Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاحْفَظُواْ أَيْمَانَكُمْ

”Hifadhini viapo vyenu.” (al-Maaidah 05:89)

2- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kiapo kinaweza kumshawishi mnunuzi kununua bidhaa, lakini kunaondosha na baraka.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

3- Salmaan (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu aina tatu hatowasemeza Allaah, hatowatakasa na watakuwa na adhabu kali: mzee mzinifu, mtu fakiri mwenye kiburi na mtu ambaye kamfanya Allaah ndio bidhaa yake; hanunui isipokuwa kwa kuapa na wala hauzi isipokuwa kwa kuapa.”[2]

Ameipokea at-Twabaraaniy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

4- Imesihi kupokelewa kutoka kwa ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu bora katika Ummah wangu ni wale wa karne yangu, kisha wale watakaowafuatia, kisha wale watakaowafuatia. Kisha baadaye kutakuja watu wanaoshuhudia bila kuombwa kushuhudia, watakuwa makhaini na wala hawatoaminiwa, wanaweka nadhiri na wala hawatekelezi na kutadhihiri kwao unene.”

´Imraan amesema:

“Sikumbuki alisema baada ya karne yangu mara mbili au mara tatu.”[3]

Ameipokea Muslim.

5- Amepokea vilevile kutoka kwa  Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Bora ya watu ni wa karne yangu, kisha watakaowafuatia, kisha watakaowafuatia. Halafu watakuja watu ambao ushahidi wao unatangulia viapo vyao na viapo vyao vinatangulia ushahidi wao.”[4]

6- Ibraahiym amesema:

“Pindi tulipokuwa wadogo walikuwa wakitupiga kwa kuapa na kwa kutoa ushahidi.”[5]

MAELEZO

Mwandishi alichokusudia ni kwamba jambo la kuapa kwa wingi linaipunguza imani na Tawhiyd kwa sababu kuapa kwa wingi ni jambo linapelekea katika yafuatayo:

1- Kuchukulia wepesi na kutojali.

2- Uongo.

3- Kumdhania uongo.

Mwenye kuapa sana hutumbukia katika uongo. Kwa ajili hiyo ndio maana inatakiwa kujiepusha na kuapa kwa wingi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاحْفَظُواْ أَيْمَانَكُمْ

”Hifadhini viapo vyenu.”

Amri inapelekea uwajibu. Ni wajibu kuchunga viapo isipokuwa wakati wa haja. Muumini anatakiwa kuhifadhi na kutekeleza viapo vyake isipokuwa wakati wa haja, manufaa makubwa ya Kishari´ah, magomvi na mfano wake. Havitakiwi kukithirishwa. Kwa sababu kuna khatari mtu akamdhania uongo.

2- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kiapo kinaweza kumshawishi mnunuzi kununua bidhaa, lakini kunaondosha na baraka.”

Katika upokezi mwingine ametajwa “Mtume”. Ni dalili inayofahamisha kwamba kuapa kwa wingi kunapelekea mtu kutumbukia katika makosa. Mtu huyu anaapa kwa sababu anataka kuuza bidhaa yake. Lakini anaingia khatarini kwa kukosa faida na kukosa baraka. Kwa hivyo anauza bidhaa yake kwa kuapa kwa jina la Allaah kwamba iko namna hii na ile na matokeo yake akawaghuri wengine na huenda wakamsadikisha na wakainunua, lakini hata hivyo inakosa faida kwa sababu ya kule kuchukulia kwake wepesi wa kiapo.

Muslim amepokea kupitia kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh):

“Watu aina tatu hatowasemeza Allaah, hatowatakasa na watakuwa na adhabu kali: mwanaume mwenye kuvaa nguo ndefu yenye kuvuka kongo mbili za miguu, mzee mzinifu, mtu fakiri mwenye kiburi na mtu ambaye kamfanya Allaah ndio bidhaa yake; hanunui isipokuwa kwa kuapa na wala hauzi isipokuwa kwa kuapa.”[6]

Bidhaa inaweza kuuzika kwa kiapo cha uongo na kiapo cha ukweli, lakini kuapa kwa wingi ni jambo linamwingiza mtu katika makosa. Tamaa nyingi inaweza kumfanya muuzaji kuanza kudanganya. Kwa ajili hiyo ni wajibu kwa mtu kutahadhari. Viapo hivi vinapelekea kukosekana baraka na kuingia katika madhambi.

3- Salmaan (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu aina tatu hatowasemeza Allaah, hatowatakasa na watakuwa na adhabu kali: mzee mzinifu, mtu fakiri mwenye kiburi na mtu ambaye kamfanya Allaah ndio bidhaa yake; hanunui isipokuwa kwa kuapa na wala hauzi isipokuwa kwa kuapa.”

Pamoja na kuwa mtu huyu ni fakiri lakini pamoja na hivyo anafanya kiburi. Tajiri anaweza kufanya kiburi kwa ajili ya mali zake, lakini fakiri huyu hana sababu yoyote ya kufanya kiburi. Hafanyi kiburi isipokuwa ni kwa sababu ni maumbile yake na ni sifa alionayo katika moyo wake.

Katika Hadiyth hii kuna matahadharisho juu ya sifa hizi akiwemo mzee mzinifu. Ni jambo kubwa kwa sababu kijana anaweza kutubia na kuachana na jambo hilo. Lakini huyu mzee hakuna kilichomfanya akaendelea kufanya hivo isipokuwa ni kwa sababu ni jambo limekita kabisa moyoni mwake. Wanachuoni wanasema kuwa Hadiyh hii ni dalili inayoonyesha kwamba dhambi inakuwa kubwa na khatari zaidi pale ambapo mtu anakuwa na uchache na udhaifu wa matamanivu.

4- Imesihi kupokelewa kutoka kwa ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu bora katika Ummah wangu ni wale wa karne yangu, kisha wale watakaowafuatia, kisha wale watakaowafuatia. Kisha baadaye kutakuja watu wanaoshuhudia bila kuombwa kushuhudia, watakuwa makhaini na wala hawatoaminiwa, wanaweka nadhiri na wala hawatekelezi na kutadhihiri kwao unene.”

´Imraan amesema:

“Sikumbuki alisema baada ya karne yangu mara mbili au mara tatu.”

Hata hivyo ni Hadiyth Swahiyh kutoka kwa ´Umar katika “al-Musnad” na Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitaja karne mbili baada ya karne yake:

“Kisha baadaye kutakuja watu wanaoshuhudia bila kuombwa kushuhudia, watakuwa makhaini na wala hawatoaminiwa, wanaweka nadhiri na wala hawatekelezi na kutadhihiri kwao unene.”

Hii ina maana kwamba hali zitabadilika baada ya karne hizi tatu bora. Baada ya hapo kutakuwepo ukhaini, wanavunja nadhiri na wanashuhudia uongo kwa sababu ya udhaifu wa imani zao, ujinga kuenea na makosa mengi.

Ni wajibu kutekeleza nadhiri na ni miongoni mwa sifa za waumini. Hata hivyo nadhiri ni kitu kisichotakikana kwa sababu Hadiyth inasema:

“Hadiyth haileti kheri yoyote. Ni kitu kinachotoka kwa bakhili.”[7]

Lakini akiweka nadhiri njema basi ni lazima aitekeleze. Ama kuhusu nadhiri ya maasi haifai kwake akaitekeleza ingawa ni wajibu kuitolea kafara:

“Kutadhihiri kwao unene.”

Kwa sababu ya kughafilika kwao na kuzama kwao katika neema na matamanio. Lakini haina manaa kwamba kila ambaye ni mnene anatakiwa kuepukwa na ni mtu mbaya. Wanaweza kuwepo watu wanene ambao ni wazuri na wema. Hadiyth inaashiria ughafilikaji na upuuziaji wa kujiandaa na Aakhirah.

5- Amepokea vilevile kutoka kwa  Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Bora ya watu ni wa karne yangu, kisha watakaowafuatia, kisha watakaowafuatia. Halafu watakuja watu ambao ushahidi wao unatangulia viapo vyao na viapo vyao vinatangulia ushahidi wao.”

Hadiyth inawahusu watu wote katika karne ile ambao ni Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Ni watu bora baada ya Mitume. Kisha wale wataokaofuatia ambao ni wanafunzi wa Maswahabah. Kisha wale waliokuja baada ya wanafunzi wa Maswahabah:

“Halafu watakuja watu ambao ushahidi wao unatangulia viapo vyao na viapo vyao vinatangulia ushahidi wao.”

Haya yanatokana na uchache wa kujali kwao na upumbavu kwa sababu ya udhaifu na uchache wa imani.

6- Ibraahiym amesema:

“Pindi tulipokuwa wadogo walikuwa wakitupiga kwa kuapa na kwa kutoa ushahidi.”

Salaf walikuwa wakiwatia adabu watoto wao pindi wanaposhuhudia na kuapa ili wasije wakazowea kufanya hivo na matokeo yake wakaja kushuhudia uongo na wakaingia katika mikataba ya kidhuluma. Mtoto anapozowea tabia kama hii baadaye anapokuwa mkubwa anakuja kuchukulia wepesi. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa Salaf walikuwa wakitilia umuhimu juu ya tabia njema na malezi mema kwa watoto wao. Hili ndio jambo la wajibu kwa kila muislamu.

[1] al-Bukhaariy (2087) na Muslim (1606).

[2] at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (6111). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (3072).

[3] al-Bukhaariy (2651) na Muslim (2535).

[4] al-Bukhaariy (2652) na Muslim (2533).

[5] al-Bukhaariy (6608) na Muslim (1639).

[6] Muslim (106).

[7] al-Bukhaariy (6608) na Muslim (1639).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 171-174
  • Imechapishwa: 14/11/2018