63. Vipi kuoanisha Hadiyth inayohimiza kumuharakisha maiti na makatazo ya kuzika katika nyakati tatu?

Swali 63: Ni vipi tutaoanisha kati ya makatazo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuswali na kuzika katika nyakati tatu na kati ya Hadiyth inayosema kuharakisha jeneza na jeneza ikawa kwa mfano baada ya alasiri[1]?

Jibu: Hakuna mgongano kati ya Hadiyth hizo mbili. Sunnah ni kuharakisha kumswalia na kumzika maiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanyeni haraka kumwandaa maiti. Akiwa ni mwema basi ni kheri mnazomtangulizia. Akiwa hayuko hivo ni shari mnayoitua kutoka shingo zenu.”[2]

Lakini hali hiyo ikikutana na wakati wa yale masaa matatu basi kutaahirishwa kumswalia na kumzika. ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Saa tatu alikuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitukataza kuswali ndani yake na kuwazika ndani yake wafu wetu; wakati linapochomoza jua mpaka linaponyanyuka, jua linapolingamana sawasawa katikati ya mbingu mpaka lipinduke na jua linapokurubia kuzama mpaka lizame.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Saa tatu zote hizi ni ndogo na haidhuru kuchelewesha kumswalia na kumzika maiti ndani yazo. Allaah (Subhaanah) anayo hekima kubwa katika hilo. Yeye (Subhaanah) ndiye Mwingi wa huruma wa wenye kuhurumia na Mwingi wa hekima wa wenye hekima.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/181-182).

[2] al-Bukhaariy (1315) na Muslim (944).

[3] Ahmad (16926) na Muslim (831).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 27/12/2021