62. Kuamini Qadhwaa´ na Qadar hakupingani na kufanya sababu


Kuamini Qadhwaa´ na Qadar na kufanya sababu ni mambo mawili yasiyopingana. Wewe unachotakiwa ni kuamini anayotaka Allaah huwa na asiyotaka hayawi. Lakini hata hivyo usiache kufanya sababu. Bali unatakiwa kutafuta riziki, kuoa, kufanya biashara na kuhangaika na kutafuta riziki. Usisemi kuwa wewe unategemea Qadhwaa´ na Qadar na kwamba ikiwa kitu kimeshaandikwa kwako basi kitakujia na kama hukuandikiwa nacho hakitokujia. Haya hayasemwi na mtu mwenye akili. Hata wanyama – kwa maumbile yao – wanatoka na kwenda kutafuta riziki. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi ´alayhi wa sallam):

“Lau kweli mngelikuwa mnamtegemea Allaah ukweli wa kumtegemea, basi angalikuruzukuni kama anavyomruzuku ndege: inatoka asubuhi haina kitu na anarudi jioni tumbo limejaa.”[1]

Ndege haibaki kwenye chicha lake. Inaruka na kwenda kutafuta riziki.

Kwa hivyo hakuna mgongano kati ya kuamini Qadhwaa´ na Qadar na kufanya sababu. Wenye kusema hivi ni Jabriyyah.

Lakini pamoja na haya yote sababu haipwekeki katika kuleta natija. Msababishi ni Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hii ni Radd kwa Qadariyyah. Hatupindukii katika kuthibitisha sababu kama walivyofanya Qadariyyah na wala hatupindukii katika kuikanusha kama walivyofanya Jabriyyah. Kufanya sababu ni jambo linalotakikana. Amesema (Ta´ala):

فَابْتَغُوا عِندَ اللَّـهِ الرِّزْقَ

“Basi tafuteni riziki kwa Allaah.” (29:17)

وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ

“Tafuteni kutoka katika fadhila za Allaah.” (62:10)

Allaah ameamrisha swalah, swawm na kufanya mema mbalimbali. Haya ni katika kufanya sababu. Kadhalika amekataza sababu za shari kama kufuru, maasi na machafu.

Kuamini Qadhwaa´ na Qadar haina maana kwamba sasa unatakiwa kuacha kufanya sababu. Unatakiwa kuendelea kutafuta na wakati huo huo kuamini ya kwamba ikiwa Allaah amekuandikia jambo, basi litakujia. Hutojiwa na jambo ilihali umekaa tu. Ni lazima ufanye sababu. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pupia lile lenye kukufaa na umtake msaada Allaah na wala usikate tamaa. Endapo utafikwa na jambo usisemi “lau ningefanya kadhaa ingelikuwa kadhaa na kadhaa”. Badala yake unatakiwa kusema “Allaah ameshakadiria. Anafanya alitakalo.””[2]

Wewe unachotakiwa ni kufanya sababu. Ukifikia natija himdi zote zinamrudilia Allaah, na usipofikia natija mshukuru Allaah na ujisalimishe ya kwamba Allaah alikuwa hakukuandikia jambo hilo. Hadiyth hii iko wazi katika kufanya sababu na kwamba kuamini Qadhwaa´ na Qadar haina maana mtu aache kufanya sababu au kwamba kufanya sababu kunatosheleza katika kuleta natija ya mambo kama wanavyosema Mu´tazilah. Mja hufanya sababu – mema au maasi – na natija inakuwa mikononi mwa Allaah. Yeye ndiye ambaye huzalisha natija na msababishaji wa sababu zinazofanywa.

[1] at-Tirmidhiy (2344), Ibn Maajah (4164), Ahmad (01/30) na wengineo. Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy

[2] Muslim (34) na (2667)