62. Nguzo ya kumi na moja: Tashahhud ya mwisho

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tashahhud ya mwisho ni nguzo na ni wajibu kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kabla hatujafaradhishiwa Tashahhud tulikuwa tukisema: “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, salaam zimwendee Jibriyl na Miykaaiyl.” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Hapana kusema “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, kwani hakika Allaah ni ndiye as-Salaam (Mwenye kutoa amani). Lakini semeni:

التحيات لله، و الصلوات و الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”

MAELEZO

Tashahhud ya mwisho ni nguzo ya kumi na moja miongoni mwa nguzo za swalah. Hili ni kwa mujibu wa Hanaabilah[1]. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amepita juu ya madhehebu yao.

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amejengea dalili ya kwamba ni nguzo kwa kusema:

kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kabla hatujafaradhishiwa Tashahhud tulikuwa tukisema: “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, salaam zimwendee Jibriyl na Miykaaiyl.” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Hapana kusema “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, kwani hakika Allaah ni ndiye as-Salaam (Mwenye kutoa amani). Lakini semeni:

التحيات لله، و الصلوات و الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah [pindi anaposema hivo basi inamgusa kila mja mwema mbinguni na ardhini]. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”[2]

Maneno yake Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh:

“Kabla hatujafaradhishiwa Tashahhud tulikuwa tukisema… “[3]

yanafahamisha ya kwamba Tashahhud ya mwisho ni nguzo.

Miongoni mwa dalili vilevile ni yale aliyopokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinishika mkono wangu kwa mikono yake miwili na akanifunza Tashahhud kama anavyonifunza Suurah katika Qur-aan:

التحيات لله، و الصلوات و الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله  و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah [pindi anaposema hivo basi inamgusa kila mja mwema mbinguni na ardhini]. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”

Tulikuwa tukisema hivo wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado yupamoja nasi. Alipofariki tukawa tunasema:

السلام على النبي

“Amani iwe juu ya Mtume.”[4]

Yapo matamshi mbalimbali ya Tashahhud. Tamko ambalo ni Swahiyh zaidi ni tamko la Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Kwa sababu ameliwekea mkazo kwa kusema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinishika mkono wangu kwa mikono yake miwili na akanifunza Tashahhud kama anavyonifunza Suurah katika Qur-aan.”

[1] Tazama ”al-Mughniy” (01/366).

[2] al-Bukhaariy (6251) na Muslim (397).

[3] an-Nasaa´iy (03/40) kupitia kwa Ibn Mas´uud.

ad-Daaraqutwniy amesema:

“Cheni ya wapokezi hii ni Swahiyh.” (Sunan ad-Daaraqutwniy (01/350)).

al-Bayhaqiy amesema:

“Cheni ya wapokezi hii ni Swahiyh.” (as-Sunan al-Kubraa (02/138)).

Ibn Mulaqin amesema:

“Hadiyth hii ni Swahiyh.” (al-Badr al-Muniyr (04/13).

[4] al-Bukhaariy (6265) na Muslim (402).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 92-93
  • Imechapishwa: 24/06/2022