1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kumwondoshea nduguye shida miongoni mwa shida za duniani basi Allaah atamwondoshea shida miongoni mwa shida za siku ya Qiyaamah.”

2 – Ni wajibu kwa waislamu wote kuwatakia mema waislamu na kuhakikisha anaondosha masononeko na shida zao. Yule mwenye kuondosha shida miongoni mwa shida za duniani kutoka kwa muislamu basi Allaah atamwondoshea shida miongoni mwa shida za siku ya Qiyaamah.

3 – Ndugu wa kweli hujulikana kipindi cha tabu. Kila mtu huwa ni rafiki kipindi cha raha. Ndugu wabaya zaidi ni wale wenye kuwapa migongo ndugu zao kipindi cha shida zaidi na miji mibaya zaidi ni ile miji isiyokuwa na mazao rutuba na amani.

4 – al-Hasan al-Baswriy amesema:

“Napendelea zaidi mtu kukidhi haja ya ndugu yake muislamu kuliko kukaa I´tikaaf kwa miezi miwili.”

5 – Ambaye anatambua thawabu basi hatakiwi kuacha kuwasaidia wenzake kutokana na nafasi au mali yake akiweza kufanya hivo. Afanye hivo kabla ya kufikwa na kifo. Kwa kifo yanakatika matendo mema yote na anasikitika kwa yale mema yaliyompita.

6 – Muhitaji hatakiwi kuomba kwa kung´ang´ania. Kuomba kwa king´ang´anizi kunaweza kupelekea mtu asipate kitu. Yule mwenye kupewa anatakiwa kushukuru na yule anayenyimwa anatakiwa kuridhi makadirio. Haitakiwi kuomba katika mahafla, misikiti na maeneo ya hadhara.

7 – ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

“Usiwaombe watu katika vikao na misikiti yao mkawaudhi. Waombeni wanapokuwa majumbani mwao. Atakayepewa, amepewa, na atakayenyimwa, basi amenyimwa.”

8 – Maneno ya ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ni juu ya yule mkarimu. Mkarimu akiomba wakati anapokuwa na wengine na akawa hana, basi huona haya. Anayezungumzwa vibaya akiombwa katika kikao au kwenye msikiti basi kuna uwezekano mkubwa akatoa. Anayesemwa vibaya hatoi kwa sababu ya imani wala muruwa. Anatoa kwa sababu tu anataka watu wamsifu.

9 – Mimi napendekeza mwenye busara ale ngozi na kunyonya mawe na kusubiri juu ya hali hiyo kuliko kumwomba anayesemwa vibaya. Kutoa kwa anayezungumzwa vibaya ni kubaya na kuzuia kwake ni kifo.

10 – Mwenye busara hatakiwi kumwelekea adui, mpumbavu, mtenda dhambi, mwongo wala yule ambaye lengo lake ni maslahi ya nafsi yake wakati anapoomba kusaidiwa. Hatakiwi kuomba mambo mawili kwa wakati mmoja. Asionyeshi pupa kubwa wakati wa kuomba haja yake. Inatosha kwa mtu mtukufu kuitambua haja pasi na kuombwa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 246-250
  • Imechapishwa: 02/09/2021