63. Waislamu wote wanaokufa wanatakiwa kuswaliwa swalah ya jeneza hata kama walikuwa watenda madhambi


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Swalah ya jeneza anaswaliwa muislamu aliyekuwa akimpwekesha Allaah. Huyu anaombewa msamaha. Hatakiwi kunyimwa hilo. Wala haitakiwi kuacha kumswalia kutokana na dhambi aliyotenda, sawa iwe kubwa au ndogo. Jambo lake liko kwa Allaah (Ta´ala).”

MAELEZO

Tunawaswalia watenda madhambi waislamu pindi wanapofariki. Vilevile inafaa kumswalia mtu wa Bid´ah. Hata hivyo haifai kwa kiongozi kumswalia mtenda dhambi huyu. Kama ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliacha kumswalia yule mwanamume aliyechukua mateka bila ya ruhusa. Badala yake akasema:

“Mswalieni mwenzenu.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu yule mtu aliyekufa akiwa na deni:

“Mswalieni mwenzenu.” Ndipo Abu Qataadah akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mimi nitamlipia nalo.” Baada ya hapo ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamswalia[2].

Tumekatazwa kuwaswalia makafiri. Hatumswalii kafiri wala mnafiki:

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ ۖ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ

“Wala usimswalie yeyote kamwe miongoni mwao akifa na wala usisimame kaburini kwake [kwa ajili ya kumuombea], kwani hakika wao wamemkufuru Allaah na Mtume Wake na wamekufa hali ya kuwa ni mafasiki.”[3]

Haijuzu kuwaswalia swalah ya jeneza makafiri na wanafiki wanaofariki. Hata hivyo tunamswalia mtenda dhambi na mzushi maadamu bado ni waislamu na hawajakufuru baada ya kusimamikiwa na dalili. Lakini yule kiongozi na mwanachuoni wanatakiwa kuacha kumswalia kwa njia ya kumtia adabu na kuwashtua watu juu madhambi au Bid´ah zake. Pamoja na hivyo hatuwakatazi watu wote kuwaswalia. Bali tunawaambia wamswalie.

[1] at-Tirmidhiy (2710) na Ibn Maajah (2848). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan Ibn Maajah” (571).

[2] al-Bukhaariy (2289).

[3] 09:84

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 444
  • Imechapishwa: 08/01/2018