Kuna aina mbili za ufanyaji mzaha:

1- Kucheza shere ambako kuko wazi. Kama mfano wa yule ambaye Aayah iliteremka kwa ajili yake wakati waliposema:

“Hatujapata kuona watu kama wasomi wetu hawa, matumbo yao yanapenda kula sana, ndimi zao zinasema wongo na ni waoga wakati wa mapambano.”

au walisema maneno mfano wa hayo katika maneno ya wenye kucheza shere. Wengine husema:

“Dini yenu hii ni dini ya tano.”

Wengine husema:

“Dini yenu ni nyonge.”

Wengine, pindi wanapowaona wale wanaoamrisha mema na kukemea maovu, husema:

“Wanakujieni watu wa dini.”

wanasema hivo kwa njia ya kuwachezea shere. Kuna maneno mengine mengi ambayo hayadhibitiwi isipokuwa kwa kujikalifisha ambayo ni khatari zaidi kuliko maneno ya wale ambao Aayah iliteremka kwa ajili yao.

2- Kucheza shere ambako hakuko wazi. Nayo ni bahari isiyokuwa na ufuo. Kwa mfano kufanya ishara kwa macho, kufanya ishara kwa mdomo, kutoa ulimi nje, kufanya ishara za mkono wakati wa kuisoma Qur-aan au Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au wakati  anapoamrishwa mema na kukatazwa maovu[1]. Mfano wa haya ni yale yanayosemwa na baadhi yao kwamba Uislamu hauendani na karne ya ishirini na kwamba unaendana na karne za katikati, kwamba ni kirudi nyuma, kwamba ndani yake kuna ugumu na unyama katika kutekeleza adhabu za Kishari´ah na kuaziriwa, kwamba umemdhulumu mwanamke haki zake kwa vile umehalalisha talaka, kuoa wake wengi, wanaposema kwamba kuhukumu kwa sheria za wanadamu ni bora kwa watu kuliko kuhukumu kwa Uislamu, wanasema juu ya yule mwenye kulingania katika Tawhiyd na kukemea kuabudia makaburi kwamba ana msimamo mkali au kwamba anataka kufarikisha umoja wa waislamu, kwamba ni Wahhaabiy, madhehebu ya tano na mfano wa maneno kama hayo ambayo yote yanaitukana dini na watu wake na kuifanyia istihzai ´Aqiydah sahihi. Miongoni mwa hayo ni kule kucheza kwao shere na yule aliyeshikamana barabara na moja katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo wanasema kwamba dini haiko katika nywele wakikusudia kufanya mzaha na ndevu na mfano wa matamshi kama haya mabaya.

[1] Majmuu´-ut-Tawhiyd an-Najdiyyah, uk. 409

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 118-119
  • Imechapishwa: 26/03/2020