Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

… kuamini siku ya Mwisho…

MAELEZO

Siku ya mwisho ni siku ya Qiyaamah. Siku hiyo watu watafufuliwa kwa ajili ya kufanyiwa hesabu na malipo. Imeitwa hivo kwa sababu hakuna siku nyingine baada yake. Siku hiyo watu wa Peponi watakaa katika majumba yao na watu wa Motoni katika majumba yao.

Kuamini siku ya mwisho kumekusanya mambo matatu:

1- Kuamini kufufuliwa. Nako ina maana ya wale wafu kurudishiwa uhai tena, baada ya kupulizwa baragumu kwa mara ya pili. Watu watasimama kwenda kwa Mola wa walimwengu. Watakuwa miguu peku, uchi na bila ya kutahiriwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ

“Kama Tulivyoanza uumbaji umbo la mwanzo tutalirudisha – hiyo ni ahadi juu Yetu hakika Sisi tumekuwa ni Wenye kufanya!” (al-Anbiyaa´ 21 : 104)

Kufufuliwa ni jambo la haki lililothibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

ثُمَّ إِنَّكُم بَعْدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ

“Kisha nyinyi baada ya hayo ni wenye kufa. Kisha hakika nyinyi siku ya Qiyaamah mtafufuliwa.” (al-Muuminuun 23 : 15-16)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu watafufuliwa siku ya Qiyaamah wakiwa miguu peku na bila ya kutahiriwa.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Waislamu wameafikiana juu ya kwamba kitatokea. Isitoshe ndivyo inavyopelekea hekima ya Allaah (Ta´ala) kuwawekea viumbe marejeo ya mwisho ambapo atakuja Kuwalipa kwa yale aliyowafaradhishia kupitia Mitume Yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ

“Je, mlidhania kwamba Sisi tulikuumbeni bila kusudio na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?” (al-Mu´minuun 23 : 115-116)

Amesema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

إِنَّ الَّذِي فَرَضَ عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لَرَادُّكَ إِلَىٰ مَعَادٍ

“Hakika Yule aliyekufaridhishia Qur-aan bila shaka atakurudisha mahali pa marejeo.” (al-Qaswasw 28 : 85)

2- Kuamini hesabu na malipo. Mja atafanyiwa hesabu kwa matendo yake na atalipwa kwayo. Hilo limefahamisha na Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم

”Hakika ni Kwetu ndio marejeo yao. Kisha bila shaka ni juu Yetu hesabu yao.” (al-Ghaashiyah 88 : 25-26)

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

“Atakayekuja kwa  jema, basi atalipwa [thawabu] kumi mfano wa hilo, na atakayekuja kwa uovu, basi hatolipwa isipokuwa mfano wa hilo, nao hawatodhulumiwa.” (al-An´aam 06 : 160)

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Tutaweka mizani za uadilifu siku ya Qiyaamah; basi haitodhulumiwa nafsi yoyote ile kitu chochote ijapo ni uzito wa mbegu ya hardali, Tutaileta. Na inatosheleza Kwetu kuwa Wenye kuhesabu.” (al-Anbiyaa´ 21 : 47)

Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah atamjongeza muumini [Naye]. Halafu Ataweka sitara Yake juu yake na kumfunika. Kisha aseme: “Unatambua dhambi kadhaa? Unatambua dhambi kadhaa? Aseme: “Ndio, Mola” mpaka atapoyakubali madhambi yake yote na kuona kuwa sasa ameangamia.  Hapo ndipo atasema: “Nilikusitiri duniani na Mimi hivi leo ninakusamehe.” Baada ya hapo apewe kitabu cha mema yake. Ama kuhusu makafiri na wanafiki, wataitwa mbele ya umati: “Watu hawa ndio wale waliokuwa wakimkadhibisha Mola Wao – laana ya Allaah iwe juu ya madhalimu!””

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Vilevile yamepokelewa mapokezi sahihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Yule mwenye kutaka kufanya tendo jema na akalifanya, basi Allaah humwandikia thawabu kumi na huziongeza mpaka mara mia saba na zaidi ya hapo. Na yule mwenye kutaka kufanya tendo baya na akalifanya, basi Allaah humwandikia tendo baya limoja tu.”

Waislamu wameafikiana juu ya kuwepo kwa hesabu na malipo. Hekima pia inapelekea hivo. Allaah (Ta´ala) ameteremsha Vitabu, akatuma Mitume na akawafaradhishia waja kukubali yale waliyokuja nayo na kuyafanyia kazi yale ambayo ni wajibu kuyafanya. Vilevile amefaradhisha kuwapiga vita wale wenye kumpinga Yeye na akahalalisha damu zao, vizazi vyao, wanawake wao na mali zao. Lau kungelikuwa hakuna hesabu wala malipo, basi yote haya yangelikuwa hayana maana yoyote, kitu ambacho Allaah anatakasika nacho. Allaah (Ta´ala) ameashiria hili pale aliposema:

فَلَنَسْأَلَنَّ الَّذِينَ أُرْسِلَ إِلَيْهِمْ وَلَنَسْأَلَنَّ الْمُرْسَلِينَ فَلَنَقُصَّنَّ عَلَيْهِم بِعِلْمٍ ۖ وَمَا كُنَّا غَائِبِينَ

“Basi kwa hakika Tutawauliza wale waliotumiliziwa na bila shaka tutawauliza Mitume; kisha tutawasimulia kwao kwa ujuzi; na wala hatukukosa kuwepo.” (al-A´raaf 07 : 06-07)

3- Kuamini Pepo na Moto na kwamba ni mahali pa makazi ya milele kwa viumbe.

Pepo ni nyumba ya neema ambayo Allaah (Ta´ala) amewaandalia waumini wenye kumcha. Watu hawa wameamini yale ambayo Allaah amewafaradhishia kuyaamini, wakamtii Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hali ya kuwa ni wenye Ikhlaasw na ni wenye kumfuata Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndani yake mna aina mbalimbali za neema ambazo hakuna yeyote ameshawahi kuziona, kuzisikia hata kujifikiria nazo. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًاۖ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ

“Hakika wale walioamini na wakatenda mema, basi hao ndio viumbe wema kabisa. Malipo yao iko kwa Mola wao: mabustani ya kudumu milele yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo milele. Allaah ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hayo ni kwa yule anayemkhofu Mola wake.” (al-Bayyinah 98 : 07-08)

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاء بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Hakuna yeyote anayejua yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho yakiwa ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.” (as-Sajdah 32 : 17)

Kuhusu Moto ni nyumba ya adhabu ambayo Allaah (Ta´ala) amewaandalia makafiri madhalimu. Watu hawa wamemkanusha na wakawaasi Mitume Yake. Ndani yake mna aina mbalimbali za adhabu na mateso ambayo hakuna yeyote anaweza kujifikiria nazo. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ

“Hivyo basi ogopeni moto ambao mafuta yake ni watu na mawe, umeandaliwa kwa ajili ya makafiri.” (al-Baqarah 02 : 24)

إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمْ سُرَادِقُهَا ۚ وَإِن يَسْتَغِيثُوا يُغَاثُوا بِمَاءٍ كَالْمُهْلِ يَشْوِي الْوُجُوهَ ۚ بِئْسَ الشَّرَابُ وَسَاءَتْ مُرْتَفَقًا

”Hakika Sisi tumewaandalia madhalimu Moto ambao kuta zake zitawazunguka na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta ya moto yanayobabua nyuso. Ubaya ulioje kinywaji hicho na uovu ulioje mahali pa kupumzikia!” (al-Kahf 18 : 29)

إِنَّ اللَّـهَ لَعَنَ الْكَافِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمْ سَعِيرًا الِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ لَّا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا

“Hakika Allaah amewalaani makafiri na amewaandalia Moto uwakao kwa nguvu; ni wenye kudumu humo milele hawatopata mlinzi na wala mwenye kunusuru. Siku zitakapopinduliwa nyuso zao Motoni, watasema: “Laiti tungelimtii Allaah na tungelimtii Mtume.” (al-Ahzaab 33 : 64-66)

Katika kuamini siku ya Mwisho ni pamoja vilevile na kuamini kila kitakachokuwa baada ya kufa. Mfano wa hayo ni haya yafuatayo:

1- Mtihani wa ndani ya kaburi: Baada ya mauti kuzikwa, basi anahojiwa juu ya Mola Wake, dini yake na Mtume wake. Hapa Allaah huwathibitisha wale waumini kwa kuwapa kauli thabiti na hivyo atajibu kwa kusema:

“Mola wangu ni Allaah, dini yangu ni Uislamu na Mtume wangu ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Upande mwingine Allaah atawafanya madhalimu kupotea. Kafiri atasema:

“Aah! Aah! Sijui.”

Mnafiki na yule aliyekuwa na shaka atasema:

“Sijui. Nilisikia watu wakisema kitu na mimi nikawa nimekisema.”

 2- Adhabu na neema za kaburi: Adhabu itakuwa kwa madhalimu kati ya wanafiki na makafiri. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ ۖ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ

“Na lau ungeliwaona madhalimu pale wakiwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamenyosha mikono yao [wakiwaambia]: “Zitoeni nafsi zenu! Hakika leo mnalipwa adhabu ya kutweza kwa yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah pasi na haki na kwa mlivyokuwa mkizifanyia kiburi alama Zake.” (al-An´aam 06 : 93)

Vilevile amesema (Ta´ala) kuhusu Fir´awn:

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni na siku itakayosimama Saa [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa.” (Ghaafir 40 : 46)

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim kumepokelewa kutoka kwa Zayd bin Thaabit kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau isingelikuwa si kuchelea msije kuanguka chini na kupoteza fahamu, basi ningelimuomba Allaah awasikilizeni adhabu ya kaburi kama jinsi mimi ninavyosikia.” Kisha akatugeukia na kusema: “Ombeni kinga kwa Allaah kutokamana na adhabu ya kaburi.” Wakasema: “Tunaomba kinga kwa Allaah kutokamana na adhabu ya kaburi.” Akasema: “Ombeni kinga kwa Allaah kutokamana na adhabu ya kaburi.” Wakasema: “Tunaomba kinga kwa Allaah kutokamana na adhabu ya kaburi.” Akasema: “Ombeni kinga kwa Allaah kutokamana na fitina zenye kuonekana na zilizojificha.” Wakasema: “Tunaomba kinga kwa Allaah kutokamana na fitina zenye kuonekana na zilizojificha.” Akasema: “Ombeni kinga kwa Allaah kutokamana na fitina za Dajjaal.” Wakasema: “Tunaomba kinga kwa Allaah kutokamana na fitina za Dajjaal.”

Kuhusiana na neema za kaburi, zitawapata wale waumini wa kweli. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ

“Hakika wale waliosema: “Mola wetu ni Allaah” kisha wakanyooka, basi Malaika huwateremkia [wakiwaambia] kwamba: “Msikhofu na wala msihuzunike na pokeeni bishara njema ya Pepo ambayo mlikuwa mkiahidiwa.” (Fuswswilat 41 : 30)

فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ  فَلَوْلَا إِن كُنتُمْ غَيْرَ مَدِينِينَ  تَرْجِعُونَهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ فَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ

“Inakuweje basi itapofika roho kooni nanyi wakati huo mnatazama, Nasi kipindi hicho tuko karibu naye zaidi kuliko nyinyi, lakini hamuoni. Basi kwa nini ikiwa mnadhani kuwa hamuwajibiki malipo? Muirudishe, mkiwa ni wakweli? Basi anayefariki akiwa miongoni mwa waliokurubishwa, basi ni raha na manukato na mabustani yenye neema.” (al-Waaqi´ah 56 : 83-89)

al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya muumini baada ya kuwajibu wale Malaika wawili humjia ndani ya kaburi lake:

“Hunadi Mwenye kunadi kutoka mbinguni: “Mja Wangu amesema kweli. Mtandikieni katika matandiko ya Peponi, mvalisheni katika mavazi ya Peponi na mfungulieni mlango katika milango ya Peponi.” Azungukwe na harufu na manukato yake. Baada ya hapo kaburi lake lipanuliwe umbali wa jicho lake linapofika.”

Ameipokea Ahmad na Abu Daawuud katika Hadiyth ndefu.

Kuamini siku ya Mwisho kunapelekea matunda ikiwa ni pamoja na:

1- Shauku na pupa ya kufanya matendo mema kwa kutaraji kulipwa siku hiyo.

2- Kuogopa kufanya maasi na kuyafurahikia kwa kuchelea adhabu ya siku hiyo.

3- Inampa liwazo muumini juu ya yale mambo anayoyakosa duniani kwa kutaraji kupata neema na thawabu za Aakhirah.

Makafiri wamepinga kufufuliwa baada ya kufa na kudai ya kwamba jambo hilo haliwezekani. Madai haya ni batili na Shari´ah, hisia na akili vimejulisha juu ya ubatilifu wake.

Kuhusu Shari´ah, Allaah amesema (Ta´ala):

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Waliokufuru wamedai kwamba kamwe hawatofufuliwa. Sema: “Bali ndio! Naapa kwa Mola wangu, bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda; na hayo kwa Allaah ni mepesi.” (at-Taghaabuun 64 : 07)

Jambo hili vitabu vyote vilivyoteremshwa kutoka mbinguni vimekubaliana juu yake.

Kuhusu hisia, Allaah amewaonyesha waja Wake jinsi anavyohuisha wafu katika dunia. Katika Suurah “al-Baqarah” ipo mifano mitano juu ya hilo:

1- Watu wa Muusa wakati walipomwambia:

لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّـهَ جَهْرَةً

“Hatutokuamini mpaka tumuone Allaah waziwazi.” (al-Baqarah 02 : 55)

Allaah (Ta´ala) akawafisha kisha baada ya hapo akawahuisha. Allaah (Ta´ala) anasema juu ya hilo wakati alipokuwa akiwazungumzisha wana wa israaiyl:

وَإِذْ قُلْتُمْ يَا مُوسَىٰ لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْكُمُ الصَّاعِقَةُ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ ثُمَّ بَعَثْنَاكُم مِّن بَعْدِ مَوْتِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Na kumbukeni mliposema: “Ee Muusa! Hatutokuamini mpaka tumuone Allaah waziwazi”; ikakunyakueni [adhabu ya] radi nanyi mnatazama. Kisha Tukakufufueni baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru.” (al-Baqarah 02 : 55-56)

2- Kisa cha yule muuliwaji ambaye wana wa israaiyl waligombana juu yake. Allaah (Ta´ala) akawaamrisha wachinje ng´ombe na halafu wapige kiungo cha ng´ombe huo ili aweze kuwaeleza ni nani aliyemuua. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu tukio hilo:

وَإِذْ قَتَلْتُمْ نَفْسًا فَادَّارَأْتُمْ فِيهَا ۖ وَاللَّـهُ مُخْرِجٌ مَّا كُنتُمْ تَكْتُمُونَ فَقُلْنَا اضْرِبُوهُ بِبَعْضِهَا ۚ كَذَٰلِكَ يُحْيِي اللَّـهُ الْمَوْتَىٰ وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ

“Na kumbukeni mlipoiua nafsi, kisha mkakhitilafiana kwayo, na Allaah ni Mwenye kutoa hayo mliyokuwa mkiyaficha – Ndipo Tukasema: “Mpigeni kwa baadhi ya sehemu yake [huyo ng’ombe]!” Namna hiyo ndivo Allaah anavyohuisha wafu na anakuonyesheni ishara Zake huenda mkatia akilini.” (al-Baqarah 02 : 72-73)

3- Kisa cha watu waliotoka majumbani mwao wakikimbia kifo. Walikuwa ni maelfu. Allaah (Ta´ala) akawafisha kisha baadaye akawahuisha. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu hilo:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ خَرَجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَهُمْ أُلُوفٌ حَذَرَ الْمَوْتِ فَقَالَ لَهُمُ اللَّـهُ مُوتُوا ثُمَّ أَحْيَاهُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُون

“Je, hukuwaona wale ambao walitoka kutoka majumbani mwao nao wakiwa ni maelfu wakikhofu mauti? Allaah akawaambia: “Kufeni” kisha akawahuisha. Hakika Allaah ni Mwenye fadhilah juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.” (al-Baqarah 02 : 243)

4- Kisa cha mtu ambaye alipita katika kijiji kisichokuwa na watu na akaona kuwa ni jambo lisilowezekana Allaah (Ta´ala) kuwafanye tena kuwa hai. Hivyo basi Allaah (Ta´ala) akamfisha kwa miaka mia na halafu akamuhuisha. Allaah (Ta´ala) amesema juu ya tukio hilo:

أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّـهُ بَعْدَ مَوْتِهَا ۖ فَأَمَاتَهُ اللَّـهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ ۖ قَالَ كَمْ لَبِثْتَ ۖ قَالَ لَبِثْتُ يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ ۖ قَالَ بَل لَّبِثْتَ مِائَةَ عَامٍ فَانظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ ۖ وَانظُرْ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجْعَلَكَ آيَةً لِّلنَّاسِ ۖ وَانظُرْ إِلَى الْعِظَامِ كَيْفَ نُنشِزُهَا ثُمَّ نَكْسُوهَا لَحْمًا ۚ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ قَالَ أَعْلَمُ أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Au [hukuzingatia mfano wa] kama yule aliyepita katika kijiji nacho ni kilichoporomoka kabisa juu ya mapaa yake – akasema: “Vipi Allaah atahuisha kijiji hichi baada ya kufa kwake?” Basi Allaah alimfisha miaka mia, kisha akamfufua. Akasema: “Umekaa muda gani?” Akasema: “Nimekaa siku au sehemu ya siku”. [Allaah] akasema: “Bali umekaa miaka mia, basi kitazame chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika na mtazame punda wako – na tutakufanya uwe ishara kwa watu – na itazame mifupa [ya punda] namna tunavyoinyanyua, kisha tunaivisha nyama.” Basi ilipombainikia alisema: “Sasa nimejua kwamba hakika Allaah juu ya kila jambo ni muweza.” (al-Baqarah 02 : 259)

5- Kisa cha Ibraahiym wakati alipomuomba Allaah (Ta´ala) kumuonyesha jinsi anavyohuisha wafu. Allaah akamwamrisha achinje ndege wanne. Halafu akamwamrisha atenganishe vipande vya wale ndege pembezoni mwa majabali na halafu awaite. Basi vile vipande vikaungana na wale ndege wakaruka kurudi kwa Ibraahiym. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu hilo:

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ۖقَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِّنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِّنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا ۚ وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Na kumbuka aliposema Ibraahiym: “Mola wangu! Nionyeshe ni vipi unahuisha wafu?” Akasema: “Je, kwani huamini?” Akasema: “Ndio, lakini moyo wangu upate kutulia.” Akasema: “Basi chukua ndege wanne wazoeshe kwako, kisha weka juu ya kila jabali katika hao ndege sehemu yao, kisha waite watakujia mbio. Na tambua kwamba hakika Allaah ni Mwenye nguvu zisizoshindika, Mwenye hekima.” (al-Baqarah 02 : 260)

Hii ni mifano ya kihisia ya kihalisi inayojulisha kwamba inawezekana wafu wakafufuliwa. Vilevile kumeshatangulia ishara kwa yale aliyoyafanya Allaah (Ta´ala) katika miujiza ya ´Iysaa bin Maryam kwa kuhuisha wafu na kuwatoa ndani ya makaburi yao kwa idhini ya Allaah (Ta´ala).

Kuhusu akili, kuna dalili kwa njia mbili:

1- Allaah (Ta´ala) ameumba mbingu, ardhi na vile vilivyomo ndani yake. Yeye ndiye ameviumba kutokea mwanzo. Yeye ambaye ni muweza wa kuanza kuumba hawezi kushindwa kuwarudisha. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ

“Naye ndiye Aliyeanzisha uumbaji kisha anaurudisha; nayo ni mepesi mno Kwake.” (ar-Ruum 30 : 27)

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ

“Kama Tulivyoanza uumbaji umbo la mwanzo tutalirudisha – hiyo ni ahadi juu Yetu hakika Sisi tumekuwa ni Wenye kufanya!” (al-Anbiyaa´ 21 : 104)

Allaah amesema hali ya kuwa ni mwenye kuamrisha kuwaraddi wale wenye kukanusha kuhuisha mifupa baada ya kuwa imeshaoza:

قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ

“Sema: “Ataihuisha Yule aliyeianzisha mara ya kwanza; Naye ana ujuzi wa kila uumbaji.” (Yaa Siyn 36 : 79)

2- Wakati fulani ardhi inakuwa ni yenye kukosa rutuba, maiti na haina miti. Inapoteremshwa mvua juu yake inaanza kuchipuka, inakuwa kijani na kuchipua kila aina ya mimea mizuri. Yule mwenye uwezo wa kuipa uhai baada ya kufa kwake, ni muweza vilevile wa kuwahuisha wafu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ ۚ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۚ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Na miongoni mwa alama Zake ni kwamba utaona ardhi imenyongeka, basi Tunapoiteremshia maji, hutaharaki na kuumuka. Bila shaka Yule aliyeihuisha, bila shaka ni Mwenye kuhuisha wafu, hakika Yeye juu ya kila jambo ni muweza.” (Fuswswilat 41 : 39)

وَنَزَّلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً مُّبَارَكًا فَأَنبَتْنَا بِهِ جَنَّاتٍ وَحَبَّ الْحَصِيدِ وَالنَّخْلَ بَاسِقَاتٍ لَّهَا طَلْعٌ نَّضِيدٌ رِّزْقًا لِّلْعِبَادِ ۖ وَأَحْيَيْنَا بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا ۚ كَذَٰلِكَ الْخُرُوجُ

“Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, kisha tukaotesha kwayo mabustani na nafaka za kuvunwa. Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi. Ni riziki kwa waja na tukahuisha kwayo nchi iliyokufa, hivyo ndivyo utakavyokuwa ufufuaji.” (Qaaf 50 : 09-11)

Kuna watu wamepotea wanaokanusha adhabu na neema za ndani ya kaburi. Wanadai kuwa hilo ni jambo lisilowezekana kwa sababu linaenda kinyume na uhalisia wa mambo. Hoja yao ni eti lau mtu atamfufua mfu ndani ya kaburi, basi atampata kama alivyokuwa kabla na kaburi halitogeuka kuwa pana wala lenye kubana.

Madai haya ni batili kwa mujibu wa Shari´ah, hisia na akili.

Kuhusu na Shari´ah, tayari yamekwishatangulia maandiko yanayofahamisha juu ya kuthibiti kwa adhabu na neema za ndani ya kaburi.

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amepokea yafuatayo:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka katika baadhi ya mabustani ya al-Madiynah na akasikia sauti za watu wawili wakiadhibiwa ndani ya makaburi yao.”

Halafu akataja Hadiyth na ndani yake imetajwa:

“Mmoja wao alikuwa hajihifadhi na mkojo.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mmoja wao alikuwa hajihifadhi na mkojo na yule mwingine alikuwa akieneza uvumi.”

Kuhusu hisia, wakati fulani mwenye kulala anaota kuwa yuko sehemu ambayo ni kunjufu na pazuri na ananeemeka. Lakini mtu pia anaweza kuota kuwa yuko sehemu penye kubana na penye kutisha na akahisi maumivu. Wakati mwingine pengine akafikia mpaka kuamka kutokana na ndoto aliyoota. Pamoja na hivyo bado mtu anakuwa amelala kwenye kitanda hichohicho na katika hali ileile aliyokuwemo mwanzo. Ndoto ni nduguye kifo. Kwa ajili hii ndio maana Allaah (Ta´ala) ameipa jina la “kifo”. Allaah (Ta´ala) amesema:

اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

“Allaah huzipokea roho pindi zinapokufa, na zile zisizokufa katika usingizi wake, basi huzizuia ambazo amezihukumia mauti na huzituma nyingine mpaka muda wake maalum uliopangwa. Hakika katika hayo bila shaka kuna alama kwa watu wanaotafakari.” (az-Zumar 39 : 42)

Kuhusu akili, mwenye kulala anaweza kuota ndoto ambayo baadaye ikatokea kikweli. Vilevile pengine hata mtu akamuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sifa yake. Yule mwenye kumuona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sifa  yake, basi atakuwa amemuona kikweli. Pamoja na hivyo muotaji amelala kwenye kitanda chake akiwa mbali na kile alichokiota. Ni vipi iwe ni jambo lisilowezekana Aakhirah ikiwa hili limewezekana hapa duniani?

Kuhusu mategemezi yao kwa yale waliyodai kwamba endapo mtu atamfufua mfu ndani ya kaburi, basi atampata kama alivyokuwa kabla na kaburi halitogeuka kuwa pana wala lenye kubana, yanajibiwa kwa njia zifuatazo:

1- Haijuzu kupingana na yaliyokuja na Shari´ah kwa hoja tata kama hizi. Laiti mpingaji huyu angelizingatia yaliyokuja na Shari´ah kwa njia sahihi, basi angelijua ubatilifu wa hoja hizi tata. Kumesemwa:

Ni wangapi wenye kukosoa kauli sahihi?

Sababu yake ni kutokana na ufahamu mbaya

2- Hali za maisha ya ndani ya kaburi ni katika mambo yaliyofichikana ambayo hisia haziwezi kuyafahamu. Lau ingelikuwa inawezekana yakafahamika kwa hisia, basi mtu angelipoteza natija ya kuamini mambo yaliyofichikana. Vilevile ingelipelekea wale wenye kuamini mambo yenye kufichikana na wenye kuyakanusha wangelikuwa sawa.

3- Adhabu, neema na kupanuka na kubana kwa makaburi yanafahamika na yule maiti peke yake na si mwengine. Linaweza kufananishwa na mtu mwenye kulala kwenye kitanda chake na akaota ya kwamba ima yuko sehemu yenye kubana na kutisha au vilevile sehemu ambayo ni pana na pazuri. Hata hivyo sehemu yake alipolala pasibadilike tofauti na mwingine. Bado yuko chumbani mwake na kati ya kitanda na shuka yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiteremshiwa Wahy na huku amekaa na Maswahabah wake. Akisikia Wahy tofauti na Maswahabah ambao hawausikii. Wakati mwingine inatokea Malaika huja kwa umbile la binadamu na akaongea naye. Pamoja na hivyo Maswahabah wasimuone wala kumsikia yule Malaika.

4- Fahamu za viumbe zimewekewa mpaka kwa mujibu wa fahamu ambazo Allaah (Ta´ala) amewawezesha. Hawawezi kufahamu yote yaliyopo. Mbingu na ardhi saba na vile vilivyomo ndani yake na kila kitu kinamsabihi Allaah kwa njia ya kikweli. Wakati mwingine Allaah (Ta´ala) anawasikilizisha wale awatakao katika viumbe Wake. Pamoja na hivyo hili ni jambo lililofichikana kwetu. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu hilo:

تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ

“Zinamsabihi mbingu saba na ardhi na vilivyomo humo na hakuna kitu chochote isipokuwa pia kinasabihi kwa sifa Zake njema, lakini hamfahamu namna wanavyomsabihi.” (al-Israa´ 17 : 44)

Vivyo hivyo mashaytwaan na majini. Wanakwenda na kurudi katika ardhi. Majini walikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakasikia kisomo chake na halafu wakarudi kwenda kwa wenzao kuwaonya. Pamoja na haya wamefichwa kwetu. Allaah (Ta´ala) amesema juu ya hilo:

يَا بَنِي آدَمَ لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُم مِّنَ الْجَنَّةِ يَنزِعُ عَنْهُمَا لِبَاسَهُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوْآتِهِمَا ۗ إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ ۗ إِنَّا جَعَلْنَا الشَّيَاطِينَ أَوْلِيَاءَ لِلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ

“Enyi wana wa Aadam! Asikufitinisheni shaytwaan kama alivyowatoa wazazi wenu katika Pepo, akiwavua nguo zao ili awaonyeshe sehemu zao za siri. Hakika yeye anakuoneni yeye na kabila lake na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya mashaytwaan kuwa ni marafiki kwa wale wasioamini.” (al-A´raaf 07 : 27)

Ikiwa viumbe hawawezi kufahamu kila kilichopo, basi haijuzu kukanusha mambo yaliyothibiti miongoni mwa mambo yaliyofichikana ambayo hayafahamiki na viumbe.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 99-110
  • Imechapishwa: 02/06/2020