.”

Kilichomfanya kuongea maneno haya mabaya ilikuwa ni ghera na ´ibaadah zake. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa mtu anaweza kuingiwa na ghera mbaya ambapo akathubutu kumuapia Allaah. Anaweza kuwa ni mwenye ghera na anaamrisha mema na kukataza maovu pasi na elimu. Pengine anakataza maovu pasi na elimu. Kwa ajili hiyo ni wajibu mtu kushikamana na vigezo vya Kishari´ah katika kuamrisha mema na kukataza maovu na kukomeka na mipaka ya Allaah. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kaongea maneno ambayo yameiharibu dunia yake na Aakhirah yake.”

Kwa sababu yalikuwa maneno khatari. Katika Hadiyth imekuja:

“Mja atatamka maneno asiyotia manani maana yake ambapo yakamfanya kutupwa Motoni umbali wa mashariki na mgharibi.”[2]

Ameipokea Muslim.

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mja atatamka maneno kwa njia ambayo haikumbainikia yakaamsha hasira za Allaah ambapo Allaah akaandika hasira Zake katika ile Siku atayokutana Naye.”[3]

[1] Muslim (2621).

[2] al-Bukhaariy (6477) na Muslim (2988).

[3] Maalik (1781), at-Tirmidhiy (2319), Ibn Maajah (3969) na al-Haakim (137). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (888).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 178-179
  • Imechapishwa: 14/11/2018