Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

… na uamini Qadar; kheri na shari yake.

MAELEZO

Qadar ni yale mambo Aliyoyakadiria Allaah (Ta´ala) kwa viumbe kutokana na ujuzi Wake uliotangulia na ikapelekea hekima Yake.

Kuamini Qadar kunakusanya mambo manne:

1- Kuamini ya kwamba Allaah (Ta´ala) alikijua kila kitu milele na kwa kudumu, kwa ujumla na kwa upambanuzi. Hili linahusiana na matendo Yake Mwenyewe na matendo ya viumbe Wake.

2- Kuamini kuwa Allaah ameyaandika hayo katika ubao Uliohifadhiwa. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu haya mambo mawili:

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yameandikwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (al-Hajj 22 : 70)

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim kumepokelewa kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Allaah aliandika makadirio ya viumbe miaka elfu khamsini kabla ya kuumba mbingu na ardhi.””

3- Kuamini kwamba kila kinachopitika, hakipitiki isipokuwa kwa matakwa ya Allaah (Ta´ala). Hili linahusiana na matendo Yake Mwenyewe na matendo ya viumbe. Allaah (Ta´ala) amesema juu ya matendo Yake Mwenyewe:

وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاء وَيَخْتَارُ

“Mola wako anaumba anayotaka na kuchagua.” (al-Qaswasw 28 : 68)

وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ

“Allaah anafanya atakavyo.” (Ibraahiym 14 : 27)

هُوَ الَّذِي يُصَوِّرُكُمْ فِي الْأَرْحَامِ كَيْفَ يَشَاءُ

“Yeye ndiye aliyekutieni sura katika matumbo ya uzazi vile atakavyo.” (Aal ´Imraan 03 : 06)

Vilevile amesema (Ta´ala) juu ya matendo ya viumbe:

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَسَلَّطَهُمْ عَلَيْكُمْ فَلَقَاتَلُوكُمْ

“Lau Allaah angelitaka, basi angeliwasaliti juu yenu, wakapigana nanyi.” (an-Nisaa´ 04 : 90)

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ ۖ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ

“Lau angetaka Mola wako, basi wasingeliyafanya hayo. Hivyo basi waachilie mbali na wanayoyazua!” (al-An´aam 06 : 112)

4- Kuamini kuwa viumbe vyote kwa dhati yavyo, sifa zake na harakati zake yameumbwa na Allaah (Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amesema:

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ

“Allaah ni  Muumbaji wa kila kitu; Naye juu ya kila kitu ni mtegemewa.” (az-Zumar 39 : 62)

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

“Ameumba kila kitu kisha akakikadiria kipimo sawasawa.” (al-Furqaan 25 : 02)

Ameeleza kuwa Mtume Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) alisema kuwaambia watu wake:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni na yale yote mnayoyafanya.” (asw-Swaaffaat 37 : 96)

Kuamini Qadar, kutokana na tuliyoeleza, haina maana kuwa kunapingana na mja kuwa na matakwa na uwezo katika kutenda. Shari´ah na uhalisia wa mambo yanafahamisha juu ya kuthibitisha hilo:

Kuhusiana na Shari´ah, Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu matakwa:

فَمَن شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ مَآبًا

“Basi atakaye, achukue njia ya kurudi kwa Mola wake!” (an-Nabaa´ 78 : 39)

فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

”Basi ziendeeni konde zenu vovyote mpendavyo.” (al-Baqarah 02 : 223)

Amesema pia kuhusu uwezo:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا وَأَطِيعُوا

“Basi mcheni Allaah muwezavyo; na sikilizeni na tiini.” (at-Taghaabuun 64 : 16)

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake. Itapata iliyoyachuma na ni dhidi yake iliyojichumia.” (al-Baqarah 02 : 286)

Ama kuhusiana uhalisia wa mambo, kila mtu anajua kuwa ana matakwa na uwezo katika kutenda na kuacha kutenda. Anatofautisha kati ya yale anayoyafanya kwa matakwa yake, kama kutembea, na yale yanayotokea pasi na matakwa yake, kama kutetemeka. Hata hivyo matakwa ya mja na uwezo wake vimefungamana na matakwa na uwezo wa Allaah (Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amesema:

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke. Na hamtotaka isipokuwa Atake Allaah, Mola wa walimwengu.” (at-Takwiyr 81 : 28-29)

Vilevile ulimwengu wote ni milki ya Allaah (Ta´ala). Kwa hivyo hakukuwi chochote katika ulimwengu huu pasi na Yeye kujua hilo na kutaka litokee.

Kuamini Qadar, kutokana na tuliyoeleza, haina maana kuwa inampa mja hoja ya kuacha mambo ya wajibu au kufanya mambo ya maasi. Kutumia hoja kwa hilo ni jambo la batili linaloraddiwa kwa njia nyingi:

1- Maneno Yake (Ta´ala):

سَيَقُولُ الَّذِينَ أَشْرَكُوا لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا أَشْرَكْنَا وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِن شَيْءٍ ۚ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ حَتَّىٰ ذَاقُوا بَأْسَنَا ۗ قُلْ هَلْ عِندَكُم مِّنْ عِلْمٍ فَتُخْرِجُوهُ لَنَا ۖ إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَخْرُصُونَ

“Watasema wale walioshirikisha: “Lau Allaah angetaka, tusingelifanya shirki wala baba zetu na wala tusingeliharamisha chochote.” Hivyo ndivyo walivyokadhibisha wale wa kabla yao mpaka walipoonja adhabu Yetu.  Sema: “Je, mna elimu yoyote mtutolee? Si jengine hamfuati isipokuwa dhana tu, nanyi si lolote isipokuwa mnabuni uongo.”” (al-An´aam 06 : 148)

Lau wangelikuwa na hoja kwa kutumia Qadar, basi Allaah asingeliwaadhibu.

2- Maneno Yake (Ta´ala):

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا

“Mitume ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kutumilizwa Mitume. Na daima Allaah ni Mwenye nguvu asiyeshindika, Mwenye hekima.” (an-Nisaa´ 04 : 165)

Lau Qadar ingelikuwa ni hoja kwa wale wahalifu, basi hoja isingelisita kwa kutumilizwa Mitume kwa sababu kwenda kwao kinyume baada ya kutumwa Mitume kunatokana na Qadar ya Allaah (Ta´ala).

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa Allaah ameshamuandikia mahali pake ima Motoni au Peponi.” Hivyo bwana mmoja akasema: “Je, situtegemee basi hilo, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Hapana. Fanyeni matendo, kwani kila kitu kimerahisishwa.” Kisha akasoma:

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ

”Basi yule anayetoa na akamcha Allaah.” (al-Layl 92 : 05)

Hili ni tamko la al-Bukhaariy. Katika tamko la Muslim imekuja:

“Kila mmoja amefanyiwa wepesi kwa yale aliyoumbiwa.”

Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha kufanya matendo na akakataza kufanya uvivu na kutegemea Qadar.

4- Allaah (Ta´ala) amemwamrisha na akamkataza mja na hakumuwajibishia mja isipokuwa yale mambo anayoyaweza. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

“Basi mcheni Allaah muwezavyo.” (at-Taghaabuun 64 : 16)

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.” (al-Baqarah 02 : 286)

Endapo mja angelikuwa ametenzwa nguvu kutenda, basi angelikuwa amelazimishwa kitu asichoweza kujinasua nacho, jambo ambalo ni batili. Kwa ajili hiyo ndio maana pindi anapofanya maasi kwa ujinga, kwa kusahau au kwa kulazimishwa, anakuwa sio mwenye kupata dhambi, kwa kuwa ni mwenye kupewa udhuru.

5- Qadar ya Allaah (Ta´ala) ni siri iliyofichwa na haijulikani isipokuwa tu baada ya kutokea kile kilichokadiriwa. Matakwa ya mja kwa yale anayoyafanya yametanguliwa kabla ya kitendo chake na hivyo kitendo chake kinakuwa hakitokani na kule kujua kwake Qadar ya Allaah. Kwa hivyo hakuna hoja kwa kutumia Qadar kwa sababu hakuna hoja yoyote kwa kitu ambacho mtu hakijui.

6- Baadhi ya watu wanafanya kila waliwezalo ili kufikia kitu chakulaumika, jambo la kidunia mpaka aweze kukifikia. Hata hivyo hawajiingizi katika matendo mazuri ili baada ya hapo mtu aseme kuwa ni katika Qadar. Kwa nini wanayapa mgongo yale yenye kuwanufaisha katika mambo ya kidini na badala yake wanafanya yale yenye kuwadhuru, halafu baada ya hapo wanailaumu Qadar? Je, mambo haya mawili si kitu kimoja? Mfano huu unaofuata utabainisha hilo:

Hebu tuseme lau kuna mtu amesimama kati ya njia mbili. Moja wapo inamwelekeza mtu katika nchi inayomtia khatarini na nyingine inamwelekeza katika nchi iliotulizana. Ni njia ipi atayochagua? Bila ya shaka atachagua ile njia ya pili ambayo inamwelekeza katika nchi iliotulizana na nzuri. Haiwezekani kwa mtu yeyote mwenye akili kuchagua ile njia ya nchi inayomtia khatarini halafu baada ya hapo akailaumu Qadar. Kwa nini anachagua njia ya Motoni badala ya Peponi, halafu baada ya hapo akailaumu Qadar?

Mfano mwingine mgonjwa huamrishwa kutumia dawa na kukatazwa kula chakula chenye kumdhuru. Akatumia dawa zile na kujiepusha na kile chakula pamoja na kwamba nafsi yake inakipenda. Anafanya yote hayo ili aweze kupona na kusalimika. Hawezi kuacha kutumia dawa yake au kutumia chakula chenye kumdhuru halafu baada ya hapo akailaumu Qadar. Kwa nini basi mwanadamu anaacha yale ambayo Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamemwamrisha au anafanya yale ambayo Allaah na Mtume Wake  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamemkataza, kisha baada ya hapo anailaumu Qadar?

6- Lau yule mwenye kuilaumu Qadar atashambuliwa na mtu, akampora mali yake au akamvunjia heshima yake, kisha akatumia hoja Qadar ya Allaah kwa yale aliyoyafanya, yule mtu hatoikubali hoja yake kamwe. Vipi basi asikubali kutumiwa hoja kwa Qadar ya Allaah juu ya haki yake na badala yake akaitumia juu ya haki ya Allaah (Ta´ala) pindi inapotumiwa vibaya?

Imesemekana kwamba kuna mwizi mmoja aliyestahiki kukatwa mkono aliletwa kwa kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Baada ya kuamrishwa kukatwa mkono wake, mwizi yule akasema: “Ee kiongozi wa waumini! Subiri kwanza! Hakika nimeiba kwa Qadar ya Allaah (Ta´ala).” Hivyo naye akasema: “Na sisi tunaukata kwa Qadar ya Allaah.”

Kuamini Qadar kunapelekea katika matunda ikiwa ni pamoja na:

1- Kumtegemea Allaah (Ta´ala)  wakati mtu anapofanya sababu. Kwa njia ya kwamba mtu asitegemei sababu peke yake, kwa sababu kila kitu kinatokea kwa Qadar ya Allaah (Ta´ala).

2- Mtu asijione pindi anapofikia yale aliyokuwa anayatarajia. Kuyafikia hakutokani na jengine isipokuwa ni neema kutoka kwa Allaah (Ta´ala) kutokana na yale aliyoyakadiria kupitia sababu za kheri na kufaulu. Kule kujikweza kunampelekea kuisahau neema hii.

3- Raha na utulivu wa nafsi kwa yale yatayompitikia kutokana na yale ambayo Allaah (Ta´ala) amekadiria. Hatohuzunika kwa kukosa kile anachokipenda au kwa kupatwa na kitu chenye kuchukiza. Yote hayo yanatokana na Qadar ya Allaah (Ta´ala) na ni Yeye ndiye mwenye ufalme wa mbinguni na ardhini. Ni jambo ambalo ni lazima litokee. Allaah (Ta´ala) amesema juu ya hilo:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa upo katika Kitabu, kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. Ili msisononeke juu ya yale mliyoyakosa na wala msifurahie kwa yale aliyokupeni. Allaah hapendi kila mwenye kujinata, mwenye kujifakharisha.” (al-Hadiyd 57 : 22-23)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ajabu ilioje juu ya jambo la muumini. Kwani hakika jambo lake siku zote huwa ni kheri. Hilo haliwi isipokuwa kwa muumini tu. Anapofikwa na kitu kizuri, basi hushukuru, na hilo likawa ni kheri kwake. Na akifikwa na kitu kibaya, basi husubiri, na hilo likawa ni kheri kwake.”

Ameipokea Muslim[1].

Kuna makundi mawili yamepotoka juu ya Qadar:

1- Jabriyyah. Wanaonelea kuwa mja ametenzwa nguvu katika kutenda na hana matakwa wala uwezo.

2- Qadariyyah. Wanaonelea kuwa mja yuko huru katika matakwa na uwezo na hivyo haathiriwi na matakwa na uwezo wa Allaah (Ta´ala).

Jabriyyah wanaraddiwa kwa Shari´ah na uhalisia wa mambo.

Kuhusu Shari´ah, Allaah (Ta´ala) amethibitisha mja kuwa na uwezo na utashi na akategemeza kitendo kwake. Allaah (Ta´ala) amesema:

مِنكُم مَّن يُرِيدُ الدُّنْيَا وَمِنكُم مَّن يُرِيدُ الْآخِرَةَ

“Miongoni mwenu wako wenye kutaka dunia na miongoni mwenu wako wenye kutaka Aakhirah.” (Aal ´Imraan 03 : 152)

وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ ۖ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ ۚ إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمْ سُرَادِقُهَا

”Sema: “Hii ni haki kutoka kwa Mola wenu; hivyo basi anayetaka aamini, na anayetaka akufuru. Hakika Sisi tumewaandalia madhalimu Moto ambao kuta zake zitawazunguka.”” (al-Kahf 18 : 29)

مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۗ وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ

“Yeyote mwenye kutenda mema, basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na yeyote yule mwenye kutenda uovu, basi ni dhidi yake; na Mola wako si Mwenye kuwadhulumu waja Wake.” (Fuswswilat 41 : 46)

Ama kuhusu uhalisia wa mambo, kila mtu anatambua kwamba kuna tofauti kati ya yale matendo anayoyafanya kwa kutaka kwake mwenyewe, kama kula, kunywa na kufanya biashara, na yale yanayotokea pasi na kutaka kwake mwenyewe, kama kutetemeka kwa sababu ya homa na kuanguka kutoka kwa juu. Matendo ya kwanza ni mwenye kuyafanya kwa matakwa yake pasi na kulazimishwa, tofauti na matendo ya pili hayafanyi kwa matakwa na kwa kupenda kwake.

Qadariyyah wanaraddiwa pia kwa Shari´ah na uhalisia wa mambo.

Kuhusu Shari´ah, Allaah (Ta´ala) ndiye ameumba kila kitu. Kila kitu kinatokea kwa matakwa Yake. Allaah (Ta´ala) amebainisha katika Kitabu Chake kuwa matendo ya waja yanatokea kwa matakwa Yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَـٰكِنِ اخْتَلَفُوا فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

“Na lau angelitaka Allaah, basi wasingelipigana wale ambao walikuja baada yao, baada ya kuwajia hoja za wazi. Lakini walikhitalifiana, basi miongoni mwao wapo walioamini na miongoni mwao wako waliokufuru. Na lau angelitaka Allaah, wasingelipigana, lakini Allaah anafanya atakayo.” (al-Baqarah 02 : 253)

وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ

“Na lau Tungelitaka, basi tungeliipa kila nafsi uongofu wake, lakini imethibiti Kauli kutoka Kwangu kwamba: “Bila shaka Nitaujaza Moto kwa majini na watu pamoja!” (as-Sajdah 32 : 13)

Ama kuhusu uhalisia wa mambo, Allaah (Ta´ala) anamiliki ulimwengu wote na mwanadamu ni mmoja katika walimwengu hawa. Hii ina maana ya kwamba ni mwenye kumilikiwa na Allaah (Ta´ala). Hivyo haiwezekani kwa mwenye kumilikiwa kuwa na uendeshaji katika utawala wa Mmiliki isipokuwa kwa idhini na kutaka Kwake.

[1] 2999.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 110-117
  • Imechapishwa: 02/06/2020