62. Kuamini kuwa Pepo na Moto vipo na hukumu ya anayepinga hayo


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Pepo na Moto vimeumbwa. Vimeshaumbwa, kama ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Nimeingia Pepo na nimeona kasiri.”[1]

“Nimeona Kawthar.”[2]

“Nimetazama Pepo na kuona wakazi wake wengi ni… Nimetazama Moto na kuona wakazi wake wengi ni… “

Mwenye kudai kuwa havijaumbwa anaikadhibisha Qur-aan na Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Siamini kuwa mtu kama huyo anaamini Pepo na Moto.”

MAELEZO

Hii ni bishara njema kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Jana usiku nimeingia Peponi na kuona kasiri ya dhahabu. Karibu yake alikuwepo mwanamke aliyesimama na kutawadha. Nikasema: “Kasiri hii ni ya nani?” Wakasema: “Ni ya mwarabu.” Nikasema: “Mimi ni mwarabu. “Kasiri hii ni ya nani?” Wakasema: “Ni ya mwanaume kutoka Quraysh.” Nikasema: “Mimi ni kutoka Quraysh. Kasiri hii ni ya nani?” Wakasema: “´Umar bin al-Khattwaab.” Nikataka kuingia ndani na kutazama, lakini nikakumbuka wivu wako, ´Umar, nikageuza na kwenda zangu.” Ndipo ´Umar bin al-Khattwaab akaanza kulia na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Hivi kweli nikuone wivu wewe?”[3]

Kinachokusudiwa ni kwamba Pepo tayari ipo hivi sasa na huko nje yake kuna kasiri ya ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo mmoja katika wanawake wa Peponi anatawadha. Haya ameyaona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa macho yake mwenyewe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema vilevile:

“Nimeona Kawthar.”

Hadiyth ni Swahiyh. Ameona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Kawthar na akaona hodhi yake wakati alipokuwa amesimama juu ya mimbari yake na akasema:

“Naiona hivi sasa.”

Kuna dalili nyingi juu ya kwamba Pepo ipo hivi sasa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ

“Hakika amemuona katika uteremko mwingine katika mkunazi wa mpaka wa mwisho. Karibu yake kuna Pepo ya al-Ma´waa.”[4]

Hii ni moja katika dalili ambazo zinawaraddi Mu´tazilah wapotevu wanaosema kuwa si Pepo wala Moto havipo hivi sasa na kwamba vingelikuwepo hivi sasa ingelikuwa haina maana yoyote. Allaah awakebehi wao na akili zao!

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ

“Kimbilieni maghfirah kutoka kwa Mola wenu na Pepo ambayo upana wake ni kama mbingu na ardhi wameandaliwa wale wenye kumcha Allaah.”[5]

Allaah  amewaandalia wale wenye kumcha. Ina maana kwamba imeshaandaliwa. Hii ni moja katika dalili nyingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimetazama Pepo na kuona wakazi wake wengi ni masikini na nimetazama Moto na kuona wakazi wake wengi ni wanawake.”[6]

Allaah (Ta´ala) amesema:

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“Wanadhihirishiwa moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa!”[7]

Kwa hiyo kuna dalili nyingi zinazoonyesha kuwa Pepo na Moto vimeumbwa na vipo. Baadhi zimetajwa na Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) na nyenginezo nimekutajieni nazo hivi sasa.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kudai kuwa havijaumbwa anaikadhibisha Qur-aan na Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Siamini kuwa mtu kama huyo anaamini Pepo na Moto.”

Anaweza kuwa katika wale wapotevu wanaopindisha na wanaofasiri kimakosa. Hao hatuwakufurishi. Anaweza vilevile kuwa mkadhibishaji mzandiki. Huyo ndiye tunayemkufurisha.

[1] al-Bukhaariy (3679).

[2] al-Bukhaariy (4964), Muslim (400) na Abu Ya´laa (3186).

[3] al-Bukhaariy (3242) na Muslim (2395).

[4] 53:13-15

[5] 03:133

[6] al-Bukhaariy (3241) na Muslim (2737).

[7] 40:46

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 442-443
  • Imechapishwa: 08/01/2018