Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

… Mitume Wake …

MAELEZO

Mitume ni wingi wa “Mtume” na maana yake “mjumbe kwa ajili ya kufikisha kitu”. Makusudio hapa ya Mtume maana yake inakuwa “mtu aliyefunuliwa Wahy wa Shari´ah na akaamrisha kuufikisha”.

Mtume wa kwanza alikuwa ni Nuuh na Mtume wa mwisho alikuwa ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama Tulivyomfunulia Nuuh na Manabii baada yake.” (an-Nisaa´ 04 : 163)

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy kumepokelewa kupitia kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) kuhusu Hadiyth ya uombezi:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametaja ya kwamba watu watamwendea Aadam ili awaombee ambapo atawaomba udhuru na kusema: “Nendeni kwa Nuuh. Yeye ndiye Mtume wa kwanza aliyetumwa na Allaah.””[1]

Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa mmoja yeyote miongoni mwa wanamme wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.” (al-Ahzaab 33 : 40)

Hakuna Ummah wowote isipokuwa Allaah aliutumia Mtume na Shari´ah maalum, au Nabii ambaye anateremshiwa Wahy ili aweze kuhuisha Shari´ah iliyokuwa kabla yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ

“Kwa hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah.” (an-Nahl 16 : 36)

وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ

“Hakuna Ummah wowote ule isipokuwa amepita humo mwonyaji.” (Faatwir 35 : 24)

إِنَّا أَنزَلْنَا التَّوْرَاةَ فِيهَا هُدًى وَنُورٌ ۚ يَحْكُمُ بِهَا النَّبِيُّونَ الَّذِينَ أَسْلَمُوا

“Hakika Tumeteremsha Tawraat humo mna uongofu na nuru; ambayo kwayo walihukumu Manabii waliyojisalimisha… ”  (al-Maaidah 05 : 44)

Mitume ni watu walioumbwa na hawana sehemu yoyote katika uola wala uungu. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndio kiongozi wa Mitume na mwenye hadhi ya juu zaidi mbele ya Allaah:

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

“Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa atakavyo Allaah. Na lau ningekuwa naelewa ya ghaibu, basi bila shaka ningelijikithirishia ya kheri na wala lisingelinigusa ovu. Mimi si chochote isipokuwa ni mwonyaji na mbashiriaji kwa watu wanaoamini.” (al-A´raaf 07 : 188)

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّـهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا

”Sema: “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.” Sema: “Hakika hakuna yeyote awezaye kunilinda kutokamana na Allaah na wala sitoweza kupata  mahali pa kukimbilia.” (al-Jinn 72 : 21-22)

Wana sifa kama hizo kama ambazo wanadamu wengine wote wako nazo, kama maradhi, mauti, kiu, kuhitajia chakula, kinywaji na mengineyo. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Ibraahiym (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) wakati alipokuwa anamsifu Mola Wake:

وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِوَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ

“Ambaye ndiye Anayenilisha na kuninywesha. Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye ndiye huniponyesha na ambaye atanifisha kisha atanihuisha.” (ash-Shua´raa’ 26 : 79-81)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ni mtu kama nyinyi. Nasahau kama mnavyosahau. Ninaposahau, basi nikumbusheni.”[2]

Allaah (Ta´ala) amewasifu kama waja Wake pindi alipokuwa anataja nafasi zao za juu na akiwasifu. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Nuuh:

إِنَّهُ كَانَ عَبْدًا شَكُورًا

“Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukurani.” (al-Israa´ 17 : 03)

Vilevile amesema kuhusu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَىٰ عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe muonyaji kwa walimwengu wote.” (al-Furqaan 25 : 01)

Amesema kuhusu Ibraahiym, Ishaaq na Ya´quub (Swalla Allaahu ´alayhim wa salaam):

وَاذْكُرْ عِبَادَنَا إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ أُولِي الْأَيْدِي وَالْأَبْصَارِ إِنَّا أَخْلَصْنَاهُم بِخَالِصَةٍ ذِكْرَى الدَّارِ وَإِنَّهُمْ عِندَنَا لَمِنَ الْمُصْطَفَيْنَ الْأَخْيَارِ

“Na kumbuka waja Wetu Ibraahiym, Ishaaq na Ya’quub, wenye nguvu na utambuzi. Hakika Sisi tumewachagua kwa kuwapa sifa maalum ya ukumbusho wa nyumba na hakika wao Kwetu bila shaka ni miongoni mwa walioteuliwa walio bora kabisa.” (Swaad 38 : 45-47)

Amesema kuhusu ´Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

إِنْ هُوَ إِلَّا عَبْدٌ أَنْعَمْنَا عَلَيْهِ وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ

“Yeye si chochote isipokuwa tu ni mja Tuliyemneemesha na tukamjaalia kuwa ni mfano kwa wana wa israaiyl.”  (az-Zukhruf 43 : 59)

Kuamini Mitume kumekusanya mambo manne:

1- Kuamini kwamba ujumbe wao kutoka kwa Allaah (Ta´ala) ni haki. Yeyote mwenye kupinga ujumbe wa mmoja katika wao, basi atakuwa amepinga wote. Allaah (Ta´ala) amesema:

كَذَّبَتْ قَوْمُ نُوحٍ الْمُرْسَلِينَ

”Watu wa Nuuh walikadhibisha Mitume.” (ash-Shu´araa´ 26 : 105)

Allaah akawafanya ni wenye kuwakanusha Mitume wote, pamoja na kwamba alikuwepo Nuuh peke yake wakati walipomkadhibisha. Kutokana na hili manaswara ambao wamemkadhibisha Muhammad na hawakumfuata wamemkadhibisha pia al-Masiyh bin Maryam. Si wenye kumfuata kwa kumkadhibisha kwao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutomfuata na khaswa kukizingatia kwamba aliwapa bishara ya ujio wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maana pekee wanayopata katika bishara hii njema, ni kwamba yeye ni Mtume wao ambaye atawaokoa wao kutokamana na upotevu na kuwaongoza katika njia iliyonyooka kupitia yeye.

2- Kuamini wale Mitume tunaowajua majina yao. Kwa mfano Muhammad, Ibraahiym, Muusa, ´Iysaa na Nuuh (´alayhim-us-Swalaatu was-Salaam). Mitume hawa watano ndio Mitume wabora kabisa. Allaah (Ta´ala) amewataja sehemu mbili ndani ya Qur-aan. Moja wapo ni katika Suurah “Ahzaab” pale aliposema:

وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ

“Na Tulipochukua kutoka kwa Manabii fungamano yao – na kutoka kwako, kutoka kwa Nuuh, Ibraahiym, Muusa, ‘Iysaa mwana wa Maryam.” (al-Ahzaab 33 : 07)

Ya pili ni katika Suurah “ash-Shuuraa” pale aliposema:

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ

“Amekuwekeeni Shari´ah katika dini yale aliyomuusia kwayo Nuuh na ambayo Tumekuletea Wahy, na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym, Muusa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni dini na wala msifarikiane ndani yake.” (ash-Shuuraa 42 : 13)

Ama kuhusu wale Mitume tusiowajua majina yao, tunatakiwa kuwaamini kwa njia ya jumla. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ

“Kwa hakika Tumewatuma Mtume kabla yako; miongoni mwao wako tuliokusimulia na miongoni mwao wako ambao hatukukusimulia.” (Ghaafir 40 : 78)

3- Kuamini maelezo yaliyosihi kutoka kwao.

4- Kufanyia kazi Shari´ah ya yule Mtume aliyetumizwa kwetu katika wao. Naye si mwingine isipokuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye Mtume wa mwisho. Ametumilizwa kwa watu wote. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Basi Naapa kwa Mola wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasione katika nyoyo zao uzito wowote katika yale uliyohukumu na wajisalimishe ukweli wa kujisalimisha.” (an-Nisaa´ 04 : 65)

Kuamini Mitume kunapelekea katika matunda ikiwa ni pamoja na:

1- Ujuzi wa kujua rehema za Allaah (Ta´ala) na kuwatilia Kwake umuhimu kwa kule kuwatumilizia Mitume. Amewatumia Mitume ili wawaongoze katika njia ya Allaah (Ta´ala) na kuwabainishia namna ya kumwabudu Allaah. Kwa sababu akili ya kibinadamu haiwezi kujitosheleza katika kuweza kutambua jambo hilo.

2- Kumshukuru (Ta´ala) kwa neema hii kubwa.

3- Mapenzi na kuwaadhimisha Mitume (´alayhim-us-Swalaatu was-Salaam). Wasifiwe kwa kiasi wanachostahiki. Kwani wao ni Mitume wa Allaah (Ta´ala) na kwa sababu wanamwabudu, wanafikisha ujumbe Wake na kuwanasihi waja Wake.

Wakaidi waliwakadhibisha Mitume na wakidai kuwa Mitume wa Allaah (Ta´ala) hawawezi kuwa watu. Allaah (Ta´ala) ametaja madai haya na kuyabatilisha pale aliposema:

وَمَا مَنَعَ النَّاسَ أَن يُؤْمِنُوا إِذْ جَاءَهُمُ الْهُدَىٰ إِلَّا أَن قَالُوا أَبَعَثَ اللَّـهُ بَشَرًا رَّسُولًا قُل لَّوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَّسُولًا

“Na hakuna kilichowazuia watu wasiamini kulipowajia uongofu isipokuwa husema: “Je, Allaah ametuma mtu kuwa ni Mtume?” Sema: “Lau ingelikuwa katika ardhi kuna Malaika wanatembea kwa utulivu, basi bila shaka Tungeliwateremshia kutoka mbinguni Malaika kuwa ni Mtume.” (al-Israa´ 17 : 94-95)

Allaah (Ta´ala) akabatilisha madai haya kwamba Mitume ni lazima wawe watu kwa sababu wametumwa kwa watu wa ardhi ambao na wao pia ni watu. Lau watu wa ardhini wangelikuwa ni Malaika, basi Allaah angeliwateremshia kutoka mbinguni Mitume Malaika. Allaah (Ta´ala) amewaeleza wale wenye kuwakadhibisha Mitume kwamba wamesema:

إِنْ أَنتُمْ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا تُرِيدُونَ أَن تَصُدُّونَا عَمَّا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُنَا فَأْتُونَا بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ قَالَتْ لَهُمْ رُسُلُهُمْ إِن نَّحْنُ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَمُنُّ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۖ وَمَا كَانَ لَنَا أَن نَّأْتِيَكُم بِسُلْطَانٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Nyinyi si chochote isipokuwa ni watu kama sisi, mnataka kutuzuia na yale waliyokuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja za wazi. Mtume wao wakawajibu: “Sisi si chochote isipokuwa ni watu kama nyinyi, lakini Allaah anamfadhilisha amtakaye miongoni mwa waja Wake na haikutupasa sisi kukujieni kwa hoja isipokuwa kwa idhini ya Allaah.” (Ibraahiym 14 : 10-11)

[1] al-Bukhaariy (4712), Muslim (194), Ahmad (9589), at-Tirmidhiy (2551) na Ibn Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” (347).

[2] al-Bukhaariy (401), Muslim (572), an-Nasaa´iy (1241) na al-Bayhaqiy (3904).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 95-99
  • Imechapishwa: 01/06/2020