63. Baadhi ya faida za kuamini Qadhwaa´ na Qadar


Tano: Kuhusu faida ya kuamini Qadhwaa´na Qadar. Kuamini Qadhwaa´ na Qadar kuna faida nyingi:

Ya kwanza: Faida kubwa kuliko zote ni kukamilisha nguzo za imani. Anayepinga Qadhwaa´ na Qadar hakukamilisha nguzo za imani ambazo amefasiri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtu kuziamini:

“Kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake na kuamini Qadar kheri na shari yake.”

Ya pili: Mja anakuwa si mwenye kujali dhana na woga. Anakuwa ni mwenye kwenda zake na huku akitambua kuwa kile alichomkadiria Allaah kitakuja tu, ni mamoja akae au asikae. Kwa ajili hii pindi wanafiki siku ya Uhud waliposema:

الَّذِينَ قَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ وَقَعَدُوا لَوْ أَطَاعُونَا مَا قُتِلُوا ۗ قُلْ فَادْرَءُوا عَنْ أَنفُسِكُمُ الْمَوْتَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Wale waliowaambia ndugu zao nao wakakaa [hawakwenda vitani]: “Lau wangelitutii basi wasingeliuawa.” Sema: “Basi ziondoleeni nafsi zenu mauti mkiwa ni wakweli.” (03:168)

Kukaa nyumbani hakumzuii mtu kutokana na kufa kama ambavyo vilevile kutoka kwenda katika Jihaad hakumfanyi mtu akafa au kuleta kifo ikiwa Allaah hakukikadiria. Ni kweli kwamba ni sababu, lakini ikiwa Allaah hakukikadiria hakina athari na wala hakileti natija yoyote. Ni wangapi wametoka kwenda vitani na wamerudi wakiwa salama salimina. Khaalid bin Waliyd (Radhiya Allaahu ´anh) yalipomfika mauti alisema:

“Mwilini mwangu hakuna shibri hata moja isipokuwa kuna kovu la kipigo.”[1]

Alikuwa ni mtu anatamani sana kufa shahidi. Alishuhudia vita vikubwa na akatamani sana auawe katika njia ya Allaah. Lakini hata hivyo Allaah hakumwandikia hivo.

Kuamini Qadhwaa´ na Qadar kunamfanya mtu kuwa na ushujaa, kutangulia na kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kukaa hakumfidishi mtu kitu. Amesema (Ta´ala):

قُل لَّوْ كُنتُمْ فِي بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ الَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ

“Sema: “Lau mngelikuwa majumbani mwenu, bila shaka wangejitokeza wale walioandikiwa kuuwawa kwenye mahali pa kuangukia wafe.” (03:15)

أَيْنَمَا تَكُونُوا يُدْرِككُّمُ الْمَوْتُ وَلَوْ كُنتُمْ فِي بُرُوجٍ مُّشَيَّدَةٍ

“Popote mtakapokuwa yatakufikieni mauti, japo mkiwa katika ngome zilizo na nguvu.” (04:78)

Qadhwaa´ ni lazima itekelezeke na itokee.

Kwa hivyo hakuna faida yoyote ya mtu kukaa na kuacha kufanya sababu za faida na kuepuka sababu mbaya. Haya yanamfanya mtu kuwa na ujasiri na ushujaa wa kumuamini Allaah (´Azza wa Jall). Vilevile kunamfanya mtu asiwe na mashaka, wasiwasi na kuamini mikosi inayowapata watu wengi. Kunamuondoshea mtu kuwa na wasiwasi. Kwa ajili watu wa imani hawakuwa wakichelewa katika kutafuta mambo yaliyo na kheri na faida. Kwa sababu walikuwa ni wenye kuamini Qadhwaa´ na Qadar. Hawakuwa ni wenye kuogopa kufa na kuuawa. Ikiwa kifo kimeshaandikwa kwako kitakujia tu hata kama hutokiendea, na kama hujaandikiwa hakitokufika hata kama utakuwa katika khatari ilio kubwa.

Ya tatu: Mtu havunjiki moyo pindi anapofikwa na tatizo. Kwa sababu anaamini kuwa limepitika kwa Qadhwaa´ na Qadar ya Allaah. Hili linasahilisha kukabiliana na matatizo. Hivyo mtu anakuwa si mwenye kukata tamaa hajipigi kwenye mashavu, hapasui nguo na haiti kwa wito wa kipindi cha washirikina. Kinyume chake anakuwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wabashirie wenye kusubiri – wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.” (02:155-157)

Ni wale ambao wanapofikwa na matatizo hawazilaumu nafsi zao na kusema ni kwa sababu hii na ile. Wanaridhia Qadhwaa´ na Qadar ya Allaah na kwamba tatizo hilo lilikuwa lenye kutokea kwa hali yoyote ile aliyokuwa Allaah kishakadiria. Kilichokadiriwa kinatokea kwa idhini ya Allaah. Wanasema:

إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Endapo utafikwa na jambo usisemi “lau ningefanya kadhaa ingelikuwa kadhaa na kadhaa”. Badala yake unatakiwa kusema “Allaah ameshakadiria. Anafanya alitakalo.””[2]

Haya yanamsahilishia mtu matatizo yake na badala yake anaridhia na kujisalimisha na Qadhwaa´ na Qadar ya Allaah. Hizi ni faida tatu zinazopatikana kwa kuamini Qadhwaa´ na Qadar:

Kwanza: Kukamilisha nguzo za imani.

Pili: Kuamini Qadhwaa´ na Qadar kunamfanya mtu kuwa na nguvu, ushujaa na kuwa msitari wa mbele katika kufanya mambo ya kheri.

Tatu: Kuamini Qadhwaa´ na Qadar kunamuwepesishia muislamu yale matatizo yanayomfika.

Kuhusiana na ambaye haamini Qadhwaa´ na Qadar utamuona ni mwenye kuvunjika moyo, kukasirika na hufika na yakumfika.

[1] Taariykh Dimashq (16/273) ya Ibn ´Asaakir

[2] Muslim (34) na (2667)